Na Amani Mbwaga, Mufindi- Iringa.
Naibu waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba amefanya ziara ya kutembelea kiwanda cha kuchakata chai Kilima kilichopo chini ya Kampuni ya uzalishaji chai Tanzania (Unilever Tea Tanzania Limited) wilayani Mufindi Mkoani Iringa.
Katika ziara hiyo ameridhishwa na juhudi zinazofanywa na kampuni hiyo za kuendelea kuzalisha chai zaidi na yenye ubora wa hali ya juu kwa kutumia mitambo ya kisasa na pia katika ulimaji wa chai ambapo pia wanatumia umwagiliaji wa mitambo ya kisasa.
Lengo la ziara ya Mhe Naibu Waziri ni kuona shughuli za kilimo cha chai jinsi zinavyofanyika katika wilaya ya mufindi, kukutana na wakulima wa chai na wawekezaji kujua wanafursa gani changamoto gani na wana mikakati gani ya kusonga mbele na kupanua masoko.
“Najua changamoto kubwa katika zao hili ni soko na hasa ukizingatia soko kuu liko Kenya, hivyo ni lazima tuwe na chai bora ili kushindana na chai ya kenya na ya nchi nyingine, lakini pia watu wa utafiti na vyuo vyetu ni lazima vitusaidie kupunguza gharama za uzalishaji ili kupata chai yenye ubora na itakayomnufaisha mkulima” alisema Mhe Mgumba.
Aidha serikali ina mpango wa kufungua soko lake la chai hapa nchini ili kuwavutia wanunuzi ikiwa ni pamoja na kuitangaza nchi lakini pia kuwasaidia wakulima kuuza chai yao kwa tija.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William alisema anajivunia uwepo wa Kampuni ya chai Uniliver katika wilaya yake kwani inamchango mkubwa sana katika wilaya na jamii inyozunguka kampuni hiyo yenye mashamba ya chai na viwanda.
“Uwepo huu unawanufaisha wananchi wa mufindi kwa kupata fursa za ajira lakini pia ni walipaji wazuri wa kodi inayochangia maendeleo ya uchumi wa wilaya na nchi kwa ujumla” alisema Mhe William.
Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya chai Tanzania UNILEVER Bwana Ashton Eastman alimshukuru Mhe Naibu waziri kwa ujio wake na kumweleza baadhi ya mafanikio ikiwemo kuwa na Bwawa kubwa la maji kwa ajili ya umwagiliaji wa chai, uzalishaji wa zao la chai bora, uendeshaji wa viwanda vya kuchakata chai kabla haijaenda sokoni na hivyo kuendana na sera ya viwanda ya nchi.
Aidha alitoa changamoto zinazokabili kampuni hiyo hasa ya ardhi na ubora wa chai kuwa mdogo kutoka kwa wakulima wadogowadogo hali inayopelekea wakulima hao kutonufaika vizuri na kilimo cha chai kisha kupelekea kuhamia shughuli zingine mbali na kilimo hicho.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bwana Theophord Ndunguru alisema changamoto ya bei ya chai ni kubwa kwani huwa inapanda na kushuka kulinganisha na bei ya sokoni.
“Kabla ya mwaka 2011 tulikuwa hatuna mfumo rasmi wa upangaji bei ya majani mabichi ya chai kwa hiyo majadiliano yalikuwa yanakuwa magumu sana, kuanzia mwaka 2012 wadau wa chai na bodi ya chai tuliandaa mfumo rasmi wa kuandaa bei elekezi kwa ajili ya majani ya chai” alisema Bwana Ndunguru.
Ule mfumo umewekwa kwa uwiano ambao majani mabichi ya chai huangaliwa gharama halisi za uzalishaji wa chai za mkulima mdogo, kilo moja ya chai na gharama za mwenye kiwanda katika namna ya kusindika na masoko kisha kupata uwiano.
Akijibu changamoto ya bei za wakulima wanapopeleka chai kiwandani Meneja wa fedha wa UNILEVER Bwana Eliya Jonas alisema “sisi kama Uniliver tunalipa zaidi ya bei ya serikali iliyopangwa, tunalipa Tsh 314 halafu 87 unakuwa na 417 vilevile tunalipa motisha ya ubora wa chai ambayo inaenda kwa Tsh 87 mpaka 125”
Kwa mwaka wa fedha uliopita Unilver ililipa bei kati ya Tsh 411 hadi 523 kwa mkuima wa chai na kuthibitisha hili walitambulika mwaka jana na kikao cha wadau wa chai na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa bodi ya chai amethibitisha hili, waliibuka washindi kwa kuwa walipaji bora wa chai Tanzania na kupata tuzo ya heshima.
Naibu Waziri wa Kilimo akiendelea kupata maelezo ya kilimo cha chai kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa Unilever Tanzania |
Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Kuchakata chai cha Kilima Bwana Abdallah Hamad Kulia akimkaribisha Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mgumba katika kiwanda hicho. |
Bwana Hamad akisalimiana na Msaidizi wa Naibu Waziri Bwana Shija |
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akisaini kitabu cha wageni katiak ofisi ya Meneja mkuu wa Kiwanda cha kuchakata chai cha Kilima |
Maelezo kwa Naibu Waziri yakiendelea |
Baadhi ya Mitambao ndani ya Kiwanda |
Bidhaa ya Chai iliyokwisha chakatwa tayari kupelekwa Sokoni |
Naibu Waziri katikati akiuliza baadhi ya maswali kuhusu upimaji wa chai bora |
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bwana Theophord Ndunguru wa Kwanza Kushoto akimweleza Naibu Waziri wa Kiimo njia nyingine inayotumika kupima ubora wa chai kuwa ni kupitia rangi zake. |
Hili ni eneo lijulikanao kama Boiler ndio chanzo cha joto lanapozalishwa kwa njia ya kuni kwa ajili ya kwenda kukaushia chai inapotoka mashambani. |
Naibu waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akipokea Majani ya chai Grade 1 toka kwa Mkurugenzi Mtendaji mkuu wa Unilever Tanzania yanayozalishwa kiwandani hapo ili kwenda kuijionea ubora wa bidhaa hiyo. |
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhri William nae akipokea Majani Hayo kutoka kwa Bwana Ashton Eastman Mkurugenzi Mkuu Unilever Tea Tanzania Ltd. |
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bwana Ndunguru nae akipokea |
No comments:
Post a Comment