Mkuu wa Wilaya Mufindi akitoa tamko la kukifunga kiwanda cha Wachina cha Evergreen kwa Siku 14 Mafinga Mjini |
Na Amani Mbwaga Mafinga- Iringa.
Ni baada ya mauaji ya mfanyakazi mmoja wa kiwanda hicho kuuwawa
kutokana na kipigo kutoka kwa walinzi wawili ambao ni wamasai na Mchina mmoja katika
eneo la Kinyanambo Mafinga Mjini, Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William leo
amefunga kiwanda cha Wachina kijulikanacho kama Evergreen kinachozalisha Siling
Bodi kwa muda wa siku 14 kutokana na Kifo cha Mfanyakazi wa kiwanda hicho
lakini pia kutokidhi kwa viwango vya ubora wa afya, mazingira na usalama kazini.
Mnamo tarehe 23 Agosti 2018 Marehemu bwana Omari Ibrahim
Chokai aliyekuwa mfanyakazi wa kiwanda hicho cha Evergreen alifariki dunia
baada ya kupokea kipigo hadi kufariki kutoka kwa Walinzi wa kampuni hiyo ambao
mpaka sasa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi katika kituo cha Polisi Mafinga kwa
ajili ya upelelezi zaidi wa tukio hilo.
Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu inasemekana kwamba siku ya
tukio Marehemu na wenzake walikua wakifanya service ya baadhi ya mashine
ikiwemo kubadilisha oil ndipo marehemu alijaribu kuondoka na oil chafu na hapo
ndio walinzi walimwita mwizi kwa kushirikiana na Mchina Mmoja kumpiga hadi
mauti yalipomkuta huku wakifahamu fika kama marehemu huyo ni mfanyakazi wa
kampuni hiyo.
Mmoja wa ndugu wa marehemu Bwana Selemani Boke aliwaambia
waandishi wa habari kwamba baada ya kifo cha ndugu yao tarehe 24 Agosti 2018
walisafirisha mwili wa marehemu hadi Kondoa Irangi na kuuzika, baadae walienda
polisi ili kufahamu kwa kina kuhusu kifo cha ndugu yao ili kuhakikisha kwamba
haki inatendeka.
Bwana Boke alisema familiya imetumia zaidi ya Tsh Milioni 3
na laki 5 lakini uongozi wa kiwanda haujafanya lolote na kila walipokuwa
wakiomba ushirikiano hawakupatiwa hata kidogo ndipo walipoamua kuandika barua
kwa Mkuu wa Wilaya mufindi ili kuona jinsi gani anawasaidia ili haki yao
ipatikane.
Mkuu wa Wilaya Mufindi baada ya kupata malalamiko hayo
alianza kuyafanyia kazi na leo hii alifika kiwandani hapo akiwa na kamati ya
ulinzi na usalama ya wilaya.
Lakini pia alikuwa na wataalamu mbalimbali kutoka NEMC, OSHA, Afisa
Kazi Mkoa, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi TUICO Mkoa wa Iringa na wataalamu
wengine kutoka Halmashauri ya Mji Mafinga ambao walifanya ukaguzi wa kiwanda na
kutoridhika na mazingira ya kiwanda hasa usalama kwa wafanyakazi na mazingira
kutokuwa rafiki.
“Kwa kuzingatia sheria zote za kazi, usalama kazini na sheria
ya mazingira kama wataalamu hawa walivyokwishafanya, Mimi Mkuu wa Wilaya Mufindi
natamka na ninasema kiwanda kinasimama na nakifunga kwa siku 14 wawe
wamerekebisha mapungufu yote yaliyoainishwa na wataalamu na pia ndani ya siku
hizo wawe wamelipa gharama zote za kumsafirisha marehemu mpaka kwao Kondoa
Irangi zinazofikia Milioni 3 na Laki 5”. Alisema Mhe Jamhuri.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kwa uchungu wasipotekeleza hayo
waje hapa wang’oe mitambo yao na kuirudisha china, ni afadhali tubaki na
unyonge wetu kuliko kunyanyaswa ndani ya nchi yetu iliyokwishapata uhuru
haiwezekani.
Wakikamilisha yote hayo wafanyakazi wote wamehakikishiwa kurudi
kazini na asisikie mtumishi hata mmoja anakatwa jina lake wote ni lazima
warudi, “Ili mbegu iote ni lazima kwanza ife ndio inamea vizuri sasa
tumeamua kufa kwa ajili ya maslahi mazuri mbele ya safari” Alisisitiza Mhe
Jamhuri.
Alimaliza kwa kuwataka wafanyakazi kuchukua tamko hilo kama
ni hatua nzuri ya kurekebisha hali ya kazi ili baada ya siku 14 mambo yawe
mazuri.
Kwa upande wake Mratibu wa NEMC Nyanda za Juu Kusini Bwana
Goodlove Mwamsojo alisema toka wamekipa kiwanda hicho cheti cha mazingira kwa
ajili ya kuendesha shuguli zake hawajatekeleza shariti hata moja.
Hivyo kwa mujibu
wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 mazingira ya kiwanda ni hatarishi, hawa watu wanatishia usalama na afya za wafanyakazi
hivyo wamestahili kupigwa faini ambayo haitapungua wala kuzidi Tsh Milioni 50.
“Sisi tutaendelea kufanya kazi wa mujibu wa sheria ya
mazingira na kama kweli wana nia ya kuendeleza uchumi wa nchi hii ni lazima wajali
afya za Watanzania”
alisema Bwana Mwamsojo.
Kwa upande mwingine Msimamizi wa Ofisi ya Wakala wa usalama
na Afya Ofisi ya Kanda nyanda za juu kusini Mbeya Injinia Faston Uswege alisema
sisi kama OSHA tunasimamia sheria namba 5 ya mwaka 2005 ya uslama kazini.
“Watu wa OSHA Walipita mwezi wa 12 mwaka jana na wakatoa
maelekezo ikiwemo kuwapatia vitendea kazi nya kiusalama na mpaka sasa
halijatekelezwa” alisema Bwana Uswege.
Lakini pia suala la vyoo, kulingana na idadi ya wafanyakazi
karibu 400 kutumia idadi ya matundu yaliyopo haiwezekani lakini pia vyoo havina
hadhi ya kwenda kujisaidia na pia suala la maji ya kunywa yanayotumika hapa si
safi na salama lakini mwajiri hajali hata kidogo.
Hatua imechukuliwa na OSHA kukitoza kiwanda hicho faini isiyopungua
wala kuzidi Tsh Milioni 17 lakini pia ametakiwa atoe vitendea kazi kwa
wafanyakazi wote ndani ya siku 14 alizopewa.
Aidha Afisa kazi Mkoa wa Iringa Bwana Daudi Samweli alisema
kiwanda kimekuwa na manyanyaso na hakuna uongozi unaoeleweka kila mchina anayekuja
ni Bosi.
“Kwa kufuata matakwa ya sheria ya kazi na miongozo
mbalimbali ya kisera sisi tunawafikisha mahakamani viongozi wa kiwanda hiki ili
watekeleze mambo tunayowaambia kila siku lakini pia wafanyakazi wenyewe hawana
mikataba na hawataki kutoa, sasa hatutakubali kuona wafanyakazi wananyanyasika
kwa namna yoyote ile" alisema Bwana Samweli.
Katibu wa chama cha wafanyakazi TUICO Mkoa wa Iringa na Njombe Bwana
Karim Bachalla kwa upande wake alisisitiza kwamba Wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi
kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi hii lakini pia nao wawekezaji wafanye
kazi kwa kufuata sheria taratibu na matakwa ya nchi.
HABARI PICHA
Mkuu wa Wilaya Mufindi (Katikati )akitoa maelekezo kwa Wachina Kushoto kwake ni Katibu wa TUICO Mkoa wa Iringa na Njombe Bwana Karim Bachalla |
Ukaguzi wa Kiwanda Ukiendelea |
Mitambo ndani ya Kiwanda cha Evergreen |
Wafanyakazi wakiendelea na kazi wakati wa ukaguzi |
Majadiliano ya Wataalamu Mbalimbali wakiwa katika Ukaguzi wa Kiwanda cha Evergreen |
Mratibu wa NEMC Nyanda za Juu Kusini Bwana Goodlove Mwamsojo (Kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya Mufindi baada ya kumaliza ukaguzi wa kiwanda |
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William Akiongea na Wafanyakazi na Wamiliki wa Kiwanda cha Evergreen kuelezea nia ya Kukifunga kutokana na kutokidhi vigezo. |
Injinia Faston Uswege Kutoka OSHA Nyanda za Juu Kusini akitoa Tamko la Kukitoza Faini kiwanda cha evergreen kwa kwenda kinyume na sheria na taratibu za Afya Mazingira na Usalama Kazini. |
Afisa Kazi Mkoa wa Iringa Bwana Daud Samweli nae akieleza alichokibaini na hatua zitakazochukuliwa |
Katibu wa chama cha wafanyakazi TUICO Mkoa wa Iringa na Njombe Bwana Karim Bachalla kwa upande wake akisisitiza kwamba Wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi |
No comments:
Post a Comment