Monday, December 8, 2014

Tuhakikishe washenzi wote hawarudi madarakani, Uchaguzi Serikali za Mitaa Na Uchaguzi Mkuu 2015: By Denis Mpagaze.


Pale Pombe, tisheti na kofia vinapotuchagulia viongozi, chamoto tunakipata!
Denis Mpagaze
Tunaingia kipipndi cha uchaguzi. Tutaskia mengi. Lakini kubwa zaidi ni zawadi au tuseme takrima. Zawadi zenye kila aina ya sura ya mkono mtupu haulambwi au nipe niupe au muosha huoshwa au atoaye hupokea. Kutoa na kupokea zawadi ni jadi yetu Watanzania.

Mgeni hupokelewa na kukirimiwa anapokuwa na mzigo kichwani, kule kwetu Kigoma tunaita “umugemu”. Kadhalika wanasiasa hutuletea zawadi. Hutuletea kofia, pombe na tisheti. Hakika ni zawadi za kipumbavu na madhara yake huwa nikulia na kusaga meno kwa muda wote waongozapo.

Leo ndugu zangu walimu,mmeteseka vya kutosha, mmepigikika vya kustosha, mmedhulumiwa vya kutosha, wengi wenu malipo ya likizi yamebaki msamiati, gharama za matibabu zimelipwa na Mungu hakika ni malipo ya zawadi za wanasiasa. Mmetuvurugia mfumo mzima wa elimu kwamba mnalipa kisasi kwa mgomo wenu wa kimya kimya bila kujua mnaumiza watoto wenu.

Watoto wa wabaya wenu hawasomi kwenye shule mnazofundisha. Wanasoma “international schools”, shule ambazo ada ya mwanafunzi mmoja ni mshahara wako wa mwaka mzima. Maisha yenu ndugu walimu hayataboreshwa kwa migomo baridi bali kwa kuwaondoa viongozi dhalimu madarakani. Muda ndiyo huu, kama mnataka maisha mema kafanyeni uamuzi wa busara.

Ndugu zangu wakulima, poleni sana kwa yanayowasibu. Mliamini katika kile kibwagizo cha KAMA MNATAKA MALI MTAYAPATA SHAMBANI na kwa moyo wote shambani mkahudhuria. Kimechowapata hata shetani anasikitika. Pembe jeo kwenu imekuwa sawa na kuchoma sindano ya kushonea viraka kwenye kidonda. Mmeingia katika mikopo mikubwa mkitegemea baada ya kuuza basi mlipe mikopo hiyo na nyie kufurahia matunda ya kazi ya mikono yenu. Kimechotokea kimewashangaza wenyewe. Mazao yenu yamekosa soko, madeni yamewabana na sasa wengi mnatamani kufa badala ya kuishi.
 Watoto wenu wamepoteza dira kwa sababu ya usaliti wenu wenyewe kwa kuchagua viongozi balaa. Mliona zawadi ni bora kuliko uzao wenu. Mkawachagua viongozi makenge kwa zawadi ya kofia, pombe na tisheti. Lakini kwa kuwa matatizo ni daraja basi tumieni daraja hilo kuvuka ng’ambo kwa maana ya kwamba achaneni na viongozi waliowatesa kwa muda mrefu. Msiwarudishe madarakani. Muwavuke. Muda ndiyo huu.

Ndugu zangu wafanyabiashara kilio chenu wote tumekisikia. Mmejitahidi kuwekeza katika biashara kwa lengo la kupata faida na kuishi maisha mazuri. Wengine mmechukua mikopo yenye riba kubwa mkiamini kabisa mtarejesha na hatimaye kupiga hatua. Lakini matokeo yake yamewashangaza. Mmelazimishwa kulipa kodi pasipo kupata faida. Mkajikuta mashakani kufilisika. Mkasemeza,
“ Na sasa tuandae mgomo wa nchi nzima kuukataa mfumo huu wa kulipishwa kodi kinyampala”. Harakati zenu zikawa mbio za sakafuni. Mkatiwa msukosuko hatimaye mkasalimu amri. Matokeo yake wengi mmejitoa katika biashara na wengine mmeishia kumlilia Mungu. Msilie, maana hata Mungu mwenyewe kasema mnaangamia kwa kukosa maarifa.
Kuwaondoa madarakani viongozi washenzi ndiyo maarifa yenyewe. Fanyeni hivyo kwa kuwapigia kura za hapana. Muda ndiyo huu. Mnawafahamu. Nendeni mkachague viongozi wenye utu badala ya kujifanya mko “busy”.
Nawajua. Wakati wakulima wenzangu wanauza haki yao ya kupiga kura kwa zawadi ya pombe, tisheti na kofia, wafanyabiashara huwa mnauza haki yenu kwa kujifanya mko “busy” na biashara zenu.

Ndugu zangu wanafunzi hasa wa Elimu ya juu mnanihuzunisha sana kwa jinsi mmevyoishi. Kuanzia mnavyokula mpaka kulala ni majanga. Wengi mnalala “stoo”, wengine mnalala kwenye nyumba zilizokuwa na mabanda ya kuku na mnalazimishwa kulipia kodi kubwa. Katika hili mmekosa mtetezi. Wengi mmeshasahau mlo wa mchana mnaita eti pasi ndefu kufikiria mnaweza kupambana na mziki wa kitabu cha chuo kikuu.
Acheni kujidanganya. Lakini linalonitoa machozi zaidi ni wengi wenu mmetoka familia duni sana kiasi kwamba kamkopo hako hako unakokapata baada ya kutoka jasho tena kwa kuchelewa ugawane na wadogo zako au wazazi wako. Mnatia huruma nyie? Lakini mnashangaza pia. Kwa sababu ya ukata wengi wenu mnamaliza shahada ya kwanza humjawahi kununua kitabu hata kimoja. Kazi kutoa “copies” tu! “Unagraduate” na “box” limejaa “miscopies” tu. Darasa zima kitabu “origino” anacho mwalimu tu. Unapitia mfumo huu goigoi wa elimu na kutegemea kupambana kwenye soko la ajira na mtoto wa kigogo aliyesoma “Oxford University”.

 Saana utaishia kuchekesha wakati wa usaili. Fedheha hii ni malipo ya makosa tuliyoyafanya ya kuchagua viongozi dhalimu. Jitokezeni basi katika chaguzi hizi.

Ndugu zangu machinga, leo hii mnaitwa uchafu na wale wale mliowachagua wakawatete. Mmejaribu kuukataa ushenzi kwa maandamano ya amani lakni cha moto mkakiona. Yaani mlisahau kama nchi yetu ni ya ajabu sana. Yaani maandamano ya amani, watu wanapigwa. Sasa sijui amani ndiyo kipigo? Tunajua wengi mmepoteza mali zenu na kuamua kurudi vijijini kwenda kuwa mafukara kwa sababu mliamini kudai haki zenu kwa maandamano ya amani.

 Labda tu niwakumbushe kwamba hapa nyumbani maandamano ni mwiko ila mnauhuru wa kufanya maamuzi mara moja tu kila baada ya miaka mitano. Na pale mnapokosea ndiyo kilio na kusaga meno vinatokea. Muda ni huu,msirudie kosa. Jitokezeni mkachague viongozi bora. Ni bora kuchagua kiongozi mbovu kuliko kumrudisha kiongozi aliyekutesa kwa kipindi chote hicho!

Ndugu zangu waendesha bodaboda mnafanya kazi nzuri sana ya kurahisisha usafiri nchini lakini mnanyonywa kweli. Kutwa nzima kushinda kwenye makoti makubwa, yenye kujaa kila aina ya vumbi na jasho. Lengo lenu ni kujikwamua katika maisha, lakini kinyume chake mmebaki kuwindwa na askari wa usalama barabarani mithili ya suala na simba nyikani.
Matokeo yake mnakwenda mwendo kasi ili kuwakwepa wabaya wenu na kuishia kuvunjika miguu na kwenda kutaabika mikonoi mwa madaktari waliokata tamaa na maisha! Yote haya ni kwa sababu mlikosea katika uchaguzi ulio pita. Mlichagua makenge mkidhani ni viongozi. Msirudie kosa, waondoeni madarakani waliowaumiza.

Madakatari pamoja na kusoma kwenu kwa miaka mingi, mmeshindwa kuonesha umahiri kwa sababu mazingira ya kazi si rafiki. Mapato yenu yamekwenda tofauti na mategemeo yenu. Matokeo yake mmekuwa wenye hasira kwa wogonjwa. Vinywaji vikali vimekuwa faraja kwa ndugu zangu madaktari. Inasikitisha.
Mmekuwa mkitufundisha kanunu za afya bora huku mkiwa wa kwanza kuzivunja. Eti Daktari mmoja hawezi kufanya upasuaji bila kupata fanta moja ya gongo na fegi mdomoni. Ebo! Msikubali hawa waliowafanya hivi kurudi madarakani.

Ndugu zangu wavuvi huko kanda ya ziwa na kwingineko, poleni kwa kuitwa wanaharamu kwa kutumia nyenzo haramu za uvuvi kami vile nyavu. Unajua mambo mengine yanashangaza. Kwani nyavu hivi zinaingiaje nchini? Si wao wenyewe? Viwanda vya kutengeneza nyavu si vya kwao? Kwa nini asikamatwe anayezitengeneza? Huu ni uonevu. Nvyavu nenu zinachomwa bila fidia. Mnaingia hasara. Maisha mnayaona machungu na cha moto mnakipata. Mwisho mnakata tamaa na kumwachia Mungu. Acheni kumtwika mizigo Mungu wangu. Yote haya mmeyasababisha wenyewe kwa kuchagua viongozi dhalimu. Pengine mateso hayo mnayoyapata ni ishara nzuri kwamba muamke na kusema basi inatosha. Msimu ndiyo huu. Jitokezeni mkachague viongozi bora kwa maisha bora ya wavuvi wote Tanzania.

Kwenu wafugaji. Mmejikuta katika vita kubwa ndani ya nchi yenye amani. Kila kukicha mnamwaga damu huku wenye jukumu la kuwalinda wakitafuna mishikaki ya kuku huku wakiangalia Asernal ikimenyana na Man U. Maisha yenu ya ufugaji yamekuwa magumu. Malisho kwa wanyama wenu imekuwa balaa. Askari wa mbugani wamewafanya nyie vyanzo vyao vya mapano.
 Mnatozwa faini kubwa pasipokupata msaada. Asira yenu ikiwaka mnajikuta katika vita na wakulima. Sikilizeni. Hakuna haja ya kupigana na mkulima. Huyo siyo adui yenu. Adui yenu ni yule aliyewapa tisheti, kofia na pombe mkampa kura. Muondoeni huyo! Muda umefika.

Ndugu zangu waandishi wa habari, poleni kwa adha za kila aina wakati mkitekeleza majukumu yenu ya kila siku. Kwanza mmetukanwa kwamba mu wavivu wa kufikiri. Hiyo haikutosha, mmeendelea kupokea vitisho, vipigo na mpaka wengine kupoteza baadhi ya viungo vyao na hata kufa. Leo ni vilema na wakati hawakuzaliwa hivyo. Wanaotenda yote haya wako pale kwa sababu ya kura zenu. Wamiliki wamendelea kuwatumikisha kana kwamba nyie si lolote si chochote. Kupata kwenu ujira ni mpaka mwajiri wako aone inafaa. .
 Serikali yenu inajua kabisa mnaonewa, sasa kwa kuwa ni mpango wake kuwa na media dhaifu basi mnaishia kulia pasipo msaada. Fanyeni uchaguzi wenye busara na hakika mtapona.

Ndugu zangu watanzania, hakikia tumepigika, tuko katika wakati mgumu. Rasilimali zetu zinatafunwa kwa kasi sana na viongozi tuliowaweka madarakani. Kulindana kwao ndiyo fasheni. Mahakama tuliyonayo ndiyo kabisa haina meno. Kumbe ni wakati muafaka sasa kutorudia kosa.
Tuhakikishe washenzi wote hawarudi madarakani. Msimu ndiyo huu. Tunaanza na serikali za mitaa, na baadaye tutamalizia na uchaguzi mkuu wa rais na wabunge. Chondechonde, tukifanya kosa tutazikwa wazima. Tufanye maamuzi pasipo msukumo wa tisheti, kofia na pombe.