Tuesday, July 16, 2019

Waziri wa Viwanda na Biashara na Mbunge wa Karagwe Mhe. Bashungwa azind...

Waziri Bashungwa Azindua ligi ya Mpira wa Miguu Karagwe


Na Amani Mbwaga,  Karagwe

Waziri wa Viwanda na Biashara ambae pia ni Mbunge wa Jimbo la Karagwe Mkoani Kagera Mhe. Innocent Bashungwa Mapema Wikendi iliyopita amezindua rasmi Mashindano ya ligi ya mpira wa miguu ambayo hufanyika kila mwaka Jimboni kwake na ni maarufu kwa BASHUNGWA KARAGWE CUP.

Akiongea na Wananchi katika kijiji cha Nyakagoyagoye Wilayani Karagwe wakati wa uzinduzi wa ligi hiyo Waziri Bashungwa amesema  wananchi wanapoendelea kuchapa kazi serikali nayo inaendelea kuleta huduma za jamii katika maeneo yote mijini na vijijini.

“Wana Karagwe Chapeni Kazi lakini sisi kwenye huduma za jamii suala la maji mlikuwa mkisikia nikiwa bungeni nazungumzia mradi wa maji mpaka koo linakauka, lakini huo mradi ndugu zangu ni mkubwa sana na uko katika hatua nzuri na hivi ninavyozungumza Waziri wa maji alikuwa hapa Karagwe jana kuhakikisha mradi huo unatekelezwa ipasavyo” alisema

Wakati huo huo Waziri Bashungwa amemshukuru Rais Magufuli kwa kupeleka miradi mingi na mikubwa Wilayani Karagwe ambapo hivi  karibuni tu Zaidi ya Bilioni 70 zitapelekwa tena katika Wilaya hiyo kwa ajili ya kuchochea miradi mingine ya maendeleo.

Mkuu wa Wilaya Karagwe Mhe. Godfrey Mhehuka amempongeza waziri Bashungwa kwa kuchapa kazi na hatimae wana karagwe wanafurahia maendeleo yanayopatikana ktokana na juhudi zake.
“Niemona niseme pongezi zangu kwako, umati huu ni mkubwa sana na unaona ni kwa sababu wewe umeamua kufanya kitu.

Aidha. Mhe Mheuka ameendelea kusema rais hakukosea kumchagua kuwa waziri wa viwanda na biashara hivyo amemuomba akachape kazi na wao wako nyuma yake kuhakikisha anawatumikia vyema wananchi wa Karagwe na Taifa kwa ujumla.

“Niseme neno moja tu, Mungu ametuona, nataka niwape siri hakika mungu amewaona DC Mwenye Waziri Mkoa wa Kagera niko peke yangu ahsanteni sana”alisema Mhe. Mheuka

Kwa mujibu wa mratibu wa mashindano ya BASHUNGWA KARAGWE CUP Bwana Majaliwa Said amesema  Mashindano hayo yameanza tarehe 13 Julai 2019 yakihusisha timu kutoka kata zote 23 za Halmashauri ya Wilaya Karagwe.

Jiogarafia ya karagwe ni kubwa hivyo tumetengeneza kanda mbalimbali ambazo zitakuwa  zinashindana na baadae kuingia katiak 16 bora hadi fainali
HABARI PICHA

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe.Innocent Bashungwa (Kushoto) akifurahia jambo na Mkuu wa Wilaya Karagwe Mhe.Godgrey Mhehuka katikati ni Katibu wa CCM wilaya ya Karagwe Bi. Mary Kananda
Pichani, Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa wa (tatu kushoto) akiwa pamoja na moja ya Timu iliyozindua mchezo wa kwanza wa ligi ya Bashungwa Karagwe Cup





Waamuzi na Ma Kapteni wa Timu

Baadhi ya Wananchi waliofika Kuhudhuria Uzinduzi wa Bashungwa Karagwe Cup Wkifuatilia kwa Makini Mchezo unaoendelea

Mratibu wa Mashindano ya BASHUNGWA KARAGWE CUP Bwana Majaliwa Said akitoa Taarifa ya Mashindano kwa Waziri wa Viwanda na Biashara  (Mbunge Karagwe) 



Wawakilishi wa Timu mbalimbali kutoka katika Kata 23 za Halmashauri ya Wilaya Karagwe wakifurahia Vifaa vya jezi na mipira vulivyotolewa na Waziri Bashungwa  wakati wa Uzinduzi wa Mashindano hayo. (Picha zote na Amani Mbwaga)

Friday, July 5, 2019

Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Bashungwa Afanya ziara katika Viwanda vya nguo na Kutatua kero zao


Na Amani Mbwaga, Dar es salaam
Waziri wa viwanda na Biashara nchini Tanzania Mhe. Innocent Bashungwa Mapema leo hii amefanya ziara katika viwanda vya nguo kikiwemo cha NIDA na kile cha NAMERA vya jijini Dar es salaam.

Akiongea mara baada ya kutembelea viwanda hivyo Mhe. Bashungwa amesema lengo la ziara hiyo ni kupita katika viwanda vyote vya nguo nchini kujua changamoto zao na kisha serikali kuzifanyia kazi na hatimae kuwa na uzalishaji endelevu wa zao la  pamba na kuwanufaisha wakulima.

“Mimi nimekuja hapa kwa ziara mahususi, Wakulima wetu wa pamba wamehamasika sana kulima pamba, Msimu huu wa mwaka 2019 tunategemea kuvuna  zaidi ya Tani Laki 4 za pamba  kutoka tani Laki 220,000 za mwaka jana kwa hiyo tuna pamba za kutosha” alisema  Mhe. Bashungwa.

Aidha amesisitiza kwamba wakulima kwa upande wao wametimiza wajibu wao hivyo ni jukumu la Serikali kupitia wizara ya viwanda na biashara kuwatafutia masoko yenye tija.

“Kwa muda mrefu soko la pamba limekuwa likitegemea mlango mmoja tu, wakati wa enzi za Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere kulikuwa na viwanda vingi vya nguo na vilikuwa vinafanya kazi ipasavyo na kama vyote vingekuwepo basi kusingekuwepo na changamoto ya masoko katika zao la pamba hivyo ni wakati sasa wa viwanda vilivyopo na vitakavyojengwa kuhakikisha vinafanya kazi ipasavyo na Kuongeza Uzalishaji mara mbili zaidi  ili kuendana na kasi ya sasa ya Tanzania ya Viwanda".

Nchi ikifanikiwa kuchakata kila zao na kuliongezea thamani basi itakua ni chachu ya ongezeko la ajira hapa nchini na hatimae kukuza uchumi wa  taifa na wananchi kwa ujumla.

Dira kuu ya Wizara ya Viwanda na Biashara  ni "Kuwa na msingi shindani wa viwanda, mazingira bora ya uwekezaji na ukuaji wa biashara unaowezesha kukua kwa uchumi shirikishi na endelevu."

Waziri Bashungwa ataendelea na ziara hiyo nchi nzima baada ya Kuanza na Mkoa wa Kilimanjaro hapo jana na leo hapa Jijini Dar es salaam.


MATUKIO KATIKA PICHA
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa akiangalia Bidhaa zinazotengenezwa na Kiwanda cha Nguo NIDA Wakati wa ziara yake.
Mhe.Waziri Bashungwa wakati wa Majumuisho ya ziara

Pamba ikiwa katika Hatua za awali za uchakataji

Waziri wa Viwanda na Biashara (Katikati) akipokea maelezo ya namna Pamba inavyoanza kuchakatwa katika hatua za awali




Shughuli za Uzalishaji Kiwandani zikiendelea






Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa (Kulia) akimsikiliza kwa Makini Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Nguo NIDA na NAMERA  (Picha zote na Amani Mbwaga)

Sunday, June 30, 2019

Bodi ya Ushauri ya Wizara kwa TFS Yapongeza Juhudi za Uendelezaji Shamba la Miti Sao Hill Mafinga


Na Amani Mbwaga, Mafinga

Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imefanya ziara hivi karibuni katika Shamba la Miti Sao Hill ikiwa ni lengo la kujitambulisha kwa wajumbe wa bodi hiyo lakini pia kuona shughuli mbalimbali zinazosimamiwa na Wakala.


Akiongoza wajumbe wa Bodi hiyo Bi. Piencia Kiure  mara baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi  Shamba la Miti Sao Hill na kutembelea baadhi ya miradi na amepongeza juhudi hizo na kusema toka ameanza ziara hiyo katika maeneo mbalimbali ya Nyanda za Juu Kusini lakini Shamba la Miti Sao Hill ni mfano wa kuigwa kwa utendaji bora na  uliotukuka.

“Nimefurahi sana taarifa zenu ni nzuri sana na pia nimeona jinsi mnavyotekeleza suala la wajibu kwa jamii yaani Corporate Social Responsibility (CSR) ikiwepo kutenga fedha kwenye bajeti yenu katika miradi ya maendeleo vijijini hapa mmenikuna zaidi kwani na mie ni mdau mkubwa sana wa (CSR) Na kwa kufanya hivyo kunasaidia sana kuwa na mahusiano mazuri baina yenu na jamii inayozunguka shamba hongereni sana”.

Kwa upande mwingine Bi. Kiure ameitaka Shamba la Miti Sao Hill Kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Kuendelea na juhudi za Ujenzi wa Viwanda hasa vya  mazao ya nyuki kwani shamba hilo limefanikiwa sana katika shughuli za ufugaji nyuki na kuwa na vifaa vya kisasa vya ufugaji nyuki na vile vya kuchakatia mazao hayo.

“Sisi kama bodi tunaona Sao Hill  mna uwezo huo na tunasisitiza zaidi kuwa na viwanda hivyo kwani nia mnayo uwezo mnao na nguvu mnazo za kutekeleza agizo hilo mkisaidiana na viongozi wenu kutoka TFS Makao makuu  hili litasaidia sana hata wale wafugaji wadogo wadogo kuinuka na hatimae kuwa na kipato cha kutosha kisha kuchangia uchumi wa Taifa”.

Aidha amewataka watumishi wote wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuongeza kuboresha utendaji kazi zaidi ili kuongeza mapato na kusaidia kukua kwa uchumi wa nchi na hii inatokana na kipindi kilichopo ambapo nchi imeamua kuja na mpango wa kujitegemea zaidi  na kupunguza misaada kutoka nje kutoka asilimia 42% hadi sasa kufikia asilimia 8% ili kuweza kujiendesha wenyewe kwa mapato ya ndani.

Mkurugenzi wa Usimamizi  Rasilimali za Misitu na Nyuki TFS Bw. Zawadi  Mbwambo amewataka watumishi wote kuendelea na juhudi kufanya kazi kwa bidii na   kuendeleza misitu kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

“Nashukuku Sao Hill na TFS kwa ujumla tunaenda vizuri na ndio maana hata bungeni kwa kipindi hiki hakuna maswali mengi bungeni tayari tumeshawarahisishia kazi mawaziri wetu zaidi tunaendelea kupokea pongezi hivyo tusibweteke na sifa hizo bali tuongeze bidii za kufanya kazi kwa Uhodari ushirikiano na kwa weledi wa hali ya juu kwa manufaa ya Taifa letu”

Kwa Upande wake Meneja Shamba la Miti Sao Hill Bw. Heriberth Haulle amesema uwepo wa Shamba la Miti Sao Hill umekuwa mkombozi mkubwa kwa uchumi wa wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Iringa kwa ujumla na kumekuwa na mahusiano mazuri baina ya shamba na wananchi wanaozunguka shamba.

Aidha shamba limekuwa likichangia sana katika shughuli za maendeleo katika vijiji vyote vinavyozunguka shamba  mfano kupitia ukatishaji wa leseni za kufanya shughuli za uchakataji mazao ya misitu kwa umoja wa wadau wa mazao hayo wamekuwa wakichangia 2% ya leseni hizo na mapato yanayopatika hupelekwa katika Halmashauri zinazozungukwa na msitu  ili kuchochea shughuli za maendeleo vijijini kulingana na vipaumbele vyao.

“Mpaka kufikia mwezi mei mwaka huu 2019 tumekusanya zaidi ya Milioni 315 kama mpango wa wavunaji kuchangia shughuli za maendeleo vijijini na tayari fedha hizo zilishapelekwa katika Halmashauri zinazozungukwa na shamba letu”

Mbali na hilo pia Shamba la Miti Sao Hill katika Bajeti ya mwaka 2019/2020 imetenga zaidi ya milioni 172 kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii hususani kujenga mabweni 02 ya Wasichana katika shule za sekondari na huu pia ni mchango wa shamba kwa jamii.

Akitoa neno la shukrani Kaimu Meneja wa TFS Nyanda za juu Kusini Bw. Ebrantino Mginje amesema maelekezo na ushauri uliotolewa na bodi kwa ziara nzima umechukuliwa na tayari hatua za utekelezaji zinaanza mara moja ili kuwa na misitu endelevu kwa faida ya sasa na baadae.

Bodi hii ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS ilizinduliwa rasmi machi 9 mwaka 2019 Jijini Mwanza na Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Dkt. Hamisi Kigwangalla na inaongozwa na Mwenyekiti wake Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy.

MATUKIO KATIKA PICHA
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara Kwa  Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS        Bi. Piencia Kiure akitoa maelekezo kwa Watumishi wa TFS Shamba la Miti Sao Hill (Hawapo pichani)



Mkurugenzi wa Usimamiziwa rasilimali za Misitu na Nyuki TFS  Bw. Zawadi Mbwambo akieleza namna Miti aina ya Mkaratusi (Eucalyptus) inavyoandaliwa
Meneja Shamba la Miti Sao Hill Bw. Herbeth Haulle akieleza jambo 
Meneja Tarafa ya I Irundi Shamba la Miti Sao Hill Bi. Glory Fortunatus akitoa maelezo ya Bustani ya Miche Irundi wakati Bodi ya Ushauri ilipotembelea eneo hilo




(Picha zote na Amani Mbwaga)



Thursday, March 21, 2019

Shamba la Miti Sao Hill Laadhimisha Siku ya Kimataifa ya Misitu Duniani na Kugawa Miche ya Miti Takribani Milioni 1 Kwa Wananchi Buree.



Na Amani Mbwaga, Mafinga.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Shamba la miti Sao Hill limeungana na taasisi nyingine duniani katika kuadhimisha siku ya misitu duniani ambayo hufanyika Tarehe 21 Machi ya kila mwaka.

Katika madhimisho ya mwaka huu shamba la miti Sao Hill limewapatia wananchi na Taasisi mbalimbali za serikali na binafsi Miche takribani Milioni Moja ya miti aina ya Msindano (Pine) kwa lengo la kuongeza kasi ya upandaji wa miti kila mwaka ili kurahisisha upatikanaji wa malighafi ya mazao ya misitu viwandani kwa dhumuni la kuunga mkono serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli ya kuwa na Tanzania ya Viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Meneja Shamba la Miti Sao Hill Bwana Herberth Haulle akiongea na waandishi wa habari ofsini kwake ameeleza namna sekta ya misitu nchini inavyochangia katika kutoa malighafi ya viwanda vya Karatasi, Mbao, Nguzo, viberiti, chai (Kukaushia-chai) nk.

Viwanda vipatavyo elfu saba huwasilisha uhitaji wa malighafi katika mashamba ya miti yanayomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, 81.2% ya viwanda hivi vinaonesha uhitaji wa malighafi kutoka eneo tengefu la Saohill.

Saohill inahudumia 71% ya viwanda vinavyohudimiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupitia mashamba ya miti.

Viwanda hivi vilionesha kuhitaji jumla ya meta za ujazo milioni 22,439, 489 kwa Sao hill pekee viwanda vilionesha uhitaji wa meta za ujazo milioni 18 hii ni asilimia 84.3%,  Ambapo malighafi iliyotolewa (uwezo wa mashamba) ni asilimia 5 tu ya malighafi iliyohitajika kwa  viwanda.

Uwezo wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kutoa malighafi kwa viwanda ni mita za ujazo millioni moja kwa mwaka ambapo Saohill hutoa 83.8% ya malighafi husika.


Chanzo cha mapato ya serikali (TFS) kwa zaidi ya nusu ya makusanyo yanayo fanywa na TFS ni makusanyo kutoka Shamba la Miti Sao hill. 
Misitu huchangia pia katika upatikanaji wa hali nzuri ya hewa na utunzaji wa vyanzo vya maji ya kutumia binadamu na mengine kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme, mfano bwawa la Kihansi na Mto Ruaha unaopeleka maji yake katika mradi mpya wa umeme Rufiji (Stigler’s Gorge).

Aidha bwana Haulle ameeleza pia namna sekta ya misitu kupitia shamba la miti Sao Hill linavyochangia katika uchumi wa wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa, Taifa na dunia kwa ujumla.

“Shamba limekua likichangia asilimia tano 5% ya mrabaha wa mauzo ya miti  (CESS) kwa mujibu wa sheria kwa Halmashauri zinazozungukwa na Shamba la Miti Sao Hill ambazo ni  Mufindi, Kilombero na Halmashauri ya Mji Mafinga ambapo kwa kipindi cha mwaka 2010/2011 hadi disemba 2018 kiasi cha Zaidi ya Bilioni 6 kilikusanywa kama CESS na kukabidhiwa kwa halmashauri husikakwa ajili ya shughuli za maendeleo” alisema.

Aidha shamba la miti Sao Hill huajiri vibarua wa kutwa Zaidi ya Elfu tatu 3000 kwa mwaka katika kazi mbalimbali za shamba na wengi wao ni wakazi wanaozungukwa na shamba hilo.

Akiongea katika Kipindi maalumu cha utoaji elimu kwa umma leo hii kuhusu siku ya Kimataifa ya  Misitu duniani katika kituo cha redio Ebony fm MKoani Iringa Meneja Msaidizi Mipango na Matumizi wa Shamba la Miti Sao Hill  Bwana Ignas Lupala ameeleza chimbuko kubwa la misitu Tanzania na hatimae hadi kuanzishwa kwa shamba la miti Sao Hill.

Kwa kuzingatia taarifa ya tathimini ya rasilimali ya misitu iliyofanyika nchini kati mwaka 2010 – 2013, inaonesha kuwa misitu inakadiriwa kufikia eneo la hekta milioni 48.1, sawa na asilimia 55 ya eneo la ardhi la Tanzania Bara lenye hekta millioni 88 (TFS, 2015).

Kati ya eneo hilo, asilimia 93 ni misitu ya mataji wazi (woodlands), wakati sehemu inayobaki inajumuisha misitu   ya lindimaji, mikoko, misitu ya pwani (coastal forests), na mashamba ya miti.

Misitu ya kupandwa ni hekta 572,000 ambayo inajumuisha yale yanayomilikiwa na serikali, watu na makampuni binafsi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, mahitaji ya mazao ya misitu yalikadiriwa kuwa ni meta za ujazo milioni 62.3 kwa mwaka huku wakati uwezo wa misitu kutoa mahitahiji hayo kwa njia endelevu ukiwa meta za ujazo milioni 42.8.

Hivyo, kuwepo na upungufu wa meta za ujazo milioni 19.5 kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama nishati (kuni na mkaa), nguzo za umeme pamoja na mbao kwa ajili ya ujenzi.

Upungufu huo umekuwa kichocheo cha uvunaji haramu katika misitu ya asili ambao husababisha uharibifu na upotevu wa misitu hiyo.
Katika jitihada za kuongeza upatikanaji wa Malighafi ya miti Ili kukabiliana na upungufu wa malighafi/ mazao ya misitu, serikali ilianzisha mashamba ya miti (forest plantations) katika maeneo mbalimbali.

Lengo ni kupunguza utegemezi wa mazao ya misitu kutoka katika misitu ya asili ili kuhifadhi mazingira na baionuai.
Kwa sasa serikali inamiliki mashamba 24 yanayopatikana maeneo mbalimbali nchini.

Mashamba hayo yana jumla hekta 306,980.20 na kusimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Kati ya hekta hizo, jumla ya hekta 105,583.56 sawa na asilimia 34 ya eneo la mashamba hayo zimepandwa miti.

Maeneo mengine yamehifadhiwa kwa ajili ya vyanzo vya maji na mengine yanaendelea kupandwa kulinganga na mipango ya usimamizi wa mashamba husika.

Shamba la Miti Sao Hill ni miongoni mwa mashamba 24 ya miti ya kupandwa ya serikali ambayo yanasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii Kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)

Shamba hili kwa sehemu kubwa lipo katika wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa na eneo dogo lipo katika Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro
Shamba hili lilianzishwa kwa majaribio mnamo mwaka 1939 hadi 1951 na upandaji wa miti kwa kiwango kikubwa ulianza rasmi kuanzia miaka ya 1960 hadi 1980.

Aidha shamba hili ndilo shamba kubwa kuliko mashamba yote 24 ya serikali ambapo kwa sasa lina ukubwa wa hekta laki moja na thelathini na tano elfu mia tisa na tatu 135,903.

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya misitu duniani kila mwaka, nchi mbalimbali duniani zinahamasishwa kuendeleza juhudi za kitaifa na kimataifa ili kuandaa na kushiriki katika shughuli zinazohusika na misitu pamoja na miti, kama vile kampeni ya kupanda miti pamoja na midahalo kuhusu misitu.

Siku hii huadhimishwa kwa ajili ya kuwafanya watu waelewe umuhimu wa aina zote za misitu duniani, ikiwemo jukumu lake katika mabadiliko ya tabia nchi.

Siku hii ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2012 na siku hiyo ilisherehekewa kwa mara ya kwanza Machi 21, 2013.

Makala hii Maalumu Imeandaliwa na Amani Mbwaga kwa kushirikiana na Kitengo cha Uenezi na Ugani katika Ofisi ya Habari na Mawasiliano TFS- Shamba la Miti Sao Hill
Tarehe 21 Machi 2019.
Mob+255 656 632 566
E-mail:prof.mbwaga@gmail.com

HABARI PICHA


Meneja Shamba la Miti Sao Hill Bwana Heriberth Haulle


Baadhi ya Miche ya Miti ya Msindano (Pines) Iliyopandwa Msimu huu katika Shamba la Miti Sao Hill na Mingine Kugawiwa kwa Wananchi bure
Daniel Silima Meneja Msaidizi Rasilimali za Misitu Shamba la Miti Sao Hill


 


Ignas Lupala Meneja Msaidizi Mipango na Matumizi Shamba la Miti Sao Hill Mapema Leo hii akitoa Elimu kwa umma kwa njia ya Redio kuhusu chimbuko la Misitu Nchini na Faida za uwepo wa Shamba la Miti Sao Hill katika kituo cha EBONY FM RADIO Mapema leo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Misitu Duniani (Picha  na Amani Mbwaga)

(Picha zote na Amani Mbwaga)

Sunday, February 17, 2019

Mbunge Chumi Akabidhi Magari 02 Bure kwa Idara ya Elimu Mafinga



Na Amani Mbwaga, Mafinga.
Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Mhe. Cosato Chumi Mapema wiki hii amekabidhi Magari idadi mawili kwa Idara ya elimu katika Halmashauri ya Mji Mafinga kwa lengo la kuongeza nguvu ya ufuatiliaji wa masuala ya elimu ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa Jimbo la Mafinga Mjini na Taifa kwa ujumla.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika viwanja vya Teachers Resource Centre (TRC Mafinga) wakati wa mkutano wa tathimini ya Elimu kwa Halmashauri ya Mji Mafinga ambapo umewakutanisha takribani waalimu wakuu wa shule zote za Sekondari na Msingi, Maafisa Elmu kata, Wilaya na Wataalamu wengine wote wa Sekta ya Elimu Mjini Mafinga.

Akiongea na Wataalamu hao wa elimu Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Mhe. Cosato Chumi ameelezea hisia zake juu ya umuhimu wa elimu kwa wananchi wa Jimbo lake na taifa kwa ujumla.
“Mimi naamini kwamba elimu ndio kila kitu bila elimu tusingekuwa hapa kwa hiyo tunapokaa kufanya tathimini ya elimu tunapanga ili kuboresha elimu ya watoto wetu” alisema

Aidha ameeleza kuwa Halmashauri ya mji mafinga bado ni changa na ilianzishwa hivi karibuni kwa hiyo idara nyingi zina uhaba wa magari kwa hiyo yeye kama mbunge ameamua kujiongeza kutafuta wadau wakamsaidia magari hayo mawili ambayo ameyakabidhi kwa idara ya elimu Msingi na Sekondari.

Kwa Mujibu wa Mhe. Chumi amesema kwamba magari hayo amepewa na Kamishina wa Ushuru na Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kumsumbua sana ili amsaidie magari kwa ajili ya idara za halmashauri yake na ndipo kamishina huyo akampatia magari hayo na leo ameikabidhi Halmshauri Kupitia Mkuu wa Wilaya Mufindi na baade kumkabidhi Mwenyekiti wa Halmashari ya Mji Mafinga tayari kwa matumizi ya kiserikali hususani idara ya elimu.

Akitoa shukrani kwa Mbunge huyo Mgeni wa rasmi wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William amempongeza Mhe. Chumi kwa kulipigania jimbo la Mafinga mjini katika kuhakikisha maendleo yanapatikana kwani amekuwa msaada mkubwa sana.

“Leo hii tumepokea magari mazuri halafu mapya kabisa yaliyotokana na jitihada za mbunge wetu Chumi, mimi kipekee nakushukuru sana naomba upeleke shukrani na salamu zetu kama Wilaya kwa wadau wote waliojitolea upatikanaji wa magari haya” alisema

Mhe. William amemhakikishia Mhe. Mbunge Chumi kuwa magari hayo yatatunzwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu zote za utunzaji wa magari ya serikali na kutumika kwa shughuli za serikali hususani shughuli za elimu tu.

Hapo awali kulikuwa kunachangamoto ya shule nyingi kutofanyiwa ukaguzi na idara ya udhibiti ubora  elimu kutokana na ukosefu na uhaba wa usafiri sasa kupatikana kwa magari haya ni wakati muafaka wa kuhakikisha hakuna tena tatizo la ufuatiliaji wa elimu Mafinga Mjini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe. Charles Makoga amesema Mhe. Mbunge Chumi amekuwa akisaidia sana katika upatikanaji wa vifaa mbalimbali toka ameingia ubunge kwa muda mfupi amechangia upatikanaji wa magari ya kubebea Wagonjwa (Ambulance) takribani manne sasa katika Halmshauri hiyo lakini pia alipigani pia kupatikana kwa gari la TASAF na la udhibiti ubora yote mapya ambayo yamepatikana pia hivi karibuni.

“Mhe Mbunge mimi nikushukuru sana na mungu akubariki sana kwa upendo wako mkubwa kwa wananchi wa Mafinga kama Mungu hua anapunguza miaka basi kwangu apunguze miwili tu akuongezee wewe” alisema Mhe. Makoga.

Akieleza lengo la tathimini ya elimu ya mwaka 2018 hasa katika matokeo ya mitihani ya kitaifa Kaimu Mkurugenzi na Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Voster Mgina amesema tathimini hiyo itachangia kupanga mipango madhubuti ya mwaka 2019.

Matokeo ya mitihani ya Taifa kwa mwaka 2018 Halmashauri ya Mji Mafinga ilifanya vizuri sana katika mitihani yote.
Mtihani wa darasa la saba Halmashauri ya Mji Mafinga iliweza kufaulisha kwa kiwango cha asilimia 92.86%

Mtihani wa Kidato cha pili ufaulu ulikuwa wa kiwango cha asilimia 96% na kidato cha nne ufaulu ulikuwa wa kiwango cha asilimia 87 wakati huo mwaka jana ufaulu ulikuwa asilimia 73% lakini mwaka huu shule zote zimepandisha ufaulu  na zimeweza kupunguza daraja 0 kutoka 350 hadi 176.

Aidha kidato cha sita kwa matokeo ya mwaka 2018 Halmashauri ya Mji Mafinga iliweza kufaulisha kwa kiwango cha asilimia 100% na hakukua na mwanafunzi aliyepata daraja la 0 wala daraja la IV  kwa shule zote za serikali na binafsi.

 Kaimu Mkurugenzi bwana Mgina amemhakikishia Mhe. Mbunge Chumi kwamba baada ya kupata usafiri huo sasa unaenda kuongeza chachu ya ufuatiliaji wa elimu na kumuahidi kwamba Halmashauri inaenda kufanya vizuri zaidi katika matokeo yajayo ya mitihani ya Taifa.

 HABARI PICHA


Magari aliyoyatoa Mbunge wa Mafinga Mjini Mhe Cosato Chumi kwa Idara za Elimu Mafinga Mji


Mhe. Charles Makoga akitoa Shukrani

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe Charles Makoga akimkabidhi Fungua Kaimu Mkurugenzi na Afisa Elimu Sekondari Bwana Voster Mgina mara baada ya kukabidhiwa na Mbunge Cosato Chumi (Picha zote na Amani Mbwaga)