WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ameingia katika mgogoro mwingine wa uzembe wa matumizi ya ulimi. Hilo lilitokea juzi katika ukumbi wa Classic Ubungo Plaza mbele ya viongozi wa dini kutoka kote nchini ambapo waziri huyo alikuwa akiwahutubia viongozi hao kuhusiana na sekta nzima ya madini na rasilimali za nchi. Kongamano hilo liliandaliwa na Kamati ya Kudumu ya viongozi wa dini inayojishughulisha na utetezi wa rasilimali za nchi na haki za wananchi.

Viongozi waliohudhuria walitoka Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata), Tume ya Kikristo Tanzania (CCT) na Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) pamoja na asasi za kiraia za haki madini, Policy Furum, Norwegian Church Aid, Ongea na wawakilishi wa taasisi za elimu ya juu hapa nchini.


Kauli ya Askofu Benson mwenyekiti wa mkutano

Mwenyekiti wa mkutano huo, Askofu Benson Bagonza wa Dayosisi ya Karagwe, katika ufunguzi, alimweleza Muhongo kuwa licha ya uwekezaji mkubwa katika uvunaji wa rasilimali za madini, wananchi wanaoishi katika maeneo ya migodi ni maskini wa kutupwa. Alisema kuwa haki zao za kibinadamu haziheshimiwi na mazingira yameharibiwa sana huku akirudia wito wa kamati yake kuitaka serikali kuweka wazi mikataba ya madini na kuondokana na usiri unaoghubika sekta hiyo.


Majibu na matusi toka kwa Waziri Muhongo kwa maaskofu na watanzania

Akijibu hotuba hiyo waziri huyo alikanusha vikali akisema mikataba yote ya madini iko wazi na kwamba ilipelekwa kwenye ofisi ya Spika ili wabunge waweze kuisoma lakini cha ajabu wabunge hao wameshindwa kuisoma huku wakiendelea kulalamika kama ilivyo kwa Watanzania wengi.


Akionekana kutamba na kujigamba mbele ya viongozi hao, Prof. Muhongo alisema Watanzania ni wavivu wa kufikiri, wavivu wa kusoma na washamba sana katika masuala ya uwekezaji. Aliwalaumu watu mbalimbali mara kadhaa bila kuwataja majina kuwa wanapenda kutumia ‘vihela’ vya familia zao kudai wapendelewe kupewa vitalu vya gesi huko Mtwara lakini akasema chini ya uongozi wake hilo halitatokea.


“Hawa wanaodai wapendelewe kwa kuwa ni wazawa, wakiishatajirika watasababisha vita kwa sababu watu maskini hawatavumilia kuona matajiri wakineemeka wakati wao ni maskini wa kutupwa,” alisema.

Katika hotuba yake iliyochukua masaa mawili, Prof. Muhogo aliendelea kutumia maneno kama ‘kukurupuka’, ‘upuuzi’, ‘ushamba’, ‘uzushi’, “non performers” na mara kadhaa alionekana kuwaponda Watanzania kuwa hawasomi ndio maana wanaishia kulalamika kila kukicha.

Askofu Oscar wa Newala/Mtwara ampa wakati mgumu Muhongo

Ndipo katika kipindi cha maswali na majibu alipokumbana na hasira ya wanakongamano ambapo wa kwanza alikuwa ni Askofu Oscar Mn’unga wa Dayosisi ya Newala na Mtwara. Askofu huyo alimwambia Waziri Muhongo kuwa ana lugha za kibabe na dharau kwa Watanzania.

“Umekuja umejihami na ubabe wako lakini ujue wananchi wa Mtwara si wajinga tena hata kama wako kimya,” alisema askofu huku akishangiliwa kwa vigelegele.


Mwenyekiti wa mkutano ampa Muhongo ushauri wa busara

Mwenyekiti wa mkutano, Askofu Bagonza, kwa kutumia hekima kubwa alimshauri Muhogo kuazima hekima na uzoefu wa viongozi wa dini.

“Ukiona mtu anakuja kwako akiwa peke yake ujue mtu huyo ana matatizo; lakini ukiona kundi la wawili au watatu wanakuja kwako kiongozi, uwe na uhakika kuwa una matatizo na uwasikilize,” alisisitiza Askofu Bagonza.

Askofu huyo aliendelea kumshauri waziri kuelewa kuwa viongozi wa dini wana wajibu wa zaidi ya kulinda kundi lisishambuliwe na mbwa mwitu na kwamba ni wajibu wao pia kuwaonyesha watawala vichaka vyenye mbwa mwitu katika sekta ya madini.

Profesa Muhongo alipopwaya kuendekeza ubabe

Kilele cha malumbano kati ya Waziri Muhogo na Askofu Oscar kilifika pale askofu huyo alipoituhumu serikali kwa kushusha mabomba ya gesi katika bandari ya Dar es Salaam badala ya Mtwara.

Alisema hatua hiyo ilisababisha yasombwe na malori yanayoharibu barabara zao, kauli iliyomwinua Waziri Muhogo na kumwita askofu huyo kuwa ni mwongo.

“Huo ni uwongo na aibu kwa askofu kusema uwongo,” alisema waziri kisha akaongeza:

“Mimi siendi kanisani mara kwa mara lakini sisemi uongo kama watu wanaoenda kanisani kila siku.”