Sunday, February 17, 2019

Mbunge Chumi Akabidhi Magari 02 Bure kwa Idara ya Elimu Mafinga



Na Amani Mbwaga, Mafinga.
Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Mhe. Cosato Chumi Mapema wiki hii amekabidhi Magari idadi mawili kwa Idara ya elimu katika Halmashauri ya Mji Mafinga kwa lengo la kuongeza nguvu ya ufuatiliaji wa masuala ya elimu ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa Jimbo la Mafinga Mjini na Taifa kwa ujumla.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika viwanja vya Teachers Resource Centre (TRC Mafinga) wakati wa mkutano wa tathimini ya Elimu kwa Halmashauri ya Mji Mafinga ambapo umewakutanisha takribani waalimu wakuu wa shule zote za Sekondari na Msingi, Maafisa Elmu kata, Wilaya na Wataalamu wengine wote wa Sekta ya Elimu Mjini Mafinga.

Akiongea na Wataalamu hao wa elimu Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Mhe. Cosato Chumi ameelezea hisia zake juu ya umuhimu wa elimu kwa wananchi wa Jimbo lake na taifa kwa ujumla.
“Mimi naamini kwamba elimu ndio kila kitu bila elimu tusingekuwa hapa kwa hiyo tunapokaa kufanya tathimini ya elimu tunapanga ili kuboresha elimu ya watoto wetu” alisema

Aidha ameeleza kuwa Halmashauri ya mji mafinga bado ni changa na ilianzishwa hivi karibuni kwa hiyo idara nyingi zina uhaba wa magari kwa hiyo yeye kama mbunge ameamua kujiongeza kutafuta wadau wakamsaidia magari hayo mawili ambayo ameyakabidhi kwa idara ya elimu Msingi na Sekondari.

Kwa Mujibu wa Mhe. Chumi amesema kwamba magari hayo amepewa na Kamishina wa Ushuru na Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kumsumbua sana ili amsaidie magari kwa ajili ya idara za halmashauri yake na ndipo kamishina huyo akampatia magari hayo na leo ameikabidhi Halmshauri Kupitia Mkuu wa Wilaya Mufindi na baade kumkabidhi Mwenyekiti wa Halmashari ya Mji Mafinga tayari kwa matumizi ya kiserikali hususani idara ya elimu.

Akitoa shukrani kwa Mbunge huyo Mgeni wa rasmi wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William amempongeza Mhe. Chumi kwa kulipigania jimbo la Mafinga mjini katika kuhakikisha maendleo yanapatikana kwani amekuwa msaada mkubwa sana.

“Leo hii tumepokea magari mazuri halafu mapya kabisa yaliyotokana na jitihada za mbunge wetu Chumi, mimi kipekee nakushukuru sana naomba upeleke shukrani na salamu zetu kama Wilaya kwa wadau wote waliojitolea upatikanaji wa magari haya” alisema

Mhe. William amemhakikishia Mhe. Mbunge Chumi kuwa magari hayo yatatunzwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu zote za utunzaji wa magari ya serikali na kutumika kwa shughuli za serikali hususani shughuli za elimu tu.

Hapo awali kulikuwa kunachangamoto ya shule nyingi kutofanyiwa ukaguzi na idara ya udhibiti ubora  elimu kutokana na ukosefu na uhaba wa usafiri sasa kupatikana kwa magari haya ni wakati muafaka wa kuhakikisha hakuna tena tatizo la ufuatiliaji wa elimu Mafinga Mjini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe. Charles Makoga amesema Mhe. Mbunge Chumi amekuwa akisaidia sana katika upatikanaji wa vifaa mbalimbali toka ameingia ubunge kwa muda mfupi amechangia upatikanaji wa magari ya kubebea Wagonjwa (Ambulance) takribani manne sasa katika Halmshauri hiyo lakini pia alipigani pia kupatikana kwa gari la TASAF na la udhibiti ubora yote mapya ambayo yamepatikana pia hivi karibuni.

“Mhe Mbunge mimi nikushukuru sana na mungu akubariki sana kwa upendo wako mkubwa kwa wananchi wa Mafinga kama Mungu hua anapunguza miaka basi kwangu apunguze miwili tu akuongezee wewe” alisema Mhe. Makoga.

Akieleza lengo la tathimini ya elimu ya mwaka 2018 hasa katika matokeo ya mitihani ya kitaifa Kaimu Mkurugenzi na Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Voster Mgina amesema tathimini hiyo itachangia kupanga mipango madhubuti ya mwaka 2019.

Matokeo ya mitihani ya Taifa kwa mwaka 2018 Halmashauri ya Mji Mafinga ilifanya vizuri sana katika mitihani yote.
Mtihani wa darasa la saba Halmashauri ya Mji Mafinga iliweza kufaulisha kwa kiwango cha asilimia 92.86%

Mtihani wa Kidato cha pili ufaulu ulikuwa wa kiwango cha asilimia 96% na kidato cha nne ufaulu ulikuwa wa kiwango cha asilimia 87 wakati huo mwaka jana ufaulu ulikuwa asilimia 73% lakini mwaka huu shule zote zimepandisha ufaulu  na zimeweza kupunguza daraja 0 kutoka 350 hadi 176.

Aidha kidato cha sita kwa matokeo ya mwaka 2018 Halmashauri ya Mji Mafinga iliweza kufaulisha kwa kiwango cha asilimia 100% na hakukua na mwanafunzi aliyepata daraja la 0 wala daraja la IV  kwa shule zote za serikali na binafsi.

 Kaimu Mkurugenzi bwana Mgina amemhakikishia Mhe. Mbunge Chumi kwamba baada ya kupata usafiri huo sasa unaenda kuongeza chachu ya ufuatiliaji wa elimu na kumuahidi kwamba Halmashauri inaenda kufanya vizuri zaidi katika matokeo yajayo ya mitihani ya Taifa.

 HABARI PICHA


Magari aliyoyatoa Mbunge wa Mafinga Mjini Mhe Cosato Chumi kwa Idara za Elimu Mafinga Mji


Mhe. Charles Makoga akitoa Shukrani

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe Charles Makoga akimkabidhi Fungua Kaimu Mkurugenzi na Afisa Elimu Sekondari Bwana Voster Mgina mara baada ya kukabidhiwa na Mbunge Cosato Chumi (Picha zote na Amani Mbwaga)


Thursday, February 14, 2019

Zaidi ya Bilioni 25 .2 za Bajeti ya 2019/2020 zapitishwa na Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Mafinga



Na Amani Mbwaga, Mafinga.
Mkutano maalumu wa baraza la madiwani  la Halmashauri ya Mji Mafinga leo limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya kipindi cha mwaka wa fedha 2019/2020 na kuidhinisha  kukusanya na kutumia zaidi ya   Bilioni 25.2 kwa ajili ya matumizi ya mishahara, mengineyo na miradi ya maendeleo.

Akisoma rasimu hiyo kwa niaba ya Mkurugenzi, Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Andambikye Kyomo amesema zaidi ya Bilioni 3.9 zinakadiriwa kukusanywa kutokana na vyanzo mbalimbali vya mapato ndani ya Halmashauri.

Makisio hayo ni zaidi ya milioni 648.8 ambayo ni asilimia 20% ukilinganisha na makisio ya mwaka 2018/2019 ya zaidi ya Tsh Bilioni 3.3, aidha katika mapato hayo kiasi cha zaidi ya Tsh milioni 602.8 ni mapato ya vyanzo fungiwa katika idara ya afya na elimu sekondari hivyo kufikia mapato halisi kuwa zaidi ya Bilioni 3.3.

Baraza hilo limeridhia pia matumizi ya kawaida kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo zaidi ya Bilioni 17.8 zimeidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mishahara , kati ya fedha hizo  kiasi cha zaidi ya  Tsh Bilioni 13.8 ni kwa ajili ya mishahara, na zaidi ya Bilioni 4 ni  kwa ajili ya matumizi mengineyo.

Aidha baraza hilo limeidhinisha pia kukusanya na kutumia zaidi ya Bilioni 7.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato kati ya fedha hizo zaidi ya bilioni 4.7 ni kutoka ruzuku ya serikali kuu, wahisani zaidi ya milioni 490, Halmashauri inatarajia kuchangia zaidi ya Bilioni 1.3 sawa na asilimia 40% ya mapato halisi ya ndani ya Halmashauro na nguvu ya wananchi wanatarajia kuchangia zaidi ya milioni 768.

Akieleza matarajio ya utekelezaji wa rasimu ya bajeti hiyo ya 2019/2020 Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Voster Mgina ametanabaisha kwamba bajeti hiyo italenga kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na kuongeza mapato ya ndani, kuongeza viwanda na fursa za uwekezaji, kuboresha huduma za usafi katika mji, kuboresha makazi na mipango miji sanjari na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na vitendea kazi na hatimae kukamilisha miradi viporo iliyoanzishwa siku nyingi katika sekta ya afya, elimu utawala na ujenzi.

Akiongoza baraza hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe. Charles Makoga amewahakikishia wananchi wa Mafinga kwamba bajeti hiyo iliyoidhinishwa leo hii itaenda kutekelezwa ipasavyo na imelenga kutatua kero za wananchi.

“Sisi kama watekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi wote kwa pamoja kwa kushirikiana na madiwani wa chadema kwa pamoja tunashirikiana kuhakikisha bajeti hii inaenda kutekelezwa katika kata zetu zote kama iliyopangwa bila kujali vyama vyetu kwani maendeleo hayana chama” Alisema

Aidha ameeleza kwamba katika kuendelea kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt John Magufuli za kuleta elimu bure na matokeo chanya yanayotokea ya ongezeko la wanafunzi, Halmashauri yake imejiandaa kuongeza kujenga shule mbili za Sekondari mpya ikiwemo ya vipaji maalumu na nyingine ya Wasichana itakayojulikana kwa jina la Mafinga Girls hii ni kutokana na ongezeko la ufaulu wa mtihani wa darasa la saba ambapo halmashauri hiyo imefikia asilimia 92.86% ya ufaulu kwa mwaka 2018 na kushika nafasi ya kwanza katika mkoa wa Iringa.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Mufindi Kaimu Katibu Tawala (DAS) Bwana Joseph Mchina ameipongeza Halmashauri ya mji wa Mafinga kwa kuwa na usimamizi mzuri wa utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Waheshimiwa Madiwani endeleeni kushirikiana na wataalamu hawa wa Halmashauri na wananchi kwa ujumla katika kufanikisha utekelezaji wa miradi yetu kwa viwango vyenye ubora unaotakiwa ambavyo thamani yake ya fedha inaonekana ili kuchochea maendeleo ya wananchi na kufikia kipato cha kati kwa manufaa ya sasa na ya kizazi kijacho” Alisema.

Mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2019/2020 yameandaliwa kwa kuzingatia mambo yafuatayo, Muongozo wa Bajeti wa 2019/2020, Ilani ya Uchaguzi ya chama Tawala –Ccm ya 2015/2016 -2019/2020, Malengo ya Maendeleo endelevu (SDGs), Dira ya Taifa ya maendeleo 2025, Maelekezo ya Ki- Sekta na Mpango wa maendeleo wa miaka mitano na mpango mkakati wa Halmashauri pamoja na vipaumbele vya Taifa kama vilivyofafanuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa kufunga bunge la 11 Mjini Dodoma.


Vilevile umezingatia mwongozo wa Serikali wa kuandaa mipango na Bajeti wa mwaka 2019/2020 uliotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango mwezi Disemba 2018 ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya Bajeti Namba 11 ya mwaka 2015 sehemu ya 21 na 22.


HABARI PICHA







Amanitz NEWS: ZAIDI YA BILIONI 25.2 ZA BAJETI ZAPITISHWA NA BARAZA LA MA...

Friday, February 1, 2019

Halmashauri ya Mji Mafinga Yazindua Kampeni ya Upandaji Miti Katika Vyanzo vya Maji.


Na Amani Mbwaga, Mafinga.
Halmshauri ya Mji Mafinga jana imezindua kampeni ya upandaji miti aina ya Mivengi katika chanzo cha maji eneo la Makamadolesi kata ya Changarawe Wilayani Mufindi Mkoani Iringa, uzinduzi huo umeoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Charles Makoga akimwakilisha Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William.

Kwa kuzingatia mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababaishwa na shughuli za kibinadamu za uvunnaji wa mazao ya misitu na kilimo kisichofuata hifadhi ya mazingira na vyanzo vya maji serikali iliamua kutenga tarehe mosi Aprili ya kila mwaka kuwa siku maalumu ya upandaji miti kitaifa.

Kampeni hiyo mwaka huu inaenda na kaulimbiu ya “Panda miti hifadhi Mazingira na Vyazo vya maji kwa vizazi vya sasa na vya baadae”

Hata hivyo kwa kuzingatia tofauti ya majira ya misimu ya mvua kuanza na kuisha katika maeneo haya, Mkoa wa Iringa ulipanga uzinduzi wa upandaji wa miti katika maeneo yote ya mkoa kufanyika mwezi Januari kila mwaka.

“Leo hii ni siku muhimu kwetu kwani inaelenga kukumbushana na kuelimishana juu ya umuhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo” alisema Mhe. Makoga.

Ameendelea kusisitiza kwamba uhaba wa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa mijini na vijijini aidha uharibifu wa vyanzo vya maji ni kero kubwa, na mfumo wa maji ni miongoni mwa  changamoto za mazingira zinazoendelea kulikumba taifa .

Pamoja na juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira ni muhimu ifahamike kwamba mazingira ni sehemu ya maisha ya binadamu na ndio uhai wa viumbe, Maisha ya binadamu yanategemea ardhi, maji, mimea na hewa.

“Takwimu za hivi karibuni za sensa ya miti zinaonesha wazi kwamba idadi inapungua sana takribani hekta zaidi ya 270,000 hadi 300,000 zinapungua kutokana na ukataji miti hovyo na uchomaji mkaa” alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi. Saada Mwaruka alisema Halmashauri yake imeandaa jumla ya miche 15,039 ambapo miche 5,000 ni pine na miche 5200 ni miti rafiki na maji (Mivengi), miche ya matunda parachichi 1,118, miche ya mapambo na vivuli 1400.

“Lengo la kupanda miche ya aina hii ni kwa ajili ya kuhifadhi mazingira kupendezesha maeneo ya wazi kuhifadhi vyanzo vya maji na kuimarisha mipaka ya maeneo mbalimbali” alisema.

Akisoma taarifa ya uzinduzi kwa mgeni rasmi Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Charles Tuyi alisema halmashauri hiyo imefanikiwa sana kwa upandaji wa miti kutokana na kuwa katika ukanda unaokubali mazao ya kilimo cha miti wananchi wake wanazidi kuhamasika kwani kila mwaka kwani  takwimu za upandaji  zimekuwa  zikizidi kuongezeka.

Licha ya mafanikio hayo Halmashauri hiyo bado inakumbwa na changamoto lukuki katika uhifadhi wa mazingira ikiwemo kuendelea kutokea kwa matukio ya moto kichaa unaoathiri misitu ya asili na ile ya kupandwa, uvamizi wa misitu na vyanzo vya maji kutokana na shughuli za kibinadamu, kukosekana takwimu halisi za miti iliyovunwa hasa miti michanga, uhaba wa wataalamu na vijiji vingi kutokuwa na mipango ya matumizi bora ya ardhi inayopelekea migogoro ya ardhi kutokea.

Bwana Tuyi ameeleza kwamba kutokana na changamoto hizo Halmashauri ya Mji Mafinga imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwa na kampeni ya utoaji elimu juu ya udhibiti mioto jamii kwa kushirikiana na wakala wa huduma za misitu Tanzania TFS-Shamba la Miti Sao Hill ambapo kila mwaka elimu hiyo hutolea na kuunda vikosi maalumu vya kudhibiti moto.

Mbali na hayo Halmashauri imeendelea kusimamia sheria ndogo za mazingira, kushawishi wizara ya maliasili na utalii kuimarisha na kusimamia matumizi ya mfumo wa viwango (Standards) sahihi katika biashara ya mazao ya misitu ili kudhibiti uvunaji holela wa miti michanga.

Kwa upande wake Afisa Misitu wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Peter Kibona amesema lengo kuu la halmashauri hiyo kwa mwaka 2019 ni kuotesha miche Milioni 1 na laki tano, hadi sasa zaidi  ya miche milioni 1 imepandwa katika maeneo mbalimbali na upandaji bado unaendeelea.

Kwa kipindi cha mwaka 2016 hadi sasa Halmashauri ya Mji Mafinga imepanda zaidi ya hekta 8,652.1 za miti.


Aidha Halmashauri hiyo imeanzisha vitalu vya miti ya aina mbalimbali ili kuweza kuhudumia wananchi kwa kuwagawia miti bure ili kuwapatia motisha katika upandaji  miti na uendelezaji wa miti hiyo kwa ajili ya  mazao ya misitu kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.