Na
Amani Mbwaga, Mafinga.
Halmshauri
ya Mji Mafinga jana imezindua kampeni ya upandaji miti aina ya Mivengi katika
chanzo cha maji eneo la Makamadolesi kata ya Changarawe Wilayani Mufindi Mkoani
Iringa, uzinduzi huo umeoongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Charles
Makoga akimwakilisha Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William.
Kwa kuzingatia
mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababaishwa na shughuli za kibinadamu za
uvunnaji wa mazao ya misitu na kilimo kisichofuata hifadhi ya mazingira na
vyanzo vya maji serikali iliamua kutenga tarehe mosi Aprili ya kila mwaka kuwa
siku maalumu ya upandaji miti kitaifa.
Kampeni hiyo mwaka
huu inaenda na kaulimbiu ya “Panda miti
hifadhi Mazingira na Vyazo vya maji kwa vizazi vya sasa na vya baadae”
Hata hivyo kwa
kuzingatia tofauti ya majira ya misimu ya mvua kuanza na kuisha katika maeneo
haya, Mkoa wa Iringa ulipanga uzinduzi wa upandaji wa miti katika maeneo yote ya
mkoa kufanyika mwezi Januari kila mwaka.
“Leo
hii ni siku muhimu kwetu kwani inaelenga kukumbushana na kuelimishana juu ya
umuhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo”
alisema
Mhe. Makoga.
Ameendelea
kusisitiza kwamba uhaba wa upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa
mijini na vijijini aidha uharibifu wa vyanzo vya maji ni kero kubwa, na mfumo
wa maji ni miongoni mwa changamoto za
mazingira zinazoendelea kulikumba taifa .
Pamoja na juhudi
zinazochukuliwa na serikali katika kukabiliana na uharibifu wa mazingira ni
muhimu ifahamike kwamba mazingira ni sehemu ya maisha ya binadamu na ndio uhai
wa viumbe, Maisha ya binadamu yanategemea ardhi, maji, mimea na hewa.
“Takwimu
za hivi karibuni za sensa ya miti zinaonesha wazi kwamba idadi inapungua sana
takribani hekta zaidi ya 270,000 hadi 300,000 zinapungua kutokana na ukataji miti
hovyo na uchomaji mkaa” alisema.
Kwa upande wake
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi. Saada Mwaruka alisema Halmashauri
yake imeandaa jumla ya miche 15,039 ambapo miche 5,000 ni pine na miche 5200 ni
miti rafiki na maji (Mivengi), miche ya matunda parachichi 1,118, miche ya
mapambo na vivuli 1400.
“Lengo
la kupanda miche ya aina hii ni kwa ajili ya kuhifadhi mazingira kupendezesha maeneo
ya wazi kuhifadhi vyanzo vya maji na kuimarisha mipaka ya maeneo mbalimbali”
alisema.
Akisoma taarifa ya
uzinduzi kwa mgeni rasmi Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana
Charles Tuyi alisema halmashauri hiyo imefanikiwa sana kwa upandaji wa miti
kutokana na kuwa katika ukanda unaokubali mazao ya kilimo cha miti wananchi
wake wanazidi kuhamasika kwani kila mwaka kwani takwimu za upandaji zimekuwa
zikizidi kuongezeka.
Licha ya mafanikio
hayo Halmashauri hiyo bado inakumbwa na changamoto lukuki katika uhifadhi wa
mazingira ikiwemo kuendelea kutokea kwa matukio ya moto kichaa unaoathiri
misitu ya asili na ile ya kupandwa, uvamizi wa misitu na vyanzo vya maji
kutokana na shughuli za kibinadamu, kukosekana takwimu halisi za miti
iliyovunwa hasa miti michanga, uhaba wa wataalamu na vijiji vingi kutokuwa na
mipango ya matumizi bora ya ardhi inayopelekea migogoro ya ardhi kutokea.
Bwana Tuyi ameeleza
kwamba kutokana na changamoto hizo Halmashauri ya Mji Mafinga imeendelea
kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwa na kampeni ya utoaji elimu juu ya
udhibiti mioto jamii kwa kushirikiana na wakala wa huduma za misitu Tanzania
TFS-Shamba la Miti Sao Hill ambapo kila mwaka elimu hiyo hutolea na kuunda
vikosi maalumu vya kudhibiti moto.
Mbali na hayo Halmashauri
imeendelea kusimamia sheria ndogo za mazingira, kushawishi wizara ya maliasili
na utalii kuimarisha na kusimamia matumizi ya mfumo wa viwango (Standards)
sahihi katika biashara ya mazao ya misitu ili kudhibiti uvunaji holela wa miti
michanga.
Kwa upande wake
Afisa Misitu wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Peter Kibona amesema lengo kuu
la halmashauri hiyo kwa mwaka 2019 ni kuotesha miche Milioni 1 na laki tano,
hadi sasa zaidi ya miche milioni 1
imepandwa katika maeneo mbalimbali na upandaji bado unaendeelea.
Kwa kipindi cha
mwaka 2016 hadi sasa Halmashauri ya Mji Mafinga imepanda zaidi ya hekta 8,652.1
za miti.
Aidha Halmashauri
hiyo imeanzisha vitalu vya miti ya aina mbalimbali ili kuweza kuhudumia
wananchi kwa kuwagawia miti bure ili kuwapatia motisha katika upandaji miti na uendelezaji wa miti hiyo kwa ajili ya
mazao ya misitu kwa faida ya vizazi vya
sasa na baadae.
No comments:
Post a Comment