Sunday, February 17, 2019

Mbunge Chumi Akabidhi Magari 02 Bure kwa Idara ya Elimu Mafinga



Na Amani Mbwaga, Mafinga.
Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Mhe. Cosato Chumi Mapema wiki hii amekabidhi Magari idadi mawili kwa Idara ya elimu katika Halmashauri ya Mji Mafinga kwa lengo la kuongeza nguvu ya ufuatiliaji wa masuala ya elimu ili kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na kuongeza ufaulu kwa wanafunzi wa Jimbo la Mafinga Mjini na Taifa kwa ujumla.

Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika viwanja vya Teachers Resource Centre (TRC Mafinga) wakati wa mkutano wa tathimini ya Elimu kwa Halmashauri ya Mji Mafinga ambapo umewakutanisha takribani waalimu wakuu wa shule zote za Sekondari na Msingi, Maafisa Elmu kata, Wilaya na Wataalamu wengine wote wa Sekta ya Elimu Mjini Mafinga.

Akiongea na Wataalamu hao wa elimu Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini Mhe. Cosato Chumi ameelezea hisia zake juu ya umuhimu wa elimu kwa wananchi wa Jimbo lake na taifa kwa ujumla.
“Mimi naamini kwamba elimu ndio kila kitu bila elimu tusingekuwa hapa kwa hiyo tunapokaa kufanya tathimini ya elimu tunapanga ili kuboresha elimu ya watoto wetu” alisema

Aidha ameeleza kuwa Halmashauri ya mji mafinga bado ni changa na ilianzishwa hivi karibuni kwa hiyo idara nyingi zina uhaba wa magari kwa hiyo yeye kama mbunge ameamua kujiongeza kutafuta wadau wakamsaidia magari hayo mawili ambayo ameyakabidhi kwa idara ya elimu Msingi na Sekondari.

Kwa Mujibu wa Mhe. Chumi amesema kwamba magari hayo amepewa na Kamishina wa Ushuru na Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) baada ya kumsumbua sana ili amsaidie magari kwa ajili ya idara za halmashauri yake na ndipo kamishina huyo akampatia magari hayo na leo ameikabidhi Halmshauri Kupitia Mkuu wa Wilaya Mufindi na baade kumkabidhi Mwenyekiti wa Halmashari ya Mji Mafinga tayari kwa matumizi ya kiserikali hususani idara ya elimu.

Akitoa shukrani kwa Mbunge huyo Mgeni wa rasmi wa hafla hiyo, Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William amempongeza Mhe. Chumi kwa kulipigania jimbo la Mafinga mjini katika kuhakikisha maendleo yanapatikana kwani amekuwa msaada mkubwa sana.

“Leo hii tumepokea magari mazuri halafu mapya kabisa yaliyotokana na jitihada za mbunge wetu Chumi, mimi kipekee nakushukuru sana naomba upeleke shukrani na salamu zetu kama Wilaya kwa wadau wote waliojitolea upatikanaji wa magari haya” alisema

Mhe. William amemhakikishia Mhe. Mbunge Chumi kuwa magari hayo yatatunzwa kwa kuzingatia kanuni na taratibu zote za utunzaji wa magari ya serikali na kutumika kwa shughuli za serikali hususani shughuli za elimu tu.

Hapo awali kulikuwa kunachangamoto ya shule nyingi kutofanyiwa ukaguzi na idara ya udhibiti ubora  elimu kutokana na ukosefu na uhaba wa usafiri sasa kupatikana kwa magari haya ni wakati muafaka wa kuhakikisha hakuna tena tatizo la ufuatiliaji wa elimu Mafinga Mjini.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe. Charles Makoga amesema Mhe. Mbunge Chumi amekuwa akisaidia sana katika upatikanaji wa vifaa mbalimbali toka ameingia ubunge kwa muda mfupi amechangia upatikanaji wa magari ya kubebea Wagonjwa (Ambulance) takribani manne sasa katika Halmshauri hiyo lakini pia alipigani pia kupatikana kwa gari la TASAF na la udhibiti ubora yote mapya ambayo yamepatikana pia hivi karibuni.

“Mhe Mbunge mimi nikushukuru sana na mungu akubariki sana kwa upendo wako mkubwa kwa wananchi wa Mafinga kama Mungu hua anapunguza miaka basi kwangu apunguze miwili tu akuongezee wewe” alisema Mhe. Makoga.

Akieleza lengo la tathimini ya elimu ya mwaka 2018 hasa katika matokeo ya mitihani ya kitaifa Kaimu Mkurugenzi na Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Voster Mgina amesema tathimini hiyo itachangia kupanga mipango madhubuti ya mwaka 2019.

Matokeo ya mitihani ya Taifa kwa mwaka 2018 Halmashauri ya Mji Mafinga ilifanya vizuri sana katika mitihani yote.
Mtihani wa darasa la saba Halmashauri ya Mji Mafinga iliweza kufaulisha kwa kiwango cha asilimia 92.86%

Mtihani wa Kidato cha pili ufaulu ulikuwa wa kiwango cha asilimia 96% na kidato cha nne ufaulu ulikuwa wa kiwango cha asilimia 87 wakati huo mwaka jana ufaulu ulikuwa asilimia 73% lakini mwaka huu shule zote zimepandisha ufaulu  na zimeweza kupunguza daraja 0 kutoka 350 hadi 176.

Aidha kidato cha sita kwa matokeo ya mwaka 2018 Halmashauri ya Mji Mafinga iliweza kufaulisha kwa kiwango cha asilimia 100% na hakukua na mwanafunzi aliyepata daraja la 0 wala daraja la IV  kwa shule zote za serikali na binafsi.

 Kaimu Mkurugenzi bwana Mgina amemhakikishia Mhe. Mbunge Chumi kwamba baada ya kupata usafiri huo sasa unaenda kuongeza chachu ya ufuatiliaji wa elimu na kumuahidi kwamba Halmashauri inaenda kufanya vizuri zaidi katika matokeo yajayo ya mitihani ya Taifa.

 HABARI PICHA


Magari aliyoyatoa Mbunge wa Mafinga Mjini Mhe Cosato Chumi kwa Idara za Elimu Mafinga Mji


Mhe. Charles Makoga akitoa Shukrani

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe Charles Makoga akimkabidhi Fungua Kaimu Mkurugenzi na Afisa Elimu Sekondari Bwana Voster Mgina mara baada ya kukabidhiwa na Mbunge Cosato Chumi (Picha zote na Amani Mbwaga)


No comments:

Post a Comment