Taasisi ya Kuzuia na
Kupamabana na Rushwa (TAKUKURU) ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa chini ya
Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007. Sheria hii
ilitungwa baada ya kufutwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) Sura ya 329
iliyofanyiwa marrejeo mwaka 2002.
Kuanzishwa kwa chombo hiki kulikuja baada ya
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Mswaada wa Sheria ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2007 mnamo tarehe 16 Aprili, 2007.
Mswaada huu
ulisainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Kikwete
kuwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mnamo tarehe 11Juni, 2007 na
ilianza kufanya kazi tarehe 1Julai, 2007.
Mapambano dhidi ya
rushwa nchini yalianza hata kabla ya Uhuru. Baada ya uhuru Tanzania ilirithi
sheria ya kikoloni ya Kuzuia Rushwa ya mwaka 1958 iliyokuwa na chimbuko lake
tangu mwaka 1930. Mwaka 1930 utawala wa Kiingereza ulitumia Kanuni ya Adhabu ya
India (The Indian Penal Code) kuwaadhibu watumishi wa Serikali ya kikoloni
waliopatikana na hatia ya kuomba na kupokea hongo.
Sheria hii ilikuwa na
vipengele vichache sana dhidi ya rushwa kama vile kuomba na kupokea hongo.
Vipengele vya sheria hii juu ya rushwa viliingizwa kwenye sheria ya makosa ya
Jinai, Sura ya 16 iliyotungwa na Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika
lililojulikana kama LEGICO (Legislative Council) mnamo mwaka 1945.
Hii ilikuwa
Sheria ya kwanza ya Kanuni za Adhabu Tanganyika iliyoanza kutumika kudhibiti
vitendo vya hongo na matumizi ya nyaraka zenye taarifa za uongo kwa lengo la
kumdanganya mwajiri. Mwaka 1958 LEGICO ilitunga Sheria ya Kuzuia Rushwa (Sura
ya 400) ambayo pia ilirejea vipengele vilivyokuwa katika Sheria ya Makosa ya
Jinai na ililenga kudhibiti vitendo vya rushwa kwa watumishi wa umma.
Kimsingi
kutungwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa, Sura ya 400, kulitokana na ukweli kwamba
Sheria ya Makosa ya Jinai , Sura ya 16, ilikuwa imeshindwa kuzuia au kupambana
na rushwa ipasavyo.
Baada ya uhuru
utumishi wa umma ulipanuka kwa kasi.Watumishi walianza kwenda kinyume na
maadili ya kazi na walianza kutumia nafasi zao kama vitega uchumi.
Mnamo mwaka
1970 Sheria ya Kuzuia Rushwa (Sura ya 400) ilifanyiwa marekebisho na kuongeza
kosa la mtumishi wa umma kupatikana na mali zilizopatikana kwa njia za rushwa.
Hata hivyo mnamo mwaka 1971 sheria hii ilifutwa na kutungwa Sheria ya Kuzuia
Rushwa, Sheria namba 16 ya mwaka 1971 (Sura ya 329) baada ya kuonekana
kushindwa kupambana na rushwa katika mazingira ya wakati huo. Sheria ya Kuzuia
Rushwa Namba 16 ya mwaka 1971 ilinakili vipengele vyote vya Sheria ya Kuzuia
Rushwa, Sura ya 400 na kuongeza makosa mengine kadhaa.
Kutokana na hali
ngumu ya kiuchumi iliyolikabili Taifa Sheria ya Kuzuia Rushwa ya mwaka 1971
haikuweza kupunguza kasi ya rushwa nchini. Kuadimika kwa bidhaa muhimu,
magendo, na ulanguzi vilichochea kasi ya ueneaji wa rushwa nchini. Rushwa
ilianza kuingia katika vyombo vya dola jambo ambalo lililazimu serikali Mnamo
mwaka 1974 kuifanyia marekebisho sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16 ya mwaka 1971
kupitia Sheria Namba 2 ya mwaka huo, kwa lengo la kuanzishwa kwa Kikosi cha
Kuzuia Rushwa (The Anti – Corruption Squad – ACS) ambacho kilianza
kufanya kazi mnamo tarehe 15Januari, 1975 kwa tamko la serikali Namba 17 la
mwaka 1975.
Kabla ya kikosi hiki kuanzishwa shughuli za kuzuia rushwa
zilifanywa na Jeshi la Polisi. Kikosi cha Kuzuia Rushwa kilikuwa na kazi kuu
tatu, yaani kuzuia rushwa, kupeleleza na kuendesha mashtaka dhidi ya watuhumiwa
wa makosa ya rushwa nchini.
Kikosi hiki kilikuwa chini ya Wizara ya Mambo ya
Ndani na kilikuwa na mamlaka ya kupambana na wala rushwa katika utumishi wa
Umma au mashirika yake na viongozi wa serikali. Hivyo kikosi hakikujihusisha na
rushwa katika sekta binafsi nchini.
Wakati wa Serikali
ya Awamu ya Pili hususani miaka ya 1980 mwishoni Serikali iliboresha masharti
ya biashara kwa kuruhusu uchumi wa soko huria na kufanya sekta binafsi kukua
kwa kasi.Vilevile katika kipindi cha awamu ya pili ya uongozi wa nchi serikali
iliruhusu mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mwanzonini mwa mwaka 1990.
Ili
kukidhi mabadiliko hayo ya kiuchumi na kisiasa Sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16
ya Mwaka 1971 (Sura ya 329) ilifanyiwa marekebisho mengine mwaka 1991.
Katika
marekebisho hayo ya kisheria Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) ilianzishwa
rasmi kuchukua nafasi ya Kikosi cha Kupambana na Rushwa kwa tamko la Serikali
Na.27 la mwaka 1991.
Mabadiliko yalilenga kukifanya chombo hicho kifanye kazi
zake kwa mbinu za kisayansi na uhuru zaidi. Wakati huo Taasisi ilikuwa na Idara
tatu ambazo ni Idara ya Utawala na Utumishi, Idara ya Sheria na Mashtaka na
Idara ya Mafunzo, Utafiti na Elimu kwa Umma.
Kutungwa kwa Sheria
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya
2007
Kutokana na maendeleo
ya sayansi, teknolojia, utandawazi, mabadiliko ya uchumi na kisiasa katika
miaka ya 1980 na mwanzoni mwa mwaka 1990 , yaliyotokea nchini na duniani kote
pamoja na kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya rushwa.
Sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16 ya mwaka 1971 ilianza kuonekana kushindwa
kuzuia na kupambana na rushwa. Baada ya kung’amua hilo, serikali iliamua
kuanzisha jitihada za kuangalia namna ya kuiboresha sheria hii ikiwa ni pamoja
na:
- Tume ya Rais ya kuchunguza kero
za rushwa nchini maarufu kama tume ya Warioba iliyoteuliwa na Rais mstaafu
wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa, tarehe 17 Januari, 1996.
- Kamati ya wataalamu kutoka ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Taasissi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) kwa
ajili ya kuangalia namna ya kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Warioba
mwaka 2000.
- Kamati ya wataalamu kutoka ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jeshi la Polisi, Kitivo cha Sheria ( Chuo
Kikuu cha Dar es salaam ) na TAKURU mnamo mwaka 2003.
- Ripoti ya Tume ya Kurekebisha
Sheria Tanzania ya mwaka 2004; na
- Kamati maalumu ya wataalamu
kutoka TAKURU, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Idara ya Mahakama, Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu, Ikulu na
Benki Kuu ya Tanzania mnamo mwaka 2005.
Kimsingi, makundi
yote haya ya watalaam yaligundua kuwa kulikuwa na mapungufu makubwa kwa upande
wa TAKURU katika vita dhidi ya rushwa nchini ikiwa ni pamoja na :
- Kutokuwepo uhakika wa ajira ya
Mkurugenzi Mkuu wa TAKURU;
- Kazi za TAKURU kutoainishwa
vizuri;
- Baadhi ya makosa ya rushwa
kutofanywa ya jinai;
- TAKURU kutowasilisha taarifa
zake Bungeni;
- Kutokuwepo vipengele katika
Sheria ya Kuzuia Rushwa ya Mwaka 1971 vinavyowalinda maofisa wa TAKURU
dhidi la tishio la kushtakiwa kutokana na shughuli zao;
- Kutokuwepo vipengele vinavyozuia
rushwa katika manunuzi na mikataba ya Serikali na kandarasi za Serikali;
na
- Kutokuwepo vipengele vya
kisheria vinavyozuia rushwa katika sekta binafsi.
Hivyo, ili kuifanya
vita dhidi ya rushwa iwe na mafanikio, ilipendekezwa kwamba wakati ulikuwa
umefika wa kuifuta Sheria ya Kuzuia Rushwa ya Mwaka 1971 na kutunga nyingine
yenye meno madubuti ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Kwa sababu hizi serikali
ilipeleka muswaada wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika kikao cha
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwezi Februari, 2007.
Kupitia
mswaada huu Sheria ya Kuzuia Rushwa Na.16/1971 ilifutwa na Sheria ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa Na.11/2007 ilipitishwa na Bunge mwezi Februali 2007 na
ilianza kutumika rasmi tarehe 01 Julai 2007.
Kufuatia kutungwa kwa Sheria hii,
jina la Taasisi ya Kuzuia Rushwa lilibadilishwa na kuwa Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Shabaha ya Sheria
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007
Kwa mujibu wa
Utangulizi wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007, Sheria
hii imetungwa kwa shabaha ya kuanzisha na kuipa nguvu Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili iweze kushughulikia kikamilifu makosa ya
rushwa na yale yanayofanana nayo hapa nchini. Sheria hii inatumika Tanzania
Bara peke yake na inahusu kila mtu atakaye jihusisha na vitendo vya rushwa
awapo nchini Tanzania au anapokuwa nje ya Tanzania au alikuwa nje ya Tanzania
na kwa wakati huo anaishi Tanzania .
Madhumuni ya Sheria
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007
Lengo kuu la Sheria
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007 limeainishwa katika kifungu
cha 4 cha Sheria hii ikiwa ni kuhakikisha ustawi wa utawala bora na kuondoa
rushwa nchini. Ili kuhakikisha lengo hili linatimia, sheria hii inaweka
mazingira bora kisheria, kiutawala, na kiutekelezaji yenye mwelekeo wa Kuzuia
na Kupambana na Rushwa nchini. Hivyo, sheria hii itawezesha:
- Kuwepo ushauri juu ya mienendo
na taratibu mbalimbali katika utekelelezaji wa shughuli za umma, mashirika
ya umma, taasisi binafsi nchini kwa lengo la kuifanyia kazi ya kung’amua
na kuzuia rushwa kuwa ya ufanisi
- Upatikanaji wa habari au taarifa
mbalimbali kuhusu athari za rushwa na vitendo mbalimbali vya rushwa
nchini;
- Kuwezesha au kufanikisha
ushirikiano mzuri na wenye manufaa kati ya taasisi mbalimbali za ndani na
nje ya nchi, zinazojihusisha na mapambanodhidi ya rushwa ;
- Kuhimiza ustawi, na kuimarisha
ushiriki wa umma kwa ujumla katika kupambana na rushwa nchini ,na
- Kuwezesha kufanyika kwa
uchunguzi, upelelezi na uendeshaji wa mashtaka dhidi ya watu
wanaojihusisha na vitendo vya rushwa nchini.
UONGOZI WA TAKUKURU
Kati ya mwaka 1973 –
1990 Taasisi (TAKURU) iliongozwa na Mkurugenzi akisaidiwa na Wakurugenzi
Wasaidizi chini ya Idara zao. Kati ya mwaka 1991- 2007 Taasisi iliongozwa
na Mkurugenzi Mkuu akisaidiwa na Wakurugenzi wa Idara.
Kuanzia mwaka 2007 hadi
sasa TAKUKURU imekuiwa ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu
akisaidiwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu na Wakurugenzi wa Idara na huteuliwa na
Rais. Toka mwaka 1973 hadi sasa TAKUKURU imeongozwa na Wakurugenzi wafuatao :
- 1973 – 1974: Ndugu Geofrey
Sawaya
- Machi,1974 – Juni,1975: Ndugu
S. Rutayangirwa
- Juni,1975-1990: Ndugu Zakaria
Maftah
- April,1990 – Novemba,
2006: Major General (Rtd), Anatory Ruta Kamazima
- Novemba, 2006 – Disemba,
2015: Edward Gamaya Hoseah
- Machi, 2015-Sasa: Ndugu
Valentino Longino Mlowola
No comments:
Post a Comment