Monday, June 4, 2018

MKUU WA WILAYA MUFINDI AWATAKA WAZAZI KUCHANGIA CHAKULA SHULENI.





 Mkuu wa Wilaya ya Mufindi amewataka wazazi na walezi waendelee kuchangia chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa kwa shabaha ya kuinua kiwango cha ufaulu, kupunguza utoro pamoja na kuleta usawa miongini mwao.

Akiongea na wananchi wa Igowole katika kilele cha wiki la kusoma  lililofanyika katika Viwanja vya shule ya Msingi Igowole iliyopo Halmashauri ya Wilaya Mufindi, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Bwana Joseph Mchina, amewataka vingozi wa serikali za vijiji kuendelea kutekeleza mkakati wa utoaji wa chakula cha Mchana shuleni kwa kuwamasisha wazazi kuchangia kwa mujibu wa sera ya Elimu bila malipo.

Aidha, amewapongeza viongozi wa siasa ambao wamekuwa bega kwa bega katika kuelimisha jamii na wazazi kuhusu umuhimu wa utoaji wa chakula cha mchana shuleni.

 “Napenda kupongeza kata zote ambazo zinazotoa chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni, utoaji wa chakula cha mchana shuleni huleta usawa kati ya walionacho na wasionacho, huimarisha mahudhurio ya wanafunzi shuleni huongeza usikivu wa wanafunzi darasani na hutunza muda wa ratiba nzima ya shule” alisema Mchina

Akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bwana Kennedy Bukagile, alisema Halmashauri ya Wilaya Mufindi imejiwekea mkakati mzuri wa kuwapatia wanafunzi chakula cha mchana ili kuimarisha usikivu  na mahudhurio shuleni,

 “wazazi wamejitoa kulima shamba la maharage na Mahindi lenye jumla ya hekari 294 kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni”        
            
Afisa huyo mwenye dhamana ya Elimu, ameongeza kuwa, Idara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamewezesha kamati za shule kujengewa uwezo wa uhamasishaji na pia kuwa na wahamasishaji jamii  wa masuala ya  elimu kwa kila shule, wakishirikiana na kamati za shule kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata chakula cha mchana jambo ambalo limesabisha kuongezeka kwa ufaulu sanjari na kushuka kwa takwimu za utoro.

Kwa upande mwingine Maadhimisho hayo yalienda sambamba na maonesho ya mabanda ya elimu na mashindano ya wanafunzi katika stadi za KKK, ambapo washindi wa shindano hilo walitangazwa na kupewa zawadi na Mgeni rasmi ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Mwanafunzi Anania Ng’umbi, darasa la pili wa Shule ya Msingi Igowole.

Aidha “kujua kusoma na kuandika ni haki ya kila mtu jambo hilo linamsaidia mtu kuwa na uwezo na njia yenye kumuwezesha kufanya maendeleo katika maisha yake pamoja na watu wengine”, Tamko la Shirika la UNESCO

Maadhimisho ya Wiki la Kusoma yanalenga kukuza na koungeza ari ya ushindani katika kujifunza stadi za msingi za kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) Ujumbe wa wiki la elimu mwaka huu ni Stadi za KKK ni Msingi wa Elimu, tuwekeze katika Elimu kuelekea Uchumi wa Viwanda  















No comments:

Post a Comment