Thursday, June 21, 2018

RC-Iringa Aipongeza Halmashauri ya Mji Mafinga Kwa Kupata Hati Safi


Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Amina Juma  Masenza akitoa Maelekezo kwa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Katika Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani lililokuwa likijadili Hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2016/2017 (Picha na Amani Mbwaga).

Na Amani Mbwaga Mafinga- Iringa
Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Amina Juma Masenza ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kupata hati safi katika mkutano maalumu wa baraza la Madiwani lililojadili majibu ya hoja za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia tarehe 30 Juni 2017, mkutano huo umefanyika leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya mji Mafinga Mkoani Iringa.

“Kwa namna ya kipekee nachukua fursa hii kuipongeza Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kupata hati safi na pia nazipongeza Halmashauri zetu zote 05 za Mkoa wetu wa Iringa kwa kupata hati safi za ukaguzi zilizoishia Juni 2017, kwani kitendo hiki kimeupa heshima kubwa Mkoa wetu, nawashukuru sana na hongereni waheshimiwa madiwani na watendaji wa serikali kwa kazi nzuri” alisema Mhe Masenza.

Katika mwaka wa Fedha ulioishia Juni 2017 Halmashauri ya Mji wa Mafinga imepata hati ya kuridhisha kutokana na ukaguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali, mkaguzi alianisha mapendekezo mbalimbali na kushauri hatua zinazotakiwa kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kutaka majibu ya hoja alizotoa.

Aidha Mhe Masenza ameliambia baraza la Madiwani kwamba tayari serikali imeshatoa Fedha kwa ajili ujenzi wa Miundombinu ya shule mbalimbali katika mkoa wa Iringa na Halmashauri ya mji wa Mafinga ni moja kati ya halmashauri zilizonufaika na Fedha hizo kwa ajili ya kupokea kidato cha tano mwaka huu 2018.

“Miongoni mwa shule zilizokwisha pokea fedha hizo ni Shule ya Sekondari Changarawe Tshs 80,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 4 na Tshs 150,000,000/= kwa ajili ya Mabweni, vilevile Shule ya Sekondari JJ Mungai nayo imepokea Tshs 80,000,000/= kwa ajili ya Madarasa na Tshs 150,000,000/= kwa ajili ya mabweni, Ujenzi huu ni kutoka katika Force Account na Mwisho wa utekelezaji wa ujenzi huo ni tarehe 30 Agosti 2018” Alisema Mhe Masenza.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe Jamhuri William akitoa salamu za Wilaya kwa Mkuu wa Mkoa Iringa, alisema “Kwa Ujumla mkuu wa mkoa wewe mwenyewe ni lazima useme na utupe maelekezo ili baraza hili liweze kutekeleza na tupo tayari kupokea maelekezo yako na kuyafanyia kazi”

Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Mhe Charles Makoga amewataka watumishi wa serikali kuongeza umakini katika kazi na kutimiza wajibu wao ili hoja ndogondogo zilizojitokeza zisijirudie tena.

Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga  Bi. Saada Mwaruka aliliambia baraza kuwa katika mwaka wa Fedha 2016/2017 ofisi yake imeandaa majibu ya hoja na ushauri mbalimbali katika hoja zilizotolewa na Mkaguzi ambapo majibu yatahakikiwa na ofisi ya mkaguzi ili kuweza kumaliza na kuendelea kutekeleza ushauri uliotolewa.

“Majibu hayo yamewasilishwa leo hii katika mkutano wa baraza la madiwani ili kuweza kupata ushauri ambao utatumika katika kuboresha utendaji wa kazi na kupunguza au kumaliza kabisa hoja mbalimbali zilizotolewa na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali” alisema Mwaruka.

Mkutano huo maalumu wa baraza la madiwani kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka unaoishia 30 Juni 2017 ni utekelezaji wa agizo alilolitoa Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kasim Majaliwa kwenye kikao na Wakuu wa Mikoa kilichofanyika tarehe 29 April 2017, ambapo aliwataka wakuu wa Mikoa kote nchini  kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha Halmashauri zote zinafanyia kazi ipasavyo hoja zote zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2016/2017 na zile zilizotolewa miaka ya nyuma.

Aidha Mhe Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi kupitia barua yake ya tarehe 20 April 2018 alisisitiza kuwa wakuu wa mikoa kote nchini wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika vikao maalumu kwenye Halmashauri wanazosimamia kwa lengo la kujadili hoja na Mapendekezo yote yaliyotolewa na Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha 2016/2017. 


HABARI KATIKA PICHA

Mkuu wa Mkoa Iringa akisoma Hotuba wakati wa mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Mafinga.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Diwani Charles Makoga akiongoza  mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali (Picha na Amani Mbwaga).

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Akiteta jambo na Katibu Tawala (RAS) Wa Mkoa Wa Iringa Bi Wamoja Ayubu Dickolagwa Kulia Kwake ni Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jahuri William.

Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William akitoa salamu za wilaya ya Mufindi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati wa Mkutano maalumu wa Baraza la madiwani Halmashauri ya Mji wa Mafinga

Mkurugenzi wa Mji wa Mafinga  Bi Saada Mwaruka akijibu baadhi ya hoja zilizoulizwa na waheshimiwa Madiwani.

Baadhi ya Waheshimiwa madiwani  wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga wakifuatilia kwa makini Majibu ya Hoja za Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za wa seikali.



Baadhi ya Wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Wakifuatilia kwa makini Maelekezo ya Mkuu wa Mkoa Kuhusu hoja zilizotolewa na CIG tayari kwa kuzitekeleza ipasavyo na kwa wakati muafaka

 






Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Sao Hill Denis Kutimile   akichangia hoja katia mutano maalumu wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji wa Mafinga.


Afisa  Kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa anaesimamia serikali za mitaa nae akichangia hoja(Picha na Amani Mbwaga)


Mtunza Hazina wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Ramadhani Mbuguyu  akijibu baadi ya hoja za idara yake  wakati wa mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani
Mkaguzi wa ndani Halmashauri ya Mji wa Mafinga Erick Ntikahela akitolea ufafanuzi baadhi ya hoja.



Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Voster Mgina nae akijibu baadhi ya hoja zinazohusu elimu.




Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Mhe Diwani Charles Makoga  Wakipongezana na  Mkurugenzi wa Mji Mafinga Bi Saada Mwaruka mara baada ya kumaliza mkutano maalumu wa baraza la madiwani katika kujadili majibu ya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 (Picha zote na Amani Mbwaga)


No comments:

Post a Comment