Thursday, March 21, 2019

Shamba la Miti Sao Hill Laadhimisha Siku ya Kimataifa ya Misitu Duniani na Kugawa Miche ya Miti Takribani Milioni 1 Kwa Wananchi Buree.



Na Amani Mbwaga, Mafinga.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Shamba la miti Sao Hill limeungana na taasisi nyingine duniani katika kuadhimisha siku ya misitu duniani ambayo hufanyika Tarehe 21 Machi ya kila mwaka.

Katika madhimisho ya mwaka huu shamba la miti Sao Hill limewapatia wananchi na Taasisi mbalimbali za serikali na binafsi Miche takribani Milioni Moja ya miti aina ya Msindano (Pine) kwa lengo la kuongeza kasi ya upandaji wa miti kila mwaka ili kurahisisha upatikanaji wa malighafi ya mazao ya misitu viwandani kwa dhumuni la kuunga mkono serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Magufuli ya kuwa na Tanzania ya Viwanda na kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025.

Meneja Shamba la Miti Sao Hill Bwana Herberth Haulle akiongea na waandishi wa habari ofsini kwake ameeleza namna sekta ya misitu nchini inavyochangia katika kutoa malighafi ya viwanda vya Karatasi, Mbao, Nguzo, viberiti, chai (Kukaushia-chai) nk.

Viwanda vipatavyo elfu saba huwasilisha uhitaji wa malighafi katika mashamba ya miti yanayomilikiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania, 81.2% ya viwanda hivi vinaonesha uhitaji wa malighafi kutoka eneo tengefu la Saohill.

Saohill inahudumia 71% ya viwanda vinavyohudimiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupitia mashamba ya miti.

Viwanda hivi vilionesha kuhitaji jumla ya meta za ujazo milioni 22,439, 489 kwa Sao hill pekee viwanda vilionesha uhitaji wa meta za ujazo milioni 18 hii ni asilimia 84.3%,  Ambapo malighafi iliyotolewa (uwezo wa mashamba) ni asilimia 5 tu ya malighafi iliyohitajika kwa  viwanda.

Uwezo wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kutoa malighafi kwa viwanda ni mita za ujazo millioni moja kwa mwaka ambapo Saohill hutoa 83.8% ya malighafi husika.


Chanzo cha mapato ya serikali (TFS) kwa zaidi ya nusu ya makusanyo yanayo fanywa na TFS ni makusanyo kutoka Shamba la Miti Sao hill. 
Misitu huchangia pia katika upatikanaji wa hali nzuri ya hewa na utunzaji wa vyanzo vya maji ya kutumia binadamu na mengine kwa ajili ya kuzalisha nishati ya umeme, mfano bwawa la Kihansi na Mto Ruaha unaopeleka maji yake katika mradi mpya wa umeme Rufiji (Stigler’s Gorge).

Aidha bwana Haulle ameeleza pia namna sekta ya misitu kupitia shamba la miti Sao Hill linavyochangia katika uchumi wa wilaya ya Mufindi Mkoa wa Iringa, Taifa na dunia kwa ujumla.

“Shamba limekua likichangia asilimia tano 5% ya mrabaha wa mauzo ya miti  (CESS) kwa mujibu wa sheria kwa Halmashauri zinazozungukwa na Shamba la Miti Sao Hill ambazo ni  Mufindi, Kilombero na Halmashauri ya Mji Mafinga ambapo kwa kipindi cha mwaka 2010/2011 hadi disemba 2018 kiasi cha Zaidi ya Bilioni 6 kilikusanywa kama CESS na kukabidhiwa kwa halmashauri husikakwa ajili ya shughuli za maendeleo” alisema.

Aidha shamba la miti Sao Hill huajiri vibarua wa kutwa Zaidi ya Elfu tatu 3000 kwa mwaka katika kazi mbalimbali za shamba na wengi wao ni wakazi wanaozungukwa na shamba hilo.

Akiongea katika Kipindi maalumu cha utoaji elimu kwa umma leo hii kuhusu siku ya Kimataifa ya  Misitu duniani katika kituo cha redio Ebony fm MKoani Iringa Meneja Msaidizi Mipango na Matumizi wa Shamba la Miti Sao Hill  Bwana Ignas Lupala ameeleza chimbuko kubwa la misitu Tanzania na hatimae hadi kuanzishwa kwa shamba la miti Sao Hill.

Kwa kuzingatia taarifa ya tathimini ya rasilimali ya misitu iliyofanyika nchini kati mwaka 2010 – 2013, inaonesha kuwa misitu inakadiriwa kufikia eneo la hekta milioni 48.1, sawa na asilimia 55 ya eneo la ardhi la Tanzania Bara lenye hekta millioni 88 (TFS, 2015).

Kati ya eneo hilo, asilimia 93 ni misitu ya mataji wazi (woodlands), wakati sehemu inayobaki inajumuisha misitu   ya lindimaji, mikoko, misitu ya pwani (coastal forests), na mashamba ya miti.

Misitu ya kupandwa ni hekta 572,000 ambayo inajumuisha yale yanayomilikiwa na serikali, watu na makampuni binafsi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, mahitaji ya mazao ya misitu yalikadiriwa kuwa ni meta za ujazo milioni 62.3 kwa mwaka huku wakati uwezo wa misitu kutoa mahitahiji hayo kwa njia endelevu ukiwa meta za ujazo milioni 42.8.

Hivyo, kuwepo na upungufu wa meta za ujazo milioni 19.5 kwa ajili ya matumizi mbalimbali kama nishati (kuni na mkaa), nguzo za umeme pamoja na mbao kwa ajili ya ujenzi.

Upungufu huo umekuwa kichocheo cha uvunaji haramu katika misitu ya asili ambao husababisha uharibifu na upotevu wa misitu hiyo.
Katika jitihada za kuongeza upatikanaji wa Malighafi ya miti Ili kukabiliana na upungufu wa malighafi/ mazao ya misitu, serikali ilianzisha mashamba ya miti (forest plantations) katika maeneo mbalimbali.

Lengo ni kupunguza utegemezi wa mazao ya misitu kutoka katika misitu ya asili ili kuhifadhi mazingira na baionuai.
Kwa sasa serikali inamiliki mashamba 24 yanayopatikana maeneo mbalimbali nchini.

Mashamba hayo yana jumla hekta 306,980.20 na kusimamiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Kati ya hekta hizo, jumla ya hekta 105,583.56 sawa na asilimia 34 ya eneo la mashamba hayo zimepandwa miti.

Maeneo mengine yamehifadhiwa kwa ajili ya vyanzo vya maji na mengine yanaendelea kupandwa kulinganga na mipango ya usimamizi wa mashamba husika.

Shamba la Miti Sao Hill ni miongoni mwa mashamba 24 ya miti ya kupandwa ya serikali ambayo yanasimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii Kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS)

Shamba hili kwa sehemu kubwa lipo katika wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa na eneo dogo lipo katika Wilaya ya Kilombero Mkoani Morogoro
Shamba hili lilianzishwa kwa majaribio mnamo mwaka 1939 hadi 1951 na upandaji wa miti kwa kiwango kikubwa ulianza rasmi kuanzia miaka ya 1960 hadi 1980.

Aidha shamba hili ndilo shamba kubwa kuliko mashamba yote 24 ya serikali ambapo kwa sasa lina ukubwa wa hekta laki moja na thelathini na tano elfu mia tisa na tatu 135,903.

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya misitu duniani kila mwaka, nchi mbalimbali duniani zinahamasishwa kuendeleza juhudi za kitaifa na kimataifa ili kuandaa na kushiriki katika shughuli zinazohusika na misitu pamoja na miti, kama vile kampeni ya kupanda miti pamoja na midahalo kuhusu misitu.

Siku hii huadhimishwa kwa ajili ya kuwafanya watu waelewe umuhimu wa aina zote za misitu duniani, ikiwemo jukumu lake katika mabadiliko ya tabia nchi.

Siku hii ilianzishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka 2012 na siku hiyo ilisherehekewa kwa mara ya kwanza Machi 21, 2013.

Makala hii Maalumu Imeandaliwa na Amani Mbwaga kwa kushirikiana na Kitengo cha Uenezi na Ugani katika Ofisi ya Habari na Mawasiliano TFS- Shamba la Miti Sao Hill
Tarehe 21 Machi 2019.
Mob+255 656 632 566
E-mail:prof.mbwaga@gmail.com

HABARI PICHA


Meneja Shamba la Miti Sao Hill Bwana Heriberth Haulle


Baadhi ya Miche ya Miti ya Msindano (Pines) Iliyopandwa Msimu huu katika Shamba la Miti Sao Hill na Mingine Kugawiwa kwa Wananchi bure
Daniel Silima Meneja Msaidizi Rasilimali za Misitu Shamba la Miti Sao Hill


 


Ignas Lupala Meneja Msaidizi Mipango na Matumizi Shamba la Miti Sao Hill Mapema Leo hii akitoa Elimu kwa umma kwa njia ya Redio kuhusu chimbuko la Misitu Nchini na Faida za uwepo wa Shamba la Miti Sao Hill katika kituo cha EBONY FM RADIO Mapema leo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Misitu Duniani (Picha  na Amani Mbwaga)

(Picha zote na Amani Mbwaga)