Thursday, June 21, 2018

RC-Iringa Aipongeza Halmashauri ya Mji Mafinga Kwa Kupata Hati Safi


Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Amina Juma  Masenza akitoa Maelekezo kwa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Katika Mkutano Maalumu wa Baraza la Madiwani lililokuwa likijadili Hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2016/2017 (Picha na Amani Mbwaga).

Na Amani Mbwaga Mafinga- Iringa
Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Amina Juma Masenza ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kupata hati safi katika mkutano maalumu wa baraza la Madiwani lililojadili majibu ya hoja za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia tarehe 30 Juni 2017, mkutano huo umefanyika leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya mji Mafinga Mkoani Iringa.

“Kwa namna ya kipekee nachukua fursa hii kuipongeza Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kupata hati safi na pia nazipongeza Halmashauri zetu zote 05 za Mkoa wetu wa Iringa kwa kupata hati safi za ukaguzi zilizoishia Juni 2017, kwani kitendo hiki kimeupa heshima kubwa Mkoa wetu, nawashukuru sana na hongereni waheshimiwa madiwani na watendaji wa serikali kwa kazi nzuri” alisema Mhe Masenza.

Katika mwaka wa Fedha ulioishia Juni 2017 Halmashauri ya Mji wa Mafinga imepata hati ya kuridhisha kutokana na ukaguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali, mkaguzi alianisha mapendekezo mbalimbali na kushauri hatua zinazotakiwa kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kutaka majibu ya hoja alizotoa.

Aidha Mhe Masenza ameliambia baraza la Madiwani kwamba tayari serikali imeshatoa Fedha kwa ajili ujenzi wa Miundombinu ya shule mbalimbali katika mkoa wa Iringa na Halmashauri ya mji wa Mafinga ni moja kati ya halmashauri zilizonufaika na Fedha hizo kwa ajili ya kupokea kidato cha tano mwaka huu 2018.

“Miongoni mwa shule zilizokwisha pokea fedha hizo ni Shule ya Sekondari Changarawe Tshs 80,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 4 na Tshs 150,000,000/= kwa ajili ya Mabweni, vilevile Shule ya Sekondari JJ Mungai nayo imepokea Tshs 80,000,000/= kwa ajili ya Madarasa na Tshs 150,000,000/= kwa ajili ya mabweni, Ujenzi huu ni kutoka katika Force Account na Mwisho wa utekelezaji wa ujenzi huo ni tarehe 30 Agosti 2018” Alisema Mhe Masenza.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe Jamhuri William akitoa salamu za Wilaya kwa Mkuu wa Mkoa Iringa, alisema “Kwa Ujumla mkuu wa mkoa wewe mwenyewe ni lazima useme na utupe maelekezo ili baraza hili liweze kutekeleza na tupo tayari kupokea maelekezo yako na kuyafanyia kazi”

Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Mhe Charles Makoga amewataka watumishi wa serikali kuongeza umakini katika kazi na kutimiza wajibu wao ili hoja ndogondogo zilizojitokeza zisijirudie tena.

Kwa upande mwingine Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga  Bi. Saada Mwaruka aliliambia baraza kuwa katika mwaka wa Fedha 2016/2017 ofisi yake imeandaa majibu ya hoja na ushauri mbalimbali katika hoja zilizotolewa na Mkaguzi ambapo majibu yatahakikiwa na ofisi ya mkaguzi ili kuweza kumaliza na kuendelea kutekeleza ushauri uliotolewa.

“Majibu hayo yamewasilishwa leo hii katika mkutano wa baraza la madiwani ili kuweza kupata ushauri ambao utatumika katika kuboresha utendaji wa kazi na kupunguza au kumaliza kabisa hoja mbalimbali zilizotolewa na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali” alisema Mwaruka.

Mkutano huo maalumu wa baraza la madiwani kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka unaoishia 30 Juni 2017 ni utekelezaji wa agizo alilolitoa Waziri mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kasim Majaliwa kwenye kikao na Wakuu wa Mikoa kilichofanyika tarehe 29 April 2017, ambapo aliwataka wakuu wa Mikoa kote nchini  kufuatilia kwa karibu ili kuhakikisha Halmashauri zote zinafanyia kazi ipasavyo hoja zote zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2016/2017 na zile zilizotolewa miaka ya nyuma.

Aidha Mhe Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi kupitia barua yake ya tarehe 20 April 2018 alisisitiza kuwa wakuu wa mikoa kote nchini wanatakiwa kushiriki kikamilifu katika vikao maalumu kwenye Halmashauri wanazosimamia kwa lengo la kujadili hoja na Mapendekezo yote yaliyotolewa na Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka wa Fedha 2016/2017. 


HABARI KATIKA PICHA

Mkuu wa Mkoa Iringa akisoma Hotuba wakati wa mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Mafinga.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Diwani Charles Makoga akiongoza  mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za Serikali (Picha na Amani Mbwaga).

Mkuu wa Mkoa wa Iringa Akiteta jambo na Katibu Tawala (RAS) Wa Mkoa Wa Iringa Bi Wamoja Ayubu Dickolagwa Kulia Kwake ni Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jahuri William.

Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William akitoa salamu za wilaya ya Mufindi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati wa Mkutano maalumu wa Baraza la madiwani Halmashauri ya Mji wa Mafinga

Mkurugenzi wa Mji wa Mafinga  Bi Saada Mwaruka akijibu baadhi ya hoja zilizoulizwa na waheshimiwa Madiwani.

Baadhi ya Waheshimiwa madiwani  wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga wakifuatilia kwa makini Majibu ya Hoja za Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za wa seikali.



Baadhi ya Wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Wakifuatilia kwa makini Maelekezo ya Mkuu wa Mkoa Kuhusu hoja zilizotolewa na CIG tayari kwa kuzitekeleza ipasavyo na kwa wakati muafaka

 






Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Sao Hill Denis Kutimile   akichangia hoja katia mutano maalumu wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji wa Mafinga.


Afisa  Kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa anaesimamia serikali za mitaa nae akichangia hoja(Picha na Amani Mbwaga)


Mtunza Hazina wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Ramadhani Mbuguyu  akijibu baadi ya hoja za idara yake  wakati wa mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani
Mkaguzi wa ndani Halmashauri ya Mji wa Mafinga Erick Ntikahela akitolea ufafanuzi baadhi ya hoja.



Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Voster Mgina nae akijibu baadhi ya hoja zinazohusu elimu.




Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Mhe Diwani Charles Makoga  Wakipongezana na  Mkurugenzi wa Mji Mafinga Bi Saada Mwaruka mara baada ya kumaliza mkutano maalumu wa baraza la madiwani katika kujadili majibu ya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017 (Picha zote na Amani Mbwaga)


Friday, June 8, 2018

Ijue Historia ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini Tanzania (TAKUKURU)

Mwanafunzi wa Shule ya Sekondari JJ Mungai iliyoko Mafinga Mjini Mkoani Iringa, Wakati wa Uzinduzi wa Klabu ya Wapinga Rushwa Shuleni Hapo ilipozinduliwa Rasmi na Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa 2018 Ndugu Charles Francis Kabeho         (Picha na Amani Mbwaga)

Taasisi ya Kuzuia na Kupamabana na Rushwa (TAKUKURU) ni taasisi ya Umma iliyoanzishwa chini ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya Mwaka 2007. Sheria hii ilitungwa baada ya kufutwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) Sura ya 329 iliyofanyiwa marrejeo mwaka 2002.

Kuanzishwa kwa chombo hiki kulikuja baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitisha Mswaada wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa wa mwaka 2007 mnamo tarehe 16 Aprili, 2007.

Mswaada huu ulisainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Kikwete kuwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mnamo tarehe 11Juni, 2007 na ilianza kufanya kazi tarehe 1Julai, 2007.

Mapambano dhidi ya rushwa nchini yalianza hata kabla ya Uhuru. Baada ya uhuru Tanzania ilirithi sheria ya kikoloni ya Kuzuia Rushwa ya mwaka 1958 iliyokuwa na chimbuko lake tangu mwaka 1930. Mwaka 1930 utawala wa Kiingereza ulitumia Kanuni ya Adhabu ya India (The Indian Penal Code) kuwaadhibu watumishi wa Serikali ya kikoloni waliopatikana na hatia ya kuomba na kupokea hongo. 

Sheria hii ilikuwa na vipengele vichache sana dhidi ya rushwa kama vile kuomba na kupokea hongo. Vipengele vya sheria hii juu ya rushwa viliingizwa kwenye sheria ya makosa ya Jinai, Sura ya 16 iliyotungwa na Baraza la Kutunga Sheria la Tanganyika lililojulikana kama LEGICO (Legislative Council) mnamo mwaka 1945.

 Hii ilikuwa Sheria ya kwanza ya Kanuni za Adhabu Tanganyika iliyoanza kutumika kudhibiti vitendo vya hongo na matumizi ya nyaraka zenye taarifa za uongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri. Mwaka 1958 LEGICO ilitunga Sheria ya Kuzuia Rushwa (Sura ya 400) ambayo pia ilirejea vipengele vilivyokuwa katika Sheria ya Makosa ya Jinai na ililenga kudhibiti vitendo vya rushwa kwa watumishi wa umma.

Kimsingi kutungwa kwa Sheria ya Kuzuia Rushwa, Sura ya 400, kulitokana na ukweli kwamba Sheria ya Makosa ya Jinai , Sura ya 16, ilikuwa imeshindwa kuzuia au kupambana na rushwa ipasavyo.

Baada ya uhuru utumishi wa umma ulipanuka kwa kasi.Watumishi walianza kwenda kinyume na maadili ya kazi na walianza kutumia nafasi zao kama vitega uchumi. 

Mnamo mwaka 1970 Sheria ya Kuzuia Rushwa (Sura ya 400) ilifanyiwa marekebisho na kuongeza kosa la mtumishi wa umma kupatikana na mali zilizopatikana kwa njia za rushwa.

Hata hivyo mnamo mwaka 1971 sheria hii ilifutwa na kutungwa Sheria ya Kuzuia Rushwa, Sheria namba 16 ya mwaka 1971 (Sura ya 329) baada ya kuonekana kushindwa kupambana na rushwa katika mazingira ya wakati huo. Sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16 ya mwaka 1971 ilinakili vipengele vyote vya Sheria ya Kuzuia Rushwa, Sura ya 400 na kuongeza makosa mengine kadhaa.

Kutokana na hali ngumu ya kiuchumi iliyolikabili Taifa Sheria ya Kuzuia Rushwa ya mwaka 1971 haikuweza kupunguza kasi ya rushwa nchini. Kuadimika kwa bidhaa muhimu, magendo, na ulanguzi vilichochea kasi ya ueneaji wa rushwa nchini. Rushwa ilianza kuingia katika vyombo vya dola jambo ambalo lililazimu serikali Mnamo mwaka 1974 kuifanyia marekebisho sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16 ya mwaka 1971 kupitia Sheria Namba 2 ya mwaka huo, kwa lengo la kuanzishwa kwa Kikosi cha Kuzuia Rushwa (The Anti – Corruption Squad – ACS) ambacho kilianza kufanya kazi mnamo tarehe 15Januari, 1975 kwa tamko la serikali Namba 17 la mwaka 1975.

 Kabla ya kikosi hiki kuanzishwa shughuli za kuzuia rushwa zilifanywa na Jeshi la Polisi. Kikosi cha Kuzuia Rushwa kilikuwa na kazi kuu tatu, yaani kuzuia rushwa, kupeleleza na kuendesha mashtaka dhidi ya watuhumiwa wa makosa ya rushwa nchini. 

Kikosi hiki kilikuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na kilikuwa na mamlaka ya kupambana na wala rushwa katika utumishi wa Umma au mashirika yake na viongozi wa serikali. Hivyo kikosi hakikujihusisha na rushwa katika sekta binafsi nchini.

Wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili hususani miaka ya 1980 mwishoni Serikali iliboresha masharti ya biashara kwa kuruhusu uchumi wa soko huria na kufanya sekta binafsi kukua kwa kasi.Vilevile katika kipindi cha awamu ya pili ya uongozi wa nchi serikali iliruhusu mfumo wa vyama vingi vya kisiasa mwanzonini mwa mwaka 1990.

Ili kukidhi mabadiliko hayo ya kiuchumi na kisiasa Sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16 ya Mwaka 1971 (Sura ya 329) ilifanyiwa marekebisho mengine mwaka 1991. 

Katika marekebisho hayo ya kisheria Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) ilianzishwa rasmi kuchukua nafasi ya Kikosi cha Kupambana na Rushwa kwa tamko la Serikali Na.27 la mwaka 1991.

Mabadiliko yalilenga kukifanya chombo hicho kifanye kazi zake kwa mbinu za kisayansi na uhuru zaidi. Wakati huo Taasisi ilikuwa na Idara tatu ambazo ni Idara ya Utawala na Utumishi, Idara ya Sheria na Mashtaka na Idara ya Mafunzo, Utafiti na Elimu kwa Umma.

Kutungwa kwa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya 2007
Kutokana na maendeleo ya sayansi, teknolojia, utandawazi, mabadiliko ya uchumi na kisiasa katika miaka ya 1980 na mwanzoni mwa mwaka 1990 , yaliyotokea nchini na duniani kote pamoja na kuzingatia matakwa ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa dhidi ya rushwa.

Sheria ya Kuzuia Rushwa Namba 16 ya mwaka 1971 ilianza kuonekana kushindwa kuzuia na kupambana na rushwa. Baada ya kung’amua hilo, serikali iliamua kuanzisha jitihada za kuangalia namna ya kuiboresha sheria hii ikiwa ni pamoja na:
  • Tume ya Rais ya kuchunguza kero za rushwa nchini maarufu kama tume ya Warioba iliyoteuliwa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin William Mkapa, tarehe 17 Januari, 1996.
  • Kamati ya wataalamu kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Taasissi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) kwa ajili ya kuangalia namna ya kutekeleza mapendekezo ya Tume ya Warioba mwaka 2000.
  • Kamati ya wataalamu kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jeshi la Polisi, Kitivo cha Sheria ( Chuo Kikuu cha Dar es salaam ) na TAKURU mnamo mwaka 2003.
  • Ripoti ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ya mwaka 2004; na
  • Kamati maalumu ya wataalamu kutoka TAKURU, Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Idara ya Mahakama, Ofisi ya Kabidhi Wasii Mkuu, Ikulu na Benki Kuu ya Tanzania mnamo mwaka 2005.
Kimsingi, makundi yote haya ya watalaam yaligundua kuwa kulikuwa na mapungufu makubwa kwa upande wa TAKURU katika vita dhidi ya rushwa nchini ikiwa ni pamoja na :
  • Kutokuwepo uhakika wa ajira ya Mkurugenzi Mkuu wa TAKURU;
  • Kazi za TAKURU kutoainishwa vizuri;
  • Baadhi ya makosa ya rushwa kutofanywa ya jinai;
  • TAKURU kutowasilisha taarifa zake Bungeni;
  • Kutokuwepo vipengele katika Sheria ya Kuzuia Rushwa ya Mwaka 1971 vinavyowalinda maofisa wa TAKURU dhidi la tishio la kushtakiwa kutokana na shughuli zao;
  • Kutokuwepo vipengele vinavyozuia rushwa katika manunuzi na mikataba ya Serikali na kandarasi za Serikali; na
  • Kutokuwepo vipengele vya kisheria vinavyozuia rushwa katika sekta binafsi.
Hivyo, ili kuifanya vita dhidi ya rushwa iwe na mafanikio, ilipendekezwa kwamba wakati ulikuwa umefika wa kuifuta Sheria ya Kuzuia Rushwa ya Mwaka 1971 na kutunga nyingine yenye meno madubuti ya kuzuia na kupambana na rushwa. 

Kwa sababu hizi serikali ilipeleka muswaada wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa katika kikao cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo mwezi Februari, 2007. 

Kupitia mswaada huu Sheria ya Kuzuia Rushwa Na.16/1971 ilifutwa na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/2007 ilipitishwa na Bunge mwezi Februali 2007 na ilianza kutumika rasmi tarehe 01 Julai 2007.

Kufuatia kutungwa kwa Sheria hii, jina la Taasisi ya Kuzuia Rushwa lilibadilishwa na kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Shabaha ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007
Kwa mujibu wa Utangulizi wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007, Sheria hii imetungwa kwa shabaha ya kuanzisha na kuipa nguvu Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili iweze kushughulikia kikamilifu makosa ya rushwa na yale yanayofanana nayo hapa nchini. Sheria hii inatumika Tanzania Bara peke yake na inahusu kila mtu atakaye jihusisha na vitendo vya rushwa awapo nchini Tanzania au anapokuwa nje ya Tanzania au alikuwa nje ya Tanzania na kwa wakati huo anaishi Tanzania .

Madhumuni ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007
Lengo kuu la Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11ya 2007 limeainishwa katika kifungu cha 4 cha Sheria hii ikiwa ni kuhakikisha ustawi wa utawala bora na kuondoa rushwa nchini. Ili kuhakikisha lengo hili linatimia, sheria hii inaweka mazingira bora kisheria, kiutawala, na kiutekelezaji yenye mwelekeo wa Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini. Hivyo, sheria hii itawezesha:
  • Kuwepo ushauri juu ya mienendo na taratibu mbalimbali katika utekelelezaji wa shughuli za umma, mashirika ya umma, taasisi binafsi nchini kwa lengo la kuifanyia kazi ya kung’amua na kuzuia rushwa kuwa ya ufanisi
  • Upatikanaji wa habari au taarifa mbalimbali kuhusu athari za rushwa na vitendo mbalimbali vya rushwa nchini;
  • Kuwezesha au kufanikisha ushirikiano mzuri na wenye manufaa kati ya taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi, zinazojihusisha na mapambanodhidi ya rushwa ;
  • Kuhimiza ustawi, na kuimarisha ushiriki wa umma kwa ujumla katika kupambana na rushwa nchini ,na
  • Kuwezesha kufanyika kwa uchunguzi, upelelezi na uendeshaji wa mashtaka dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa nchini.
UONGOZI WA TAKUKURU
Kati ya mwaka 1973 – 1990 Taasisi (TAKURU)  iliongozwa na Mkurugenzi akisaidiwa na Wakurugenzi Wasaidizi chini ya Idara zao. Kati ya  mwaka 1991- 2007 Taasisi iliongozwa na Mkurugenzi Mkuu akisaidiwa na Wakurugenzi wa Idara. 

Kuanzia mwaka 2007 hadi sasa TAKUKURU imekuiwa ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu akisaidiwa na Naibu Mkurugenzi Mkuu na Wakurugenzi wa Idara na huteuliwa na Rais. Toka mwaka 1973 hadi sasa TAKUKURU imeongozwa na Wakurugenzi wafuatao :
  • 1973 – 1974: Ndugu Geofrey Sawaya
  • Machi,1974 – Juni,1975: Ndugu S. Rutayangirwa
  • Juni,1975-1990: Ndugu Zakaria Maftah
  • April,1990 – Novemba, 2006: Major General (Rtd), Anatory Ruta Kamazima
  • Novemba, 2006 – Disemba, 2015: Edward Gamaya Hoseah
  • Machi, 2015-Sasa: Ndugu Valentino Longino Mlowola
Chanzo:   www.pccb.go.tz

Monday, June 4, 2018

MKUU WA WILAYA MUFINDI AWATAKA WAZAZI KUCHANGIA CHAKULA SHULENI.





 Mkuu wa Wilaya ya Mufindi amewataka wazazi na walezi waendelee kuchangia chakula cha mchana kwa wanafunzi wa kutwa kwa shabaha ya kuinua kiwango cha ufaulu, kupunguza utoro pamoja na kuleta usawa miongini mwao.

Akiongea na wananchi wa Igowole katika kilele cha wiki la kusoma  lililofanyika katika Viwanja vya shule ya Msingi Igowole iliyopo Halmashauri ya Wilaya Mufindi, Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Bwana Joseph Mchina, amewataka vingozi wa serikali za vijiji kuendelea kutekeleza mkakati wa utoaji wa chakula cha Mchana shuleni kwa kuwamasisha wazazi kuchangia kwa mujibu wa sera ya Elimu bila malipo.

Aidha, amewapongeza viongozi wa siasa ambao wamekuwa bega kwa bega katika kuelimisha jamii na wazazi kuhusu umuhimu wa utoaji wa chakula cha mchana shuleni.

 “Napenda kupongeza kata zote ambazo zinazotoa chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni, utoaji wa chakula cha mchana shuleni huleta usawa kati ya walionacho na wasionacho, huimarisha mahudhurio ya wanafunzi shuleni huongeza usikivu wa wanafunzi darasani na hutunza muda wa ratiba nzima ya shule” alisema Mchina

Akitoa taarifa kwa mgeni rasmi, Afisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bwana Kennedy Bukagile, alisema Halmashauri ya Wilaya Mufindi imejiwekea mkakati mzuri wa kuwapatia wanafunzi chakula cha mchana ili kuimarisha usikivu  na mahudhurio shuleni,

 “wazazi wamejitoa kulima shamba la maharage na Mahindi lenye jumla ya hekari 294 kwa ajili ya chakula cha mchana kwa wanafunzi shuleni”        
            
Afisa huyo mwenye dhamana ya Elimu, ameongeza kuwa, Idara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wamewezesha kamati za shule kujengewa uwezo wa uhamasishaji na pia kuwa na wahamasishaji jamii  wa masuala ya  elimu kwa kila shule, wakishirikiana na kamati za shule kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata chakula cha mchana jambo ambalo limesabisha kuongezeka kwa ufaulu sanjari na kushuka kwa takwimu za utoro.

Kwa upande mwingine Maadhimisho hayo yalienda sambamba na maonesho ya mabanda ya elimu na mashindano ya wanafunzi katika stadi za KKK, ambapo washindi wa shindano hilo walitangazwa na kupewa zawadi na Mgeni rasmi ambapo nafasi ya kwanza ilichukuliwa na Mwanafunzi Anania Ng’umbi, darasa la pili wa Shule ya Msingi Igowole.

Aidha “kujua kusoma na kuandika ni haki ya kila mtu jambo hilo linamsaidia mtu kuwa na uwezo na njia yenye kumuwezesha kufanya maendeleo katika maisha yake pamoja na watu wengine”, Tamko la Shirika la UNESCO

Maadhimisho ya Wiki la Kusoma yanalenga kukuza na koungeza ari ya ushindani katika kujifunza stadi za msingi za kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) Ujumbe wa wiki la elimu mwaka huu ni Stadi za KKK ni Msingi wa Elimu, tuwekeze katika Elimu kuelekea Uchumi wa Viwanda