Mkutano maalumu wa
baraza la madiwani la Halmashauri ya Mji
Mafinga leo limepitisha rasimu ya mpango wa bajeti ya kipindi cha mwaka wa
fedha 2019/2020 na kuidhinisha kukusanya
na kutumia zaidi ya Bilioni 25.2 kwa ajili ya matumizi ya
mishahara, mengineyo na miradi ya maendeleo.
Akisoma rasimu hiyo
kwa niaba ya Mkurugenzi, Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana
Andambikye Kyomo amesema zaidi ya Bilioni 3.9 zinakadiriwa kukusanywa kutokana
na vyanzo mbalimbali vya mapato ndani ya Halmashauri.
Makisio hayo ni zaidi
ya milioni 648.8 ambayo ni asilimia 20% ukilinganisha na makisio ya mwaka
2018/2019 ya zaidi ya Tsh Bilioni 3.3, aidha katika mapato hayo kiasi cha zaidi
ya Tsh milioni 602.8 ni mapato ya vyanzo fungiwa katika idara ya afya na elimu
sekondari hivyo kufikia mapato halisi kuwa zaidi ya Bilioni 3.3.
Baraza hilo
limeridhia pia matumizi ya kawaida kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ambapo zaidi ya
Bilioni 17.8 zimeidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na mishahara ,
kati ya fedha hizo kiasi cha zaidi ya Tsh Bilioni 13.8 ni kwa ajili ya mishahara, na
zaidi ya Bilioni 4 ni kwa ajili ya
matumizi mengineyo.
Aidha baraza hilo
limeidhinisha pia kukusanya na kutumia zaidi ya Bilioni 7.3 kwa ajili ya
kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato kati ya
fedha hizo zaidi ya bilioni 4.7 ni kutoka ruzuku ya serikali kuu, wahisani zaidi
ya milioni 490, Halmashauri inatarajia kuchangia zaidi ya Bilioni 1.3 sawa na
asilimia 40% ya mapato halisi ya ndani ya Halmashauro na nguvu ya wananchi wanatarajia
kuchangia zaidi ya milioni 768.
Akieleza matarajio
ya utekelezaji wa rasimu ya bajeti hiyo ya 2019/2020 Kaimu Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Voster Mgina ametanabaisha kwamba bajeti hiyo italenga
kuimarisha mifumo ya ukusanyaji na kuongeza mapato ya ndani, kuongeza viwanda
na fursa za uwekezaji, kuboresha huduma za usafi katika mji, kuboresha makazi
na mipango miji sanjari na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi na vitendea
kazi na hatimae kukamilisha miradi viporo iliyoanzishwa siku nyingi katika
sekta ya afya, elimu utawala na ujenzi.
Akiongoza baraza
hilo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe. Charles Makoga amewahakikishia
wananchi wa Mafinga kwamba bajeti hiyo iliyoidhinishwa leo hii itaenda kutekelezwa
ipasavyo na imelenga kutatua kero za wananchi.
“Sisi
kama watekelezaji wa ilani ya chama cha mapinduzi wote kwa pamoja kwa
kushirikiana na madiwani wa chadema kwa pamoja tunashirikiana kuhakikisha
bajeti hii inaenda kutekelezwa katika kata zetu zote kama iliyopangwa bila
kujali vyama vyetu kwani maendeleo hayana chama”
Alisema
Aidha ameeleza
kwamba katika kuendelea kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt John Magufuli za kuleta
elimu bure na matokeo chanya yanayotokea ya ongezeko la wanafunzi, Halmashauri
yake imejiandaa kuongeza kujenga shule mbili za Sekondari mpya ikiwemo ya
vipaji maalumu na nyingine ya Wasichana itakayojulikana kwa jina la Mafinga
Girls hii ni kutokana na ongezeko la ufaulu wa mtihani wa darasa la saba ambapo
halmashauri hiyo imefikia asilimia 92.86% ya ufaulu kwa mwaka 2018 na kushika
nafasi ya kwanza katika mkoa wa Iringa.
Kwa upande wake mwakilishi
wa Mkuu wa Wilaya Mufindi Kaimu Katibu Tawala (DAS) Bwana Joseph Mchina
ameipongeza Halmashauri ya mji wa Mafinga kwa kuwa na usimamizi mzuri wa
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Waheshimiwa
Madiwani endeleeni kushirikiana na wataalamu hawa wa Halmashauri na wananchi
kwa ujumla katika kufanikisha utekelezaji wa miradi yetu kwa viwango vyenye
ubora unaotakiwa ambavyo thamani yake ya fedha inaonekana ili kuchochea
maendeleo ya wananchi na kufikia kipato cha kati kwa manufaa ya sasa na ya kizazi
kijacho” Alisema.
Mapendekezo ya
Bajeti ya mwaka 2019/2020 yameandaliwa kwa kuzingatia mambo yafuatayo, Muongozo
wa Bajeti wa 2019/2020, Ilani ya Uchaguzi ya chama Tawala –Ccm ya 2015/2016
-2019/2020, Malengo ya Maendeleo endelevu (SDGs), Dira ya Taifa ya maendeleo
2025, Maelekezo ya Ki- Sekta na Mpango wa maendeleo wa miaka mitano na mpango
mkakati wa Halmashauri pamoja na vipaumbele vya Taifa kama vilivyofafanuliwa na
Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli wakati wa
kufunga bunge la 11 Mjini Dodoma.
Vilevile umezingatia mwongozo wa Serikali wa kuandaa mipango na Bajeti wa mwaka 2019/2020 uliotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango mwezi Disemba 2018 ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya Bajeti Namba 11 ya mwaka 2015 sehemu ya 21 na 22.
HABARI PICHA
No comments:
Post a Comment