Na
Amani Mbwaga, Dar es salaam
Waziri wa viwanda
na Biashara nchini Tanzania Mhe. Innocent Bashungwa Mapema leo hii amefanya
ziara katika viwanda vya nguo kikiwemo cha NIDA na kile cha NAMERA vya jijini Dar es salaam.
Akiongea mara baada
ya kutembelea viwanda hivyo Mhe. Bashungwa amesema lengo la ziara hiyo ni
kupita katika viwanda vyote vya nguo nchini kujua changamoto zao na kisha
serikali kuzifanyia kazi na hatimae kuwa na uzalishaji endelevu wa zao la pamba na kuwanufaisha wakulima.
“Mimi nimekuja hapa
kwa ziara mahususi, Wakulima wetu wa pamba wamehamasika sana kulima pamba,
Msimu huu wa mwaka 2019 tunategemea kuvuna
zaidi ya Tani Laki 4 za pamba kutoka tani Laki 220,000 za mwaka jana kwa
hiyo tuna pamba za kutosha” alisema Mhe.
Bashungwa.
Aidha amesisitiza
kwamba wakulima kwa upande wao wametimiza wajibu wao hivyo ni jukumu la
Serikali kupitia wizara ya viwanda na biashara kuwatafutia masoko yenye tija.
“Kwa muda mrefu
soko la pamba limekuwa likitegemea mlango mmoja tu, wakati wa enzi za Baba wa
Taifa Mwl. Julius Nyerere kulikuwa na viwanda vingi vya nguo na vilikuwa
vinafanya kazi ipasavyo na kama vyote vingekuwepo basi kusingekuwepo na
changamoto ya masoko katika zao la pamba hivyo ni wakati sasa wa viwanda vilivyopo na
vitakavyojengwa kuhakikisha vinafanya kazi ipasavyo na Kuongeza Uzalishaji mara mbili zaidi ili kuendana na kasi ya sasa
ya Tanzania ya Viwanda".
Nchi ikifanikiwa kuchakata
kila zao na kuliongezea thamani basi itakua ni chachu ya ongezeko la
ajira hapa nchini na hatimae kukuza uchumi wa
taifa na wananchi kwa ujumla.
Dira kuu ya Wizara ya Viwanda na Biashara
ni "Kuwa na msingi shindani wa viwanda, mazingira bora ya uwekezaji
na ukuaji wa biashara unaowezesha kukua kwa uchumi shirikishi na
endelevu."
Waziri Bashungwa
ataendelea na ziara hiyo nchi nzima baada ya Kuanza na Mkoa wa Kilimanjaro hapo
jana na leo hapa Jijini Dar es salaam.
MATUKIO KATIKA PICHA
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa akiangalia Bidhaa zinazotengenezwa na Kiwanda cha Nguo NIDA Wakati wa ziara yake.
|
Pamba ikiwa katika Hatua za awali za uchakataji |
Waziri wa Viwanda na Biashara (Katikati) akipokea maelezo ya namna Pamba inavyoanza kuchakatwa katika hatua za awali |
Shughuli za Uzalishaji Kiwandani zikiendelea |
Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Innocent Bashungwa (Kulia) akimsikiliza kwa Makini Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Nguo NIDA na NAMERA (Picha zote na Amani Mbwaga) |
No comments:
Post a Comment