Sunday, September 16, 2018

RC Hapi Atamani Rais Magufuli Kuweka Jiwe la Msingi Ujenzi wa Ofisi za Utawala Halmashauri ya Mji Mafinga.

Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Ally Hapi akiongea na wananchi baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa ofisi za utawala za Halmashauri ya Mji Mafinga

Na Amani Mbwaga, Mafinga-Iringa

Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe. Ally Salum Hapi ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya Iringa Mpya ya Tarafa kwa Tarafa alipotembelea, Kukagua na kuridhika na maendeleo ya ujenzi wa mradi wa ofisi za utawala zinazojengwa kwa pesa za serikali chini ya Kampuni ya Ujenzi ya SUMAJKT katika eneo la Luganga Mjini Mafinga Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.

Amewataka wakala wa majengo ya serikali (TBA) kusimamia mradi huo ipasavyo ili viwango vilivyoanishwa vionekane na thamani ya fedha iliyotumika nayo ionekane na kama Mhe Rais akija Mafinga basi Mkuu wa Mkoa Iringa anatamani Mhe Rais aweke jiwe la msingi la jengo hilo ili aone fedha anazotoa za serikali zinafanya kazi.

“Hivyo kwa kipekee nimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe DKT. John Pombe Magufuli kwa kuona umuhimu wa kuleta fedha hizi kwa ajili ya kujenga jengo hili kwa wananchi wa Mafinga na ni imani yangu kwamba watu wengi zaidi ya 200 hapa wamepata ajira kwa hiyo sehemu kubwa ya fedha imerudi mifukoni mwa wananchi na akina mama wapo hapa wanauza chakula kwa Mafundi” alisema Mhe Hapi.

Aidha ametoa rai kwa wasimamizi na waliopewa dhamana ya kusimamia miradi wahakikishe wanaisimamia vizuri ili fedha ya serikali itumike kwa makusudi na dhamira iliyokusudiwa.

“Mradi huu na miradi mingine yote, Wakurugenzi mnawajibika kuisimamia ipasavyo na kufuatilia kwa makini ili kuhakikisha kila senti ya serikali inayoletwa hapa inatumika kwa makusudi yaliyopangwa” alisema Mhe Hapi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi Saada Mwaruka  aliishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuwapatia fedha na kuanza kwa ujenzi huo unaotarajia kukamilika tarehe  30 Machi , 2019.

“Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Serikali kwa kuwezesha utekelezaji wa Mradi huu ambao hadi kukamilika utaondoa adha tuliyonayo kwa sasa ya uhaba wa vyumba vya Ofisi na ukumbi wa Mikutano” alisema Bi Saada Mwaruka.

Changamoto ya uhaba wa Ofisi za idara na Vitengo iliyopo sasa ilipelekea kuwasilisha ombi serikali kuu kuwezeshwa fedha za ujenzi wa jengo la utawala.

Na katikati ya mwaka 2016/2017 iliidhinishiwa bajeti ya ujenzi wa jengo la utawala.

Ujenzi wa Jengo hilo unagharimu jumla ya kiasi cha zaidi ya Tsh Bilioni 3.38 mpaka kukamilika, lakini mpaka sasa Halmashauri imepokea jumla ya Tsh Bilioni 2 kwa awamu mbili tofauti awamu ya kwanza mwaka wa fedha 2016/2017 ilipokea jumla ya Tsh. Milioni 500 na awamu ya pili mwaka wa fedha 2017/2018 ilipokea jumla ya Tsh. Bilioni 1.5

Fedha hizo ni kutoka wizara ya Fedha na Mipango kupitia Ruzuku ya Miradi ya Maendeleo mpaka sasa jumla ya Tsh. Bilioni 1.3 zimetumika.

Mradi huo unajengwa na Mkandarsi National Services Construction Department (SUMAJKT) kwa gharama ya Tshs Bilioni 3.38 chini ya Mkataba namba LGA.169/2016-2017/HQ/W/06 na unasimamiwa na Wakala wa Majengo wa Serikali (TBA).

Ujenzi ulianza kwa kupima udongo na kufuatiwa na kazi ya kuchimba msingi wa jengo, kumimina nguzo na linta zake, kumimina sakafu hadi ghorofa ya kwanza. Mpaka sasa ujenzi huu umefikia asilimia 60 ya mpango kazi (Framework).

Kazi zinazoendelea kufanyika kwa sasa ni kupiga lipu ghorofa ya chini na kujenga kuta ghorofa ya kwanza.

Aidha, kwa kuzingatia mpango kazi wa mkataba mkandarasi yupo mbele ya ratiba kwa mwezi mmoja.

Hadi kukamilika kwa mradi huu utawezesha Halmashauri ya Mji kuwa na ofisi za uhakika kwa ajili ya utoaji wa huduma na kuondoa adha ya uhaba wa vyumba vya ofisi.

Wakati wa utekelezaji wa mradi huo umekuwa na manufaa kwa wakazi wa Mji wa Mafinga na maeneo yanayozunguka eneo la mradi kwani umekuwa ni chanzo cha kipato kwa kupitia ajira za muda mfupi na wafanyabiashara wadogo wadogo na wakubwa.

Jumla ya wakazi 211 kati yao wanawake 68 na wanaume 143 wamepata ajira kutokana na mradi huu.

Mradi wa ujenzi wa jengo la utawala katika Halmashauri ya Mji Mafinga ulianza kujengwa tarehe 22.9.2017 na unatarajiwa kukamilika Tarehe 30 Machi 2019.

Halmashauri ya Mji Mafinga ilianzishwa tarehe 01, Julai 2015, ikianzishwa kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.

Wakati inanzishwa ilikuwa na uhaba wa ofisi za kuwezesha idara na vitengo kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, Halmashauri ililazimika kuazima baadhi ya majengo ya Halmashauri ya Mufindi na kuyatumia kama Ofisi ya Halmashauri ya Mji Mafinga.

HABARI PICHA
Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Ally Hapi akiongea Na Wakazi wa kijiji cha Luganga baada ya Kukagua Mradi wa Ujenzi wa ofisi za Utawala za Halmashauri ya Mji Mafinga








Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William akimshukuru  RC Hapi baada ya Ukaguzi wa Jengo la Utawala
Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Hapi akisalimiana na mmoja wa Wananchi wa Mtaa wa  Luganga na Kusikiliza kero yake kubwa ya Upatikanaji wa Maji katika mtaa wake

Jengo la Ofisi za Utawala Halmashauri ya Mji Mafinga likiwa katika hatua nzuri ya Ujenzi



Muonekano wa Juu








Ukaguzi ukindelea
Picha zote na Amani Mbwaga
Kwa Maoni au Ushauri wasiliana nasi
Mob+255 656 632 566
E-mail:prof.mbwaga@gmail.com



No comments:

Post a Comment