Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Ally Salum Hapi akikagua gwaride la Vijana wa JKT Mujibu wa Sheria Operesheni Mererani Wakati akifunga Mafunzo hayo katika kikosi cha Jeshi Mafinga (Picha na Amani Mbwaga) |
Na Amani Mbwaga, Mafinga
Mkuu wa Mkoa wa Iringa
Mhe Ally Salum Hapi akiwa Mgeni Rasmi Leo amefunga mafunzo ya awali ya kijeshi
kwa vijana wa Mujibu wa Sheria 2018 Oparesheni Mererani katika Kikosi cha Jeshi
Mafinga JKT Kilichopo Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.
Hapi amewataka vijana
kufanya kazi kwa bidii, kuepuka vitendo vyote viovu, kukemea rushwa, uvivu
usaliti, ukosefu wa maadili na uvunjaji wa sheria za nchi.
“Serikali yetu chini ya
Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli inathamini na kutambua mchango wa vijana
katika Taifa hili na ndio maana imeendelea kugharamia mafunzo yenu kwa kila
namna hivyo kwa pamoja tunakila sababu ya kuipongeza serikali yetu kwa kutambua
juhudi hizi, ni imani yetu kwamba mtatuunga mkono katika ujenzi wa Tanzania ya
Viwanda” alisema Mhe Hapi
Amewasihi vijana kwenda
kuishi kwa mujibu wa kiapo walichoapa, wakawe mfano kwa vijana wengine ili
waige mema waliyojifunza ikwemo kuwa na nidhamu ya kijeshi katika maisha yao na
kuzingatia mambo makuu matatu kwa mwanajeshi ambayo ni Uaminifu, Utii, na
Uhodari katika kufanya kazi na kulinda rasilimali za Taifa.
Mafunzo ya awali ya
kijeshi kwa vijana wa mujibu wa sheria Oparesheni Mererani yalifunguliwa rasmi
na aliyekuwa Kamanda Kikosi Kanali Hamis Maiga mnamo tarehe 25 Juni 2018 kukiwa
na vijana 1438 kati yao wasichana idadi 363 na wavulana idadi 1075.
Mpaka leo vijana
waliomaliza mafunzo idadi ni 1416 wavulana wakiwa idadi 1055 na wasichana 361
baada ya vijana 20 kati yao vijana 19 ambao ni wavulana na msichana 01 kuacha
mafunzo kwa sababu ya utoro na vijana 02 kupata uhamisho kwenda Ruvu JKT.
Katika kipindi chote
cha mafunzo vijana hawa wamejifunza mambo mbalimbali ikiwemo masomo ya nadharia
ambayo yalijumuisha masomo ya uraia, mbinu za kivita na afya.
Pia wamefundishwa mafunzo
ya vitendo ikiwemo utimamu wa mwili, mafunzo ya porini, kwata na stadi za kazi
ikiwemo kilimo, ufugaji na utunzaji wa mazingira.
Aidha Mkuu wa Wilaya
Mufindi Mhe Jamhuri William alisema Wilaya ya Mufindi inanufaika sana na uwepo
wa Kikosi cha Jeshi Mafinga na vijana hao kuwepo kikosini kwani toka wamefika
hajawahi kupata taarifa yoyote mbaya kuhusiana na utendaji wao wa kazi.
“Vijana hawa wamekuwa
mfano wa kuigwa na jamii yetu inayowazunguka na mufindi kwa ujumla hivyo
ninawaomba mkawe mabalozi wazuri kwa kuitangaza vyema wilaya yetu Mufindi, Mkoa
wetu wa Iringa na Tanzania kwa Ujumla” alisema Mhe William.
Kwa upande wake
Mwakilishi wa Mkuu wa JKT Kanali Ahmed Abas Ahmed ambaye anamuwakilisha Mkuu wa
JKT Meja Jenerali Martin Busungu alisema waasisi wa taifa hili waliona umuhimu
kwa vijana wa Tanzania kupata malezi yanayoendana na misingi ya Taifa letu
ndipo wakaaamua kuanzisha chombo hiki JKT kitakachowalea vijana ili waendane na
desturi na utamaduni wa Taifa letu.
“Pamoja na jukumu hilo
la msingi la Jeshi la Kujenga Taifa liliongezewa majukumu ya uzalishaji mali na
ulinzi, majukumu hayo matatu yanalenga kuwaandaa vijana kuwa na moyo wa
uzalendo na kupenda kazi za mikono, kijutuma, kulinda na kutetea nchi yetu”
alisema Kanali Ahmed.
Naye Mkuu wa Kikosi cha
JKT Mafinga Luteni Kanali Issa Daud Chalamila alieleza baadhi ya changamoto
zilizojitokeza katoka mafunzo hayo ya Vijana wa mujibu wa Sheria 2018 ikiwemo
Vijana kuchelewa kuripoti vikosini kwa ajili ya kuanza mafunzo kwa wakati baada
ya kuchaguliwa kujiunga na JKT, Muda wa mafunzo kuwa mfupi, kuingiliwa kwa
ratiba za udahili wa vyuo vikuu na uombaji wa mikopo ya elimu ya juu ambapo
hupelekea kusimamishwa kwa kozi kwa takribani wiki mbili, changamoto zingine
ziligeuzwa kuwa fursa.
Luteni Kanali Chalamila
akitoa nasaha kwa vijana alisema “Vijana wetu mnaomaliza leo mafunzo haya naomba
niwakumbushe kuwa ninyi ni miongoni mwa vijana wachache mliopata fursa ya kufanya
mafunzo ya JKT, kupitia kodi za wananchi, serikali imegharamia mafunzo yenu hivyo mnalo deni la kulipa, mkawe wazalendo
wa kweli kwa Taifa lenu na kuiunga mkono serikali kwa kufanya kazi kwa bidii
ili kuleta maendeleo kwa kuzingatia sera ya Hapa kazi tu na pia muwe chachu ya
mabadiliko chanya yenye kuleta tija na ufanisi katika jamii ya Tanzania
kuelekea Tanzania ya Viwanda”.
JKT ilianzishwa Julai
10, 1963 katika uwanja wa ndani wa Michezo wa Taifa (Indoor Stadium) Majira ya
saa Kumi Jioni ambapo viana 11 wakiwa makatibu wa Tanzania Youth League (TYL) walijiunga
kwa mafunzo katika kambi ya JKT Mgulani Jijini Dar es salaam.
Katika uzinduzi huo
Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere alihutubia taifa akisema kuwa “umuhimu
wa JKT ni Taifa kuhitaji huduma ya vijana kulitumikia Taifa lao katika majukumu
mbalimbali yatakayotolewa ama kujitokeza kijamii, kiuchumi, kielimu na
kiitikadi”
Sanjari na hilo mwaka
1964 ilitungwa sheria ya JKT (National Service Act) ambayo ilimpa madaraka
Mkurugenzi wa JKT Kuandikisha vijana wa kujitolea kujiunga na Mafunzo.
Sheria hiyo ilifanyiwa
marekebisho mwaka 1966 na 1967 ili kuwezesha vijana waliokuwa wakihitimu elimu
ya sekondari ya kidato cha nne na sita kujiunga JKT Kwa mujibu wa sheria.
Kufuatia marekebisho
hayo kulitoa fursa kwa kundi la vijana 11 kujiunga na JKT Kwa mujibu wa sheria
ambao walitawanywa katika vikosi mbalimbali vya mafunzo.
Baadhi ya Vijana hao ni
aliyekuwa Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) na Makamu wa kwanza
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania marehemu mzee Aboud Jumbe, Makamu wa
kwanza wa Rais na Waziri mkuu Marehemu Rashid
Kawawa na Spika wa Bunge Hayati Chifu Adamu Sapi Mkwawa wakiwa
operesheni Kazi “A”
Mwaka 1975 JKT
Iliunganishwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ambapo majukumu
yake ya malezi kwa vijana na uzalishaji mali na ulinzi wa Taifa yalibaki katika
taasisi hiyo, hivyo ilikuwa Kamandi ya Uzalishaji mali ya Jeshi.
Mafunzo ya JKT kwa
vijana wa Kujitolea na mujibu wa sheria yaliendelea kwa ufanisi mpaka mwaka
1994 serikali ilipositisha kwa sababu mbalimbali za kiuchumi.
Kusitishwa kwake watafiti
walisema kuwa jamii ilishuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili na uwajibikaji
usiozingatia nidhamu hasa kada ya vijana.
Mmmomonyoko huo
ulizusha malalamiko ya Makundi mbalimbali ya jamii yakitaka kurejeshwa kwa
taasisi hiyo hali iliyowezeshwa na serikali ya Awamu ya tatu chini ya Rais na
Amiri Jeshi mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe Benjamini William Mkapa kuyahisha mwaka 2001 kwa vijana wa
kujitolea.
Mnamo Machi 26 mwaka
2013 serikali ya Awamu ya nne chini ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Mjeshi ya
Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete Alizindua
upya mpango wa Mafunzo ya JKT kwa vijana wa Mujibu wa Sheria.
JKT inachangia sana
kuimarika kwa umoja wa kitaifa ambapo vijana wengi wanaohitimu mafunzo haya
wanapenda kufanya kazi za mikono kwa moyo, kujituma, kujitolea ujasiri,
uvumilivu, ushirikiano na nidhamu.
Aidha Mnamo Machi 15
mwaka 1967 Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mafinga kilianzishwa
baada ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya ulinzi na Usalama wa awamu ya
kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere
kukabidhiwa shamba lililokuwa likimilikiwa na Kabaila wa Kizungu Bwana Lord
Cheseum, litumike kwa mafunzo ya vijana, Ufugaji na Kilimo.
Mkuu wa Kikosi wa
Kwanza alikuwa ni Senior Master EP Njau aliyeweza kutekeleza majukumu yake kwa
weledi, uadilifu, uaminifu na nidhamu ya hali ya juu ya malezi ya vijana na miradi
ya uzalishaji mali.
Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Ally Hapi Akipokea Salamu ya Heshima |
Mkuu Wa Mkoa Iringa Mhe Ally Hapi akikagua Kikundi cha Brass Band cha Mafinga JKT Wakati wa Mahafali ya Vijana hao yaliyofanyika leo |
Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Ally Hapi Akiteta jambo na Kamanda Kikosi wa Mafinga JKT Luteni Kanali Chalamila |
Kikundi cha Singe |
RC Hapi Akiwa katika Eneo la vikwazo |
Picha zote na Amani Mbwaga
Kwa Maoni au Ushauri Wasiliana nasi;
Mob: +255 656 632 566
E-mail Prof.mbwaga@gmail.com
No comments:
Post a Comment