Wednesday, September 19, 2018

DC Mufindi Amaliza Mgogoro wa Ardhi uliodumu Miaka 12 na Kurudisha Ekari 643



Na Amani Mbwaga, Mafinga Iringa
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William amemaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda wa miaka 12 baina ya Mwekezaji Tom Duvile Mkurugenzi wa Highland Holding Company dhidi ya Wananchi wa Kinyanambo na Kijiji cha Kikombo ambapo zaidi ya ekari 643 zilizonunuliwa kinyume na utaratibu na sheria zimerudishwa kwa wananchi na Halmashauri ya Mji Mafinga.

Ekari zilizorejeshwa ni 396 kwa wananchi 17 walalamikaji kutoka katika kata ya Kinyanambo, ekari 87 za Kijiji cha Kinyanambo, ekari 79.9 za kijiji cha Kikombo zimerudishwa kwa Halmashauri ya Mji Mafinga  na Ekari 80.1 zimerudishwa kwa wananchi mbalimbali wa kijiji cha Kikombo.

Mhe William alibainisha kuwa mara baada ya kukabidhiwa ofisi ya Ukuu wa wilaya alikutana na malalamiko ya wazee 17 kutoka Mtaa wa Kinyanambo ambapo viongozi waliopita walijaribu kuutatua lakini haukufikia muafaka ndipo yeye akaamua kuunda tume ya wataalamu mbalimbali wakiwemo wa ardhi kupitia upya madai ya hao wazee na pia kufika katika eneo la ardhi linalolalamikiwa na mwekezaji huyo.

Mgogoro wa ardhi kati ya wananchi 17 wa kata ya kinyanambo dhidi ya mwekezaji ndugu Tom Duvile ambaye alivamia mashamba ya wananchi waliyopewa na serikali ya kijiji cha kinyanambo  mwaka 1977 na lalamiko lao walipeleka kwa mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi tangu mwaka 2006 hawakupatiwa ufumbuzi.

“Nimechukua muda mrefu sana kushughulikia tatizo hili nilikuwa nataka nione mimi mkuu wa Wilaya nimekuja sasa ni miaka 03 imepita lakini wenzangu walitangulia niliona walitatua vipi mgogoro huu na walikwama wapi kwa hiyo nilikuwa nataka kujiridhisha na ndio maana suala hili limechukua muda mrefu sana” alisema Mhe William

Mgogoro huu ulishatolewa maamuzi na viongozi mbalimbali akiwepo aliyekuwa Mkuu wa Wilaya Mufindi Bi Evarista Kalalu lakini maamuzi hayo hayakutekelezwa hivyo mgogoro huo uliendelea.

“Na leo hii ninmekuja kutoa uamuzi kero yenu inaisha leo kwani waswahili husema mvumilivu hula mbivu, wananchi waliolalamika na mwekezaji kila mtu atapata anachostahili na hivyo ndio serikali yetu inavyofanya kazi kusikiliza kero na kuzitatua” alisistiza Mhe William.

Mhe William ameongeza kwamba katika mgogoro huo ofisi yake ilibaini kwamba taratibu za ununuaji wa ardhi hiyo zilikiukwa.
Ardhi inayolalamikiwa ni ekari 396 na hakuna mkutano mkuu ulioridhia uuzwaji wa ardhi hiyo.

Viongozi wa vijiji vya Kinyanambo, Kikombo na Ndolezi walipaswa kuwasilisha mapendekezo ya mkutano mkuu wa kijiji unaoonesha kukubali mauzo ya ardhi hiyo kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi ambae angewasilisha kwenye kamati ya ugawaji ardhi ya Halmashauri ya Mufindi kwa vile ardhi iliyouzwa ilikuwa zaidi ya ekari 50 zinazoruhusiwa kisheria kugawiwa na kijiji.

Kwa mujibu wa tume ya wataalamu iliyoundwa na Mkuu wa wilaya ilibaini mapungufu ya msingi ikiwemo kijiji cha Kikombo eneo ambalo uongozi wa kijiji walionesha ekari 79.9 ambalo limezidi kutolewa kwa mujibu wa sheria ambapo walitakiwa kutoa ekari zisizozidi 50.

Katika Kijiji cha Kinyanambo Kijiji kilimpa mwekezaji  ekari 100 na ekari 13 ziliingia kwa ndugu mawazo Chengula hivyo eneo la kijiji lililouzwa ni ekari 87 ambalo pia lilitolewa kinyume na sheria ya ardhi ya vijiji.

Vilevile Ndugu Tom Duvile alinunua jumla ya ekari 249.5 kutoka eneo la kijiji na wananchi mbalimbali lakini baada ya upimaji imebainika kuwa eneo la kinyanambo lina ukubwa wa ekari 483 na kufanya zidio la ekari 233.5

Kutokana na mapungufu hayo ofisi ya Mkurugenzi wa mji Mafinga ilimtaarifu Kamishina wa ardhi kwa barua yenye kumbukumbu Namba HM/MF/A.30/76 ya tarehe 28/11/2016 na ushauri wake ulikuwa, mnunuzi afuate taratibu za umilikishaji wa ardhi ambazo zipo kisheria.

Mkuu wa Wilaya Mufindi baada ya kupitia hatua zote na kujiridhisha kwamba mwekezaji hakufuata taratibu na sheria za nchi ametoa maagizo ya utekelezaji ikiwemo maeneo yote yaliyouzwa bila kufuata utaratibu yarejeshwe mara moja kwa mamlaka husika au mwekezaji afuate upya taratibu za kupata maeneo hayo ikiwemo kujulikana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

“Naagiza eneo lipatalo ekari 166 kuanzia sasa linarejeshwa kwa Halmashauri ya Mji Mafinga, maeneo ambayo yalinunuliwa kwa wananchi bila kufuata sheria na taratibu katika kijiji cha Kikombo hekari 80.1 kunzia sasa yanarudi kwa wananchi na Jumla ya ekari 396 kuanzia sasa hivi zinarudishwa kwa wananchi 17 wa kata ya Kinyanambo waliokuwa wakilalamika kwa muda mrefu” alisema Mhe William

Aidha eneo ambalo Mwekezaji Bwana Tom Duvile alinunua kwa familia ya Mdeka eekari 451 atabaki nazo na hilo ndio eneo alilopata kihalali lakini inaambatana na maelekezo yafuatayo kwa kuwa yeye ni raia wa kigeni basi afuate taratibu na sheria za kujimilikisha eneo hilo alisisitiza Mhe William.

Mwekezaji Bwana Tom Duvile kwa upande wake hakuridhika na Maamuzi hayo huku akidai kuchangia ujenzi wa shule ya Msingi katika kijiji cha Kikombo kama ngao yake ya kuendelea kumiliki ardhi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kinyanambo  Mhe Chesco Lyuvale alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kufikia maamuzi hayo kwani hata yeye toka ameingia udiwani amekutana na tatizo hilo na lilikuwa likimsumbua kwa muda mrefu hadi kulipeka kwenye chama chake ccm  lakini lilikuwa bado haijatatuliwa.

“Ndugu zangu kwenye ukweli tuseme ukweli na kwenye haki ya mtu tusimame kwenye haki ya mtu, sisi hatujapanga kumuonea Bwana Tom Duvile mimi nasema wewe mkuu wa Wilaya umemaliza kama yeye haridhiki na maamuzi haya, sisi hatumlazimishi aridhike yeye anaweza kwenda mahakamani ili tukapambane huko kwenye vyombo vya sheria” alisema Mhe Lyuvale.

Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Gangilonga kata ya Kinyanambo  Bwana Reginald Kivinge kwa niaba ya wananchi amempongeza Mkuu wa wilaya kwa kufanya maamuzi hayo kwa faida ya wananchi wa Kinyanambo, Mafinga na Tanzania kwa ujumla.

“Naomba nitoe pongezi kwa Mhe Mkuu wa Wilaya, ni kweli jambo hili lilianza muda mrefu na ilifikia wakati wananchi tukawa kama tumeshindwa kuwa na majibu., kiukweli nichukue nafasi hii kukupongeza wewe, kwa kweli umewatendea haki wananchi wa kata ya Kinyanambo na umeweka historia katika uongozi wako hata siku unaondoka Mafinga tutakukumbuka kwa tukio hili” alisema Bwana Kivinge

HABARI PICHA
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe Charles Makoga akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na wananchi wa Kinyanambo
Diwani wa Kata ya Kinyanambo Mhe Chesco Lyevule akiongea na Wananchi wa Kata ya Kinyanambo wakati wa utatauzi wa mgogoro wa ardhi


Baadhi ya Wazee 17 waliokuwa wakidai haki yao ya ardhi kwa muda wa miaka 12 sasa wamerejeshewa

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Bi Saada Mwaruka akitolea ufafanuzi baadhi ya hoja za wananchi wa Kinyanambo
Mwekezaji Bwana Tom Duvile 

Mwenyekiti wa Mtaa wa Kinyanambo





Afisa Ardhi Halmashauri ya Mji Mafinga  Bwana  Rajabu Bogwa




Mkuu wa Wilaya Mufindi akiongea na Wananchi wa Kijiji cha Kikombo
Picha zote na Amani Mbwaga
 Kwa Maoni au Ushauri Wasiliana nasi
Mob:+255 656 632 566
E-mail: prof.mbwaga@gmail.com

No comments:

Post a Comment