Friday, August 31, 2018

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba Akipongeza Chama cha Ushirika wa Wakulima wa Chai Mkonge – Mufindi.

Naibu waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba

Na Amani Mbwaga, Mufindi-Iringa
Naibu waziri wa Kilimo Mhe Omari Mgumba amekipongeza chama cha ushirika cha wakulima wa chai Mkonge baada ya kupata tuzo ya kuwa chama bora cha ushirika ngazi ya mkoa mwaka 2017 na mwaka huu 2018 kilipata tuzo ya mshindi ngazi ya taifa katika tasnia ya chai katika vyama vya msingi Tanzania.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu waziri wa kilimo alipokuwa katika ziara yake ya kikazi katika Kijiji cha Mkonge kata ya Luhanga Tarafa ya Ifwagi wilaya Mufindi Mkoani Iringa kwa lengo la kujionea shughuli za kilimo cha chai jinsi zinavyofanyika katika Wilaya ya Mufindi hususani kukutana na Wakulima kujua wanafursa gani changamoto, zipi na mikakati gani wanayo ili kusonga mbele katika kilimo chao.

Chama hiki kimesajiliwa kwa sheria ya nchi ya vyama vya ushirika mnamo tarehe 29 Aprili 2018 na kupewa hati Na IR 417, pia kimefanikiwa kutoa washindi wa ukulima bora kitaifa wa zao la chai, kikanda na kitaifa kwa miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2008-2012.

“Niwapongeze sana kwa ushindi mkubwa wa mkoa kanda na kitaifa kwa kuwa chama bora cha msingi wa mazao na masoko Tanzania na mlipokuwa mnapewa nafasi hii na kuchukukua kombe nilikuwepo pale Mwanza kweli mnastahili na mwanzo nilikuwa sijawafahamu vizuri lakini kwa namna tu maonesho yenu yalivyokuwa yanaendelea kila mtu aliona kwamba mnastahili kupata ngao hizi” alisema Mhe Mgumba.

 Mhe. Mgumba aliendelea kusema kuwa wanawatia moyo na pia wanawatoa kimasomaso kama serikali na Wizara ya kilimo ambayo ushirika uko chini yao ambapo wengine hubeza uwepo wa ushirika lakini chama cha ushirika Mkonge wameonesha kwa vitendo.

Mafanikio ya Chama cha ushirika wa wakulima wa Chai Mkonge ni mengi sana lakini baadhi ni ongezeko la wanachama kutoka 174 mwaka 1971 hadi kufikia wanchama 652 waliopo sasa, Upanuzi wa Mashamba ya chai kutoka hekta 118 za mwaka 1971 kufikia hekta 344 zilizopo sasa, Uzalishaji wa majani mabichi ya chai umeongezeka kutoka kilo takribani laki 856,829 za mwaka 1971 na kufikia wastani wa kilo milioni 2 na zaidi za majani mabichi kwa mwaka.

Mchango wa taasisi na mashirika mbalimbali katika kuendeleza zao la chai katika ushirikwa wa Mkonge hawakuwa nyuma, ambapo Mkonge Tea Block Farm ilipata mkopo toka kwa wahisani wenye mashariti nafuu kutoka kwa shirika la Marekani African Development Foundation (ADF) kupitia shirika la CSDI Tanzania na kutoa mkopo wa Tsh. Milioni 271.9 kwa ajili ya kuimarisha na kuendeleza zao la chai katika Ushirika wa wakulima wa chai Mkonge Wilayani Mufindi.

Halmashauri ya Wilaya Mufindi kupitia DAPS ilisaidia kukamilisha miradi minne ambayo iliibuliwa na wanachama wenyewe ikiwemo ukarabati wa barabara ziendazo mashambani kilomita 6 yeye thamani ya Tsh Milioni 80, ujenzi wa mabanda10 kwenye vituo vya kupimia chai vyenye thamani ya Tsh milioni 22, ununuzi wa Powertiler 2 zenye thamani yaTsh Milioni 16 na mradi wa ufugaji kuku Tsh milioni 2.

Wakala wa maendeleo ya wakulima wadogo wa chai Tanzania (TASHTDA) ni miongoni mwa taasisi zilizochangia maendeleo ya chai Mkonge, wao walichangi fedha kiasi cha Tsh milioni 1 na mafuta Dizeli lita 100 kusaidia ujenzi wa ofisi.
Aidha bodi ya chai Tanzania (TBT) nao wapo bega kwa bega katika kutetea haki katika tasnia ya chai katika mikataba na matatizo yanapotokea kati ya ushirika na wanunuzi wa chai basi huingilia kati pia wamejenga banda moja la mfano kwa ajili ya kupimia chai.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William alisema serikali imejitahidi kutafuta wafadhili na wadau mbalimbali ambapo tayari kuna uhakika wa kupata km 40 kutoka sawala hadi Lulanda ikiwa ni moja ya kupunguza changamoto ya miundombinu ya barabara.

Nae Diwani wa kata ya Luhanga Mhe Abeid Mhongole akitoa salamu zake kwa Naibu Waziri wa kilimo alisema wakulima wa chai katika eneo lake wamekuwa na changamoto nyingi ikiwemo bei ya mauzo ya majani mabichi ya chai kuwa ndogo, ingawa bei ya mauzo ya majani mabichi viwandani iliongezeka mwaka 2017 kutoka 250 kwa kilo hadi 287.11 pia mwaka 2018 kutoka 287.11 hadi 314.11 kwa kilo.


“Mheshimiwa Naibu Waziri bei ya kilo moja ya chai kwa sasa ni Tsh 314 lakini yeye huyu mkulima ni mmiliki wa shamba, analima kwa nguvu zake mwenyewe anagharamia mbolea pamoja na madawa lakini ukilinganisha na wenzetu wenye makampuni mfano UNLIVER mfanyakazi wa chai yeye analipwa Tsh 300 kwa kilo tofauti ya Tsh 14 tu ya mkulima wa chai hivyo unakuta huyu mkulima gharama za uzalishaji shambani kuwa kubwa na kumeza faida ya mkulima na kipato chake kuwa chini sana, hali hii inapelekea baadhi ya wakulima kutelekeza mashamba yao na kujihusisha na shughuli nyingine kama kusomba mbao ” alisema Mhe. Mhongole.

Akisoma risala Katibu wa Chama cha Ushirika Bwana Venusto France aliongeza kwamba Changamoto nyingine ni mkulima kutoshiriki katika mnyororo wa thamani katika zao la chai kwa kuishia kuuza majani mabichi pekee na bei kubwa ya pembejeo inayopatikana bila ruzuku ya serikali.

Akijibu changamoto ya bei Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya chai Tanzania Bwana Theophord Ndunguru alikiri changamoto hiyo na kusema kwamba tatizo hilo linatokana na mnada wa soko kuwa Mombasa Kenya hivyo wao kujipendelea lakini pia ubora  wa chai hivyo serikali tayari inamkakati wa kuanzisha mnada wake Jijini Dar es salaam ili kusaidia bei kupanda.

Kilimo cha chai Mkonge kilianzishwa mwaka 1971 chini ya mamlaka ya chai Tanzania (MACHATA) au TTA wakulima waanzilishi walikuwa 174 ambao walimiliki hekta 118.Chama kilianzishwa mwaka 1989 kama kikundi cha wakulima baada ya Mamlaka ya chai Tanzania (TTA) Kusitishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa chama hiki lilikuwa ni kuwaunganisha wakulima wa chai Mkonge Katika kilimo cha zao la chai na kuwa na sauti moja katika kudai haki kutatua changamoto pamoja na kutafuta fursa.


HABARI PICHA
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akieleza lengo la ziara yake katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya Mufindi

Naibu waziri wa Kimlimo Mhe Mgumba katikati, kulia kwake ni  Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi Ndugu Yassin na kushoto kwa waziri ni Mkuu wa Wilaya Mufindi he Jamhuri William.


Chai inayolimwa Mufindi


Wataalamu mbalimbali na Wananchi wa kijiji cha Mkonge Wilayani Mufindi wakimsijiliza kwa makini Mhe Naibu Waziri wa Kilimo

Mkuu wa Wilaya Mufindi  Mhe William akitoa utambulisho kwa wananchi na wanachama wa ushirika wa wakulima wa chai mkonge kutokana na ugeni wa Naibu waziri wa Kilimo ,he Mgumba 


Mwenyekiti wa Ushirika wa Wakulima wa Chai Mkonge Bwana Sentino Mdena akiukaribisha ugeni wa Naibu waziri wa Kilimo.


Katibu wa Ushirika wa Wakulima wa Chai Mkonge bwana Venusto France akisoma taarifa ya ushirika kwa Naibu Waziri wa Kilimo


Naibu Waziri wa Kilimo akiongea na Wananchi na Wakulima wa Chai Katika Kijiji cha Mkonge Kata ya Luhanga Tarafa ya Ifwagi Wlayani Mufindi Mkoani Iringa.


Wananchi na Wakulima wa Chai wakiendelea kumsikiliza Mhe Mgumba Naibu Waziri wa Kilimo.
Picha Zote na Amani Mbwaga
Kwa Maoni au Ushauri Wasiliana nasi:
Mob: +255 656 632 566
E-mail:prof.mbwaga@gmail.com



No comments:

Post a Comment