Tuesday, August 14, 2018

RC Mpya Iringa Mhe Ally Hapi Ametoa Siku 90 Wazee Wote Kupewa Vitambulisho vya Kutibiwa Bure!


Mkuu Mpya wa Mkoa wa Iringa Mh Ally Salum Hapi akiongea na Watumishi wa Wilaya ya Mufindi wakati wa ziara yake ya kujitambulisha Mapema wiki hii (Picha na Amani Mbwaga)

Na Amani Mbwaga, Mafinga-Iringa
Mkuu Mpya wa Mkoa Iringa Mhe Ally Salum Hapi ametoa Siku 90 toka tarehe 11 Agosti 2018 Kuhakikisha wazee wote wa mkoa wa Iringa waliotambuliwa   wanapewa vitambulisho vya kutibiwa bure.

Ameyasema hayo leo wakati akiongea na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi na Mji Mafinga zilizoko Mkoani Iringa wakati wa ziara yake ya kwanza Wilayani Mufindi kwa ajili ya kujitambulisha.

“Na Kwenye hili nimesema wazee wasiwafuate Halmashauri kwenda kupewa hivyo vitambulisho bali Halmashauri Kupitia DMO na timu yake mtoke muwafuate wananchi kata kwa kata muwaandikishe, Muwasajili na kisha muwapelekee vitambulisho mahali walipo”.

Aidha amewataka watumishi kutofanya kazi kwa mazoea bali watimize wajibu wao kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria na pia waongeze ubunifu katika kazi zao ili kuleta matokeo chanya na kusisitiza kwamba kazi yao ni moja tu kuhakikisha wanamsaidia Rais.

Awamu ya tano inazungumzia hapa kazi tu ni lazima watendaji watoke ofsini na kwenda kuwahudumia wananchi ili kutatua shida zao, kutenda haki na kuwa waadilifu.

“Pia ni lazima tuongeze juhudi za kukusanya mapato ya serikali kwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili Halmashauri zetu zote za Mkoa wa Iringa zisishuke asilimia 90%”alisema Mhe Hapi.

Hata hivyo mhe Hapi ametangaza kuanza kwa kampeni ya Iringa Mpya ambapo atazunguka tarafa zote ndani ya siku 18 na kufanya mikutano isiyopungua 03 kwa ajili ya kusikiiza kero za wananchi.

Akisoma taarifa ya wilaya, Mkuu wa wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William amesema anaishukuru serikali ya awamu ya tano inayo ongozwa na Rais Dkt John Pombe Magufuli kwa kuendelea kupeleka fedha za Maendeleo na matumizi ya kawaida katika Wilaya yake.

Mwaka 2017/2018 Wilaya ya Mufindi ilipokea fedha kutoka serikali kuu kiasi cha Tsh Bilioni 6 na Milioni 200 kwa ajili ya maendeleo na matumizi ya kawaida.

Vilevile Halmashauri zote za Wilaya Mufindi zilikuwa zikitimiza wajibu wake wa kukusanya mapato Mfano Halmashauri ya Wilaya Mufindi mwaka 2017/2018 wamekusanya mapato asilimia 90.9%, walikuwa na lengo la kukusaya Tsh Bilioni 3.8 na wamekusanya Tsh Bilioni 3.5 sawa na asilimia 90.9%

Halmashauri ya mji wa Mafinga mwaka 2017/2018 wamekusanya Tsh Bilioni 2.6 kati ya lengo la kukusanya Bilioni 2.7 sawa na asilimia 84%

“Mbali na hivyo umetuelekeza pia tuandike andiko maalumu kwa ajili ya mradi mwingine wa kimkakati wa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mafinga mjini hadi Mgololo kilomita 80. tunaenda kutekeleza kwani barabara hiyo inapita kwenye viwanda vingi ndani ya Wilaya yetu na itaamsha uchumi wa maeneo mengi sana katika wilaya yetu” alisema Mhe Wiliam.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mhe Festo Mgina lisema kwenye hotuba ya mkuu wa Mkoa imesheheni mambo muhimu yote yatakayosaidia utekelezaji katika utendaji wa kila siku.
“Ninaamini tukitembea katika hotuba yako Mhe Mkuu wa Mkoa tutakuwa na Mkoa uliofanywa upya na Mufindi yetu Mpya” alisema Mh Mgina.

Akitoa Shukrani Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga            Mhe Charles Makoga alisema “yote uliyoyasema kwetu sisi ni maagizo tunakuahidi tunakwenda kutekeleza na ninaomba watumishi sasa tukaanze vizuri kuanzia leo”.

Tarehe 28 Julai Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alimteua Mhe Ally Salum Hapi Kuwa Mkuu wa Mkoa Iringa na kuchukua nafasi ya Mhe Amina Juma Masenza aliyestaafu kwa mujibu wa sheria, awali Mhe Mkuu wa Mkoa Hapi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es alaam.


                                     HABARI KATIKA PICHA


Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Ally Salum Hapi  akipokelewa na  Mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William alipowasili Wialayani hapo kwa ajiliZiara yake ya Kwanza ya Kujitambulisha


Mkuu wa Mkoa Iringa Mh Ally Salum Hapi akiongea na Watumishi wa Wilaya ya Mufindi (hawapo pichani) .
Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi na Mji Mafinga wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa Iringa Ally Hapi (Hayupo Pichani) 
Mkuu wa Mkoa Iringa akiongea na Watumishi wa Halmashauri ya WilayaMufindi

Kaimu Chifu wa Wahehe akiongea na watumishi wa Wilaya ya Mufindi ikiwa ni Moja ya Ukaribisho wa RC Mpya Mufindi
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mhe Festo Mgina akitoa salamu za Shukrani kwa ujio wa Mkuu wa Mkoa


Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Ally Hapi Katikati akiwa katika Picha Ya Pamoja na Machifu wa Iringa Kulia Kwake ni Mkuu wa Wilaya Mufindi na Kushoto kwake ni Mbunge wa Viti Maalumu CCM Mkoa wa Iringa Rose Tweve na Nyuma Kushoto ni RPC -Iringa Kamanda Juma Bwire
RC-Iringa waliokaa  (katikati) akiwa katika Picha Ya Pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Mufindi
Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Hapi akiongea na Wafanyabiashara wa Stendi ya Mji wa Mafinga alipita kuwasalimia mara baada ya kumaliza ziara yake ya Kujitambulisha Wilayani Mufindi (Picha zote na Amani Mbwaga) 







                             Picha Zote na Amani Mbwaga 

Mob:0656 632 566
Email:prof.mbwaga @gmail.com

No comments:

Post a Comment