Wednesday, August 29, 2018

Halmashauri ya Wilaya Mufindi yavuka lengo Ukusanyaji wa mapato na kufikia asilimia 90.96


Na Amani Mbwaga Mafinga.
Halmashauri ya Wilaya Mufindi Imevuka lengo la Ukusanyaji Mapato yatokanayo na vyanzo vya ndani katika mwaka wa fedha 2017/2018, na kufikia silimia 90.96.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mhe Festo Mgina wakati wa kutano wa Baraza la Madiwani la robo ya nne lililofanyika leo katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mkoani Iringa.

Ilielezwa kuwa katika kipindi cha Julai 2017 hadi Juni 2018 Halmashauri ilikusanya na kupokea jumla ya Tsh Bilioni 35.3 kati ya mapato hayo Tsh Bilioni 3.5 ni mapato yaliyotokana na vyanzo vya ndani, Tsh Bilioni 24.6 ni mishahara, Tsh bilioni 5 ni miradi ya maendeleo na Tsh Bilioni 2 ni matumizi ya kawaida.

Aidha katika kipindi cha Julai 2017 hadi Juni 2018 mchango wa wananchi katika kutekeleza miradi ya maendeleo ulikuwa na thamani ya Tsh Milioni 793.5.

Mlinganisho wa mapato halisi ya Tsh Bilioni 35.3 kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Juni 2018 na makisio ya Tsh Bilioni 51.13 ya mwaka 2017/2018 unaonesha kuwa Halmashauri imekusanya asilimia 68.4 ya lengo la mwaka wa fedha wa 2017/2018.

Aidha mlinganisho wa mapato yatokanayo na vyanzo vya ndani yaliyokusanywa kwa kipindi cha Julai 2017 hadi Juni 2018 ya Tsh  Bilioni 3.5 na makisio ya mapato yanayotokana na vyanzo vya ndani ya Bilioni Tsh 3.8 kwa kipindi hicho yanaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya Mufindi imekusanya asilimia 90.96 ya lengo la mwaka.

“Mimi nawapongeza sana Mkurugenzi na timu yako kwa kufikia mafanikio Makubwa ya ukusanyaji mapato katika Halmasahuri yetu, niwasihi muendelee kufanya vizuri zaidi katika ukusanyaji lakini pia ni lazima tuongeze kasi na kuwa wabunifu wa kuwapata watu wakorofi wanaokwepa kulipa ushuru na kodi mbalimbali za serikali” alisema Mhe Mgina.

Aidha amewaasa Waheshimiwa Madiwani kushirikiana na kuendelea kujenga Mahusiano mazuri zaidi na Ofisi ya Mkurugenzi na wataalamu wake ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Mufindi na Taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William aliwashukuru waheshimiwa madiwani kwa kuasidia utekelezaji wa majukumu ya serikali na hasa katika uhamasishaji wa kampeni ya ujenzi wa vyoo bora kwa wanachi.

Mhe Mwenyekiti tumezindua kampeni ya ujenzi wa vyoo bora kwenye wilaya yetu na haya ni maelekezo ya serikali, na sisi mufindi katika utekelezaji wa hilo tumejipa hadi tarehe 30 Oktoba 2018, tuhakikishe kila kaya inakuwa na choo bora. Alisema Mhe William.

Tafsiri ya choo bora tayari imekwishatolewa na wananchi wanaelewa, waheshimiwa madiwani wote wameombwa kuzungumza lugha moja, ili kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na vyoo bora.

Utekelezaji wa kampeni hiyo unaambatana na usimamizi wa sheria ya mazingira.

Takribani asilimia 20% ya kaya ndio zenye vyoo bora Wilaya ya mufindi na asilimia 80% ni vyoo ambavyo si bora, kaya nyingi zinatumia vyoo vya asili sasa ni wakati wa kuhakikisha jamii inakuwa na vyoo bora.

Nae Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Isaya Mbenje amewakumbusha waheshimiwa madiwani kuhusu kulinda mali za asili na mazingira kwa ujumla kutokana Msimu wa kulimo unaokuja hivi karibuni ambapo watu wakati wa kuandaa mashamba huchoma moto hovyo unaoathiri mazingira na maliasili zilizopo.


“Katika Wilaya yetu tunatarajia msimu wa kilimo na tunaanza maandalizi ya mashamba kwa ajili ya kilimo hivyo tunaenda kuwa na kampeni ya kuhakikisha wananchi wanapoenda kusafisha mashamba yao wasichome na maeneo mengine” alisema Bwana Mbenje.

HABARI PICHA















No comments:

Post a Comment