Na Amani
Mbwaga, Mafinga.
Baraza la Madiwani
Halmashauri ya Mji Mafinga limedhamiria kununua gari ya taka katika mwaka huu
wa fedha ili kuongeza kasi ya ukusanyaji taka katika mji wa Mafinga na kuhakikisha
mji unakuwa safi wakati wote.
Hayo yamesemwa na
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Mhe Charles Makoga katika Mkutano wa
baraza la Madiwani wa Robo ya nne 2017/18 uliofanyika leo katika Ukumbi wa
Halmashauri mjini Mafinga, Mkoani Iringa.
“Tumenunua trekta
jipya pia tuna gari nyingine kwa ajili ya kubeba taka lakini mwaka huu
tunanunua gari nyingine ya taka kuhakikisha kwamba tunakuwa na magari ya kutosha
kubebea taka katika mji wetu ili uwe safi zaidi na tutasimamia hapo”
alisema Mhe Makoga.
Baraza limeagiza pia
kila duka, taasisi za serikali na zile za binafsi kuhakikisha zinakuwa na vyombo
vya kutunzia taka.
Agizo la Mkuu wa Wilaya
Mufindi Mhe Jamhuri David William linawataka Wananchi wote kila Jumamosi ya
Mwisho wa Mwezi kufanya usafi wa kina katika maeneo yote yanayowazunguka.
“Usafi ni jukumu la
sisi wote hata Waheshimiwa Madiwani tunatakiwa kwenda kufanya usafi, basi kesho
ni siku ya usafi tuungane wote kwenda kushiriki kufanya usafi katika Mji wetu
wa Mafinga” alisema Mhe Makoga.
Kwa upande wake
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ambae pia
ni Afisa Tarafa wa Tarafa ya Malangali Ndugu Daniel Dugange akitoa salamu za
Mkuu wa wilaya amewataka watendaji kuja na mikakati bora zaidi ili kuboresha
huduma bora kwa wananchi.
Amehimiza kudumisha
ushirikiano zaidi katika kutatua changamoto mbalimbali ikiwemo migogoro ambayo
viongozi wa ngazi ya kijiji, Kata na Tarafa imeshindikana ili kuwahudumia
wananchi kwa ukaribu.
“Tukumbuke kwamba
katika kutekeleza ilani ya CCM ya mwaka 2015 tumeshatafuna miezi 32 bado miezi
28 tu tumalize kipindi cha miaka 05, kwa hiyo tujipange vizuri tuwe na mpango
mkakati mpango ambao unaangalia mambo 04, uwezo tulionao, udhaifu, fursa
zilizopo na matatizo yaliyopo” Alisema Bwana Dugange.
Rasilimali ni chache
lakini ni lazima kujipanga kwa uchache wa rasilimali zilizopo ili kuweza
kufikia malengo na dira ya Taifa ya 2025.
Aidha Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Bwana Voster Mgina
amelieleza baraza la madiwani kuhusu ushirikiano ulioanza kufanywa baina ya
shule za serikali na zile za binafsi ili kuongeza ufaulu katika Halmashauri ya
mji Mafinga ukizingatia shule nyingi za binafsi katika mji huu zinafanya vizuri
katika matokeo ya mitihani ya Taifa zaidi ya shule za serikali.
“Sasa hivi
Waheshimiwa Madiwani tuna mitihani yetu ya Muhula ambapo tunatarajia kuwa na
mtihani mmoja kwa shule zote za serikali na zile za binafsi hata hivi leo
ninavyozungumza waalimu wetu wa shule zote wako shule ya Sekondari Bethel
wakipitia mitahani ambayo itafanyika mwezi wa Novemba 2018 ni mtihani mmoja
unatungwa na Waalimu wana upitia pale kuhakikisha unakuwa vizuri”
alisema Bwana Mgina.
Aliongeza pia
kumekuwa na mafunzo ya pamoja kwa waalimu wa shule zote za binafsi na serikali
ambayo hufanyika mara kwa mara, na jana tu Baadhi ya waalimu wa Sayansi
walikuwa wakipewa mafunzo ya vitendo katika sule ya Sekondari JJ Mungai kutoka
kwa wakufunzi wa Chuo cha Kleruu ili kuwafundisha waalimu namna nzuri ya
kuandaa masomo ya sayansi kwa vitendo.
Mkutano huu wa Baraza la Madiwani wa robo ya nne 2017/2018 umefanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni za kudumu, na taratibu za uendeshaji wa serikali za mitaa.
HABARI PICHA
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya Mufindi, Afisa Tarafa ya Malangali Bwana Daniel Dugange akitoa salamu za Mkuu wa Wilaya katika Mkutano wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Mafinga. |
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Voster Mgina akitolea ufafanuzi jambo wakati wa Mkutano wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Mafinga |
Diwani wa Kata ya Boma Mhe Julist Kisoma akiuliza swali katika Mkutano wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Mafinga |
Diwani Mhe Chesco Lyuvale akichangia katika moja ya agenda iliyokuwa inaendelea katika Mkutano wa Baraza la Madiwani |
Diwani Mhe Denis Kutemile akiuliza swali wakati wa maswali ya papo kwa papo kwa Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Mafinga |
Waheshimiwa Madiwani wakifuatilia kwa makini Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Kwanza Kushoto ni Diwani wa kata ya Boma Mhe Damian Kyando naNyuma ni Wataalamu kutoka Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Mafinga. |
Picha zote na Amani Mbwaga Kwa Maoni au Ushauri Wasiliana nasi, Mob:+255 656 632 566 E-mail:prof.mbwaga@gmail.com |
No comments:
Post a Comment