Na Amani Mbwaga, Mufindi-Iringa
Naibu waziri wa Kilimo Mhe Omari Mgumba amekipongeza chama
cha ushirika cha wakulima wa chai Mkonge baada ya kupata tuzo ya kuwa chama
bora cha ushirika ngazi ya mkoa mwaka 2017 na mwaka huu 2018 kilipata tuzo ya
mshindi ngazi ya taifa katika tasnia ya chai katika vyama vya msingi Tanzania.
Pongezi hizo zimetolewa na Naibu waziri wa kilimo alipokuwa
katika ziara yake ya kikazi katika Kijiji cha Mkonge kata ya Luhanga Tarafa ya
Ifwagi wilaya Mufindi Mkoani Iringa kwa lengo la kujionea shughuli za kilimo
cha chai jinsi zinavyofanyika katika Wilaya ya Mufindi hususani kukutana na
Wakulima kujua wanafursa gani changamoto, zipi na mikakati gani wanayo ili
kusonga mbele katika kilimo chao.
Chama hiki kimesajiliwa kwa sheria ya nchi ya vyama vya
ushirika mnamo tarehe 29 Aprili 2018 na kupewa hati Na IR 417, pia kimefanikiwa
kutoa washindi wa ukulima bora kitaifa wa zao la chai, kikanda na kitaifa kwa
miaka mitano mfululizo kuanzia mwaka 2008-2012.
“Niwapongeze sana kwa ushindi mkubwa wa mkoa kanda na
kitaifa kwa kuwa chama bora cha msingi wa mazao na masoko Tanzania na mlipokuwa
mnapewa nafasi hii na kuchukukua kombe nilikuwepo pale Mwanza kweli mnastahili
na mwanzo nilikuwa sijawafahamu vizuri lakini kwa namna tu maonesho yenu
yalivyokuwa yanaendelea kila mtu aliona kwamba mnastahili kupata ngao hizi” alisema Mhe Mgumba.
Mhe. Mgumba
aliendelea kusema kuwa wanawatia moyo na pia wanawatoa kimasomaso kama serikali
na Wizara ya kilimo ambayo ushirika uko chini yao ambapo wengine hubeza uwepo
wa ushirika lakini chama cha ushirika Mkonge wameonesha kwa vitendo.
Mafanikio ya Chama cha ushirika wa wakulima wa Chai Mkonge
ni mengi sana lakini baadhi ni ongezeko la wanachama kutoka 174 mwaka 1971 hadi
kufikia wanchama 652 waliopo sasa, Upanuzi wa Mashamba ya chai kutoka hekta 118
za mwaka 1971 kufikia hekta 344 zilizopo sasa, Uzalishaji wa majani mabichi ya
chai umeongezeka kutoka kilo takribani laki 856,829 za mwaka 1971 na kufikia
wastani wa kilo milioni 2 na zaidi za majani mabichi kwa mwaka.
Mchango wa taasisi na mashirika mbalimbali katika kuendeleza
zao la chai katika ushirikwa wa Mkonge hawakuwa nyuma, ambapo Mkonge Tea Block
Farm ilipata mkopo toka kwa wahisani wenye mashariti nafuu kutoka kwa shirika
la Marekani African Development Foundation (ADF) kupitia shirika la CSDI
Tanzania na kutoa mkopo wa Tsh. Milioni 271.9 kwa ajili ya kuimarisha na
kuendeleza zao la chai katika Ushirika wa wakulima wa chai Mkonge Wilayani
Mufindi.
Halmashauri ya Wilaya Mufindi kupitia DAPS ilisaidia
kukamilisha miradi minne ambayo iliibuliwa na wanachama wenyewe ikiwemo
ukarabati wa barabara ziendazo mashambani kilomita 6 yeye thamani ya Tsh
Milioni 80, ujenzi wa mabanda10 kwenye vituo vya kupimia chai vyenye thamani ya
Tsh milioni 22, ununuzi wa Powertiler 2 zenye thamani yaTsh Milioni 16 na mradi
wa ufugaji kuku Tsh milioni 2.
Wakala wa maendeleo ya wakulima wadogo wa chai Tanzania (TASHTDA)
ni miongoni mwa taasisi zilizochangia maendeleo ya chai Mkonge, wao walichangi
fedha kiasi cha Tsh milioni 1 na mafuta Dizeli lita 100 kusaidia ujenzi wa
ofisi.
Aidha bodi ya chai Tanzania (TBT) nao wapo bega kwa bega
katika kutetea haki katika tasnia ya chai katika mikataba na matatizo
yanapotokea kati ya ushirika na wanunuzi wa chai basi huingilia kati pia
wamejenga banda moja la mfano kwa ajili ya kupimia chai.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William
alisema serikali imejitahidi kutafuta wafadhili na wadau mbalimbali ambapo
tayari kuna uhakika wa kupata km 40 kutoka sawala hadi Lulanda ikiwa ni moja ya
kupunguza changamoto ya miundombinu ya barabara.
Nae Diwani wa kata ya Luhanga Mhe Abeid Mhongole akitoa
salamu zake kwa Naibu Waziri wa kilimo alisema wakulima wa chai katika eneo
lake wamekuwa na changamoto nyingi ikiwemo bei ya mauzo ya majani mabichi ya
chai kuwa ndogo, ingawa bei ya mauzo ya majani mabichi viwandani iliongezeka
mwaka 2017 kutoka 250 kwa kilo hadi 287.11 pia mwaka 2018 kutoka 287.11 hadi
314.11 kwa kilo.
“Mheshimiwa Naibu Waziri bei ya kilo moja ya chai kwa sasa ni Tsh 314 lakini yeye huyu mkulima ni mmiliki wa shamba, analima kwa nguvu zake mwenyewe anagharamia mbolea pamoja na madawa lakini ukilinganisha na wenzetu wenye makampuni mfano UNLIVER mfanyakazi wa chai yeye analipwa Tsh 300 kwa kilo tofauti ya Tsh 14 tu ya mkulima wa chai hivyo unakuta huyu mkulima gharama za uzalishaji shambani kuwa kubwa na kumeza faida ya mkulima na kipato chake kuwa chini sana, hali hii inapelekea baadhi ya wakulima kutelekeza mashamba yao na kujihusisha na shughuli nyingine kama kusomba mbao ” alisema Mhe. Mhongole.
Akisoma risala Katibu wa Chama cha Ushirika Bwana Venusto France aliongeza kwamba Changamoto nyingine ni mkulima kutoshiriki katika mnyororo wa thamani katika zao la chai kwa kuishia kuuza majani mabichi pekee na bei kubwa ya pembejeo inayopatikana bila ruzuku ya serikali.
Akijibu changamoto ya bei Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya chai Tanzania Bwana Theophord Ndunguru alikiri changamoto hiyo na kusema kwamba tatizo hilo linatokana na mnada wa soko kuwa Mombasa Kenya hivyo wao kujipendelea lakini pia ubora wa chai hivyo serikali tayari inamkakati wa kuanzisha mnada wake Jijini Dar es salaam ili kusaidia bei kupanda.
Kilimo cha chai Mkonge kilianzishwa mwaka 1971 chini ya mamlaka ya chai Tanzania (MACHATA) au TTA wakulima waanzilishi walikuwa 174 ambao walimiliki hekta 118.Chama kilianzishwa mwaka 1989 kama kikundi cha wakulima baada ya Mamlaka ya chai Tanzania (TTA) Kusitishwa.
Lengo la kuanzishwa kwa chama hiki lilikuwa ni kuwaunganisha wakulima wa chai Mkonge Katika kilimo cha zao la chai na kuwa na sauti moja katika kudai haki kutatua changamoto pamoja na kutafuta fursa.
Lengo la kuanzishwa kwa chama hiki lilikuwa ni kuwaunganisha wakulima wa chai Mkonge Katika kilimo cha zao la chai na kuwa na sauti moja katika kudai haki kutatua changamoto pamoja na kutafuta fursa.
HABARI PICHA
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akieleza lengo la ziara yake katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya Mufindi |
Naibu waziri wa Kimlimo Mhe Mgumba katikati, kulia kwake ni Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi Ndugu Yassin na kushoto kwa waziri ni Mkuu wa Wilaya Mufindi he Jamhuri William. |
Chai inayolimwa Mufindi |
Wataalamu mbalimbali na Wananchi wa kijiji cha Mkonge Wilayani Mufindi wakimsijiliza kwa makini Mhe Naibu Waziri wa Kilimo |
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe William akitoa utambulisho kwa wananchi na wanachama wa ushirika wa wakulima wa chai mkonge kutokana na ugeni wa Naibu waziri wa Kilimo ,he Mgumba |
Mwenyekiti wa Ushirika wa Wakulima wa Chai Mkonge Bwana Sentino Mdena akiukaribisha ugeni wa Naibu waziri wa Kilimo. |
Katibu wa Ushirika wa Wakulima wa Chai Mkonge bwana Venusto France akisoma taarifa ya ushirika kwa Naibu Waziri wa Kilimo |
Naibu Waziri wa Kilimo akiongea na Wananchi na Wakulima wa Chai Katika Kijiji cha Mkonge Kata ya Luhanga Tarafa ya Ifwagi Wlayani Mufindi Mkoani Iringa. |
Wananchi na Wakulima wa Chai wakiendelea kumsikiliza Mhe Mgumba Naibu Waziri wa Kilimo. Picha Zote na Amani Mbwaga Kwa Maoni au Ushauri Wasiliana nasi: Mob: +255 656 632 566 E-mail:prof.mbwaga@gmail.com |