Wednesday, October 3, 2018

Shamba la Miti Sao Hill lachangia zaidi ya Bilioni 47 pato la Taifa.


Na Amani Mbwaga, Mafinga

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William alipokuwa akizindua rasmi kampeni ya kuzuia moto Mufindi yenye kauli mbiu “Moto jamii chukua tahadhari” Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.
Kampeni ya kuzuia moto HATARISHI Mufindi imezinduliwa rasmi kwa kufanya kikao cha kimkakati na watendaji wa kata,vijiji,mitaa na Maafisa Tarafa wote wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi  na Halmashauri ya Mji wa Mafinga na baadae kufanya ziara katika vijiji vya Kitilu, Kihanga, Sao Hill, Mtula na Matanana ambapo alieleza umuhimu wa tasnia ya misitu katika uchumi wa Wilaya ya Mufindi na Tanzania kwa ujumla.Shamba la Miti Saohill ndilo linalobebe sehemu kubwa ya mchango huu.
  “Mwaka jana Shamba la Miti Sao Hill lilikusanya maduhuli ya zaidi ya Tsh Bilioni 47  kwenye mfuko mkuu wa hazina na ndio maana Halmashauri zetu za Mufindi na Mkoa wetu wa Iringa zinashika nafasi za juu sana katika kuchangia pato la taifa” alisema Mhe William.
Mhe William alibainisha kwamba mwaka huu kampeni ya kuzuia moto hatarishi itafanyika kwa utofauti kidogo, mwaka jana jumla ya hekta 129 zilizoungua katika shamba la miti Sao Hill lakini sasa hivi kwa kipindi cha siku nne tu takribani hekta 400 zimeteketea kwa moto hali hii inatisha na hapa bado mashamba hayajaanza kusafishwa hivyo ni lazima tujipange kudhibiti matukio yasitokee tena.
Kutokana na hali mbaya ya hewa upepo mkali katika wilaya ya Mufindi Mhe William amesitisha zoezi  la usafishaji wa mashamba kwa muda wa siku 7 kuanzia tarehe 30 Septemba 2018 hadi tarehe 07 Oktoba 2018 ili kupisha athari kubwa inayoweza kutokea kutokana na moto ukiwashwa kipindi hiki sio rahisi kuuzima na unaweza kuteketeza zaidi mashamba ya miti na hatimae kudumaza uchumi wa Taifa kupitia sekta hii.
“Msitu huu ni mali yetu ni lazima tuwe na uchungu nao na sote tuulinde kwa hali na mali  na kila mmoja wetu atimize wajibu wake kwa kufuata  sheria taratibu na kanuni zinazotuongoza ili kunusuru hali hiyo ya kupoteza utajiri wetu isiendelee alisisitiza” Mhe William.
Kwa upande wake Afisa Uenezi na Ugani wa Shamba la Miti Sao Hill Bwana Joseph Sondi ameiomba jamii kutoa ushirikiano na taarifa pale wanapoona dalili za moto hatarishi sehemu yoyote ile ili hatua madhubuti za kuzuia moto  zifanyike kwa kushirikiana na Kikosi cha Uzimaji moto ambacho kipo tayari muda wote katikaShamba la Miti Sao Hill kwa ajili ya matukio kama hayo.
Pia amesisitiza sheria ndogo za udhibiti moto hatarishi zilizopo katika vijiji na mitaa zifuatwe.Kabla mtu hajawasha moto katika kusafisha mashamba ni lazima apate kibali na awe na watu wa kutosha wa kumsaidia ili moto ukitokea kumshinda basi wale watu wasaiide kuzima kabla haujasambaa sehemu kubwa na kuathtiri sehemu nyingine.
Nae Kamanda wa Zimamoto Wilaya ya Mufindi Mkaguzi Msaidizi (A/ Inspector) Jackline Mtei ameiasa jamii kuwa makini na matumizi mabaya ya moto kwani yanaweza kupelekea umaskini na hata kifo aidha amesisitiza kwamba kila kiongozi na kila mwananchi anawajibu wa kudhibiti moto usitokee na kama ukitokea ni lazima wote kushirikiana kwa kuuzima ili usiendelee kuleta athari nyingine.
Wananchi mbalimbali na viongozi wa vijiji nao wametoa maoni yao wakiomba kamati za kuzuia moto kwa kila kijiji kuongezewa mafunzo ya jinsi ya kupambana na majanga ya moto pale yanapotokea sanjari na kugawiwa vifaa vya kuzimia moto kwa kila kijiji. 
Kampeni hii inaendelea chini ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mufindi na kuratibiwa na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Shamba la Miti Sao Hill lililopo katika Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa ambapo vijiji 60 vitafikiwa kwa awamu mbili,  mpaka sasa ni siku ya pili tayari vijiji 5 vimefikiwa.

Uwekezaji katika Shamba la miti Sao Hill umelenga katika upandaji mkubwa wa miti ili kuhakikisha upatikanaji endelevu wa malighafi ya mazao ya misitu kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

                        HABARI PICHA
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William
Afisa Uenezi na Ugani wa Shamba la Miti Sao Hill Bwana Joseph Sondi akitoa elimu ya Moto Hatarishi katika moja ya vijiji Wilayani Mufindi.
Kamanda wa Zimamoto Wilaya ya Mufindi Mkaguzi Msaidizi (A/ Inspector) Jackline Mtei akitoa elimu ya jinsi ya kujikinga na Majanga ya Moto



Afisa Uenezi na Ugani wa Shamba la Miti Sao Hill Bwana Joseph Sondi akitoa elimu ya Moto Hatarishi kwa Watendaji na Maafisa Tarafa Wilayani Mufindi (Hawapo Pichani)

































Diwani wa Kata ya Sao Hill Mhe Denis Kutemile akikaribisha ugeni ulifika katika vijiji vyake ili kutoa elimu ya moto hatarishi na athari zake kwa jamii




Baadhi ya Wananchi wa Kijiji cha Mtula wakisikiliza kwa maki ni elimu inayotolewa










No comments:

Post a Comment