Monday, October 1, 2018

Mtendaji Mkuu wa (TFS) Professa Silayo akagua Maeneo yaliyoungua moto katika Shamba la Miti Sao Hill.



Na Amani Mbwaga, Mafinga
Baadhi ya Eneo la Shamba la Miti Sao Hill lililoungua.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Professa Dos Santos Silayo ametembelea Shamba la Miti Saohill ili kukagua maeneo ambayo yaliungua moto kwa siku nne mfululizo kuanzia tarehe 25 hadi 28 septemba, 2018 na kuteketeza karibia hekta 400 za  miti katika Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.

“Nawapongeza watumishi wote kwa kushirikiana katika kipindi hiki ambacho kimekuwa na matukio mengi ya moto hivyo nawataka watumishi kuendelea kushirikiana na kila mmoja atimize wajibu wake katika nafasi aliyonayo” alisema Bwana Silayo.

Mnamo tarehe 26 Septemba 2018 majira ya saa nane mchana moto ulizuka tena katika eneo la sao hill safu ya pili, jitihada za kuuzima zilifanyika na kufanikiwa kuuzima sanjari na uwepo wa upepo mkali, jumla ya viunga (Compartments) 11 ziliungua zenye ukubwa wa hekta 347.314.

Aidha Kijiko (Grader) kimoja ambacho kilitumika katika kutengeneza barabara ya kuzuia moto usiruke katika jitihada za kukabiliana na moto huo kilipata hitilafu ya kiufundi na kushindwa kutembea na hivyo kupitiwa na moto lakini yameungua tu matairi na baadhi ya paipu tu za kijiko.

Tarehe 27 Septemba 2018 moto tena ulitokea majira ya saa tatu usiku katika safu ya matanana na kuunguza takribani hekta 5.9.

Hata hivyo tarehe 28 Septemba moto mwingine ulitokea katika safu ya Ngwazi kutokana na shughuli za usafi katika maeneo ya makazi ya watumisha wa Taasisi ya utafiti wa chai na kupelekea kuunguza jumla ya hekta 28 yenye miti ya kupandwa.

Bwana Silayo ameendelea kusisitiza kusisitiza kuhusu utatuzi wa migogoro iliyopo kati ya vijiji vinavyopakana na Shamba la Miti Saohill kwani hadi sasa inakadiriwa jumla ya hekta 21,000 zimevamiwa.
Amewataka zoezi hili la utatuzi wa migogoro lifanyike mapema ili shamba liendelee kuwa katika hali ya usalama.

Akisoma taarifa ya shamba mbele ya Mtendaji Mkuu, Meneja wa Shamba Bw. Heriberth Haule amemueleza Mtendaji Mkuu kuhusu chanzo cha moto.

“Ukiondoa tukio la moto ulioanzia kwenye makazi ya watumishi wa Taasisi ya Utafiti wa chai kule Ngwazi mpaka sasa chanzo kamili cha moto katika matukio mengine manne hakijafahamika”alisema Bwana Haule
Ameeleza kuwa zoezi la uzimaji moto lilikuwa gumu kutokana na upepo mkali uliokuwepo na hivyo kupelekea sehemu kubwa ya shamba kuungua moto.

Bwana Haule aliendelea kusema kuwa uhaba wa watumishi na mitambo pia imekuwa ni changamoto kubwa ambayo inasababisha kupunguza kasi ya utendaji wa kazi ndani ya shamba hasa katika kipindi hiki cha kiangazi ambapo matukio mengi ya moto yamekuwa yakijitokeza.

Shamba la miti Sao Hill linaukubwa wa hekta 135,903 ambazo zimehifadhiwa kwa ajili ya upandaji miti na hifadhi ya mazingira kati ya eneo hilo kiasi cha hekta 86,003 ni kwa ajili ya upandaji miti kibiashara, hekta  48,200 kwa ajili ya utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji na hekta 1,700 ni kwa ajili ya makazi na uwekezaji.

HABARI PICHA

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa  Misitu Tanzania( TFS) Bwana Silayo wa Tatu Kushoto akipokea maelezo ya chanzo cha moto Kilipoanzia kutoka kwa Meneja wa Shamba la Sao Hill Bwana Haule





Picha zote na Amani Mbwaga



No comments:

Post a Comment