Sunday, January 13, 2019

UFAULU ELIMU MSINGI WAENDELEA KUSTAWI MUFINDI


Takwimu za ufaulu wa mitiahani ya kuhitimu elimu ya Msingi kwa Shule za Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, zinaonesha kuendelea kupanda kwa kipindi cha miaka minne mfululizo kati ya mwaka 2015 - 2018 huku Halmashhauri ikiendelea kushika nafasi za kuridhisha Katika ushindani wa Kitaifa.

Hayo yamebainishwa na Ofisa mwenye dhamana ya taaluma wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bi. Mariamu Ngalla, wakati akiwasilisha taarifa ya tathimini ya Mtihani wa kuhitimu Elimu ya Msingi kwa mwaka 2018 katika kikao maalum cha kila mwaka ambacho hutathimini na kuweka mikakati ya kufanya vizuri zaidi kwa mitini inayofuata.

Akiwasilisha mbele ya Mgeni wa heshima Mkuu wa Wilaya ya Mufindi  Mhe. Jamhuri William, Maofisa Elimu kata Waalimu Wakuu na Waalimu wa taaluma, ametanabaisha kuwa ufaulu umeendelea kupanda kutoka mwaka moja baada ya mwingine.

“Mwaka 2015 ufaulu wetu ulikuwa asilimia 84.4, mwaka 2016 ufaulu asilimia 84.9 tukishika nafasi ya 22 kitaifa kati ya Halmashauri 185, mwaka 2017 asilimia 84.37 tukishika nafasi ya 32 kitaifa kati ya Halmshauri 186, wakati mapema mwaka jana 2018 ufaulu umepanda kufikia asilimia 86.73 ambapo katika ushindani wa kitaifa tumeshika nafasi ya 35 kati ya Halmashauri 186. amesema

Akifafanua zaidi mafanikio ya mtihani wa mwaka 2018 Bi Ngalla, ameendelea kubainisha kuwa kati ya Shule kumi (10) zilizofanya vizuri kimkoa Halmshauri ya Mufindi imeingiza shule mbili (02) ambazo ni Ifwagi na Brooke Bond, lakini pia imeingiza Shule tano (05) kati ya Shule kumi (10) bora  za Serikali kwa ngazi ya Mkoa ambazo ni Shule ya Msingi Ifwagi, Mlimani, Nyanyembe, Kasanga na Makungu.

Akizungumza katika kikao hicho mgeni wa heshima Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. Jamhuri Willia, ameitaka idara ya Elimu Msingi kuongeza juhudi na mbinu za ufundishaji ili mtihani wa mwaka huu   waweze kufanya vizuri kwa kufaulisha kwa Zaidi ya asilimia 90 na kusisitiza kuwa mazingira na rasilimali za Mufindi ni rafiki kwa Watoto kusoma na kufaulu.

Halmshauri ya Wilaya ya Mufindi yenye jumla ya shule 146 ilishiriki katika mtihani wa mwaka jana 2018, ikiwa na watahiniwa 6,570 kati yao wavulana ni 3,053 na Wasichana 3,517 sawa na asilimia 99.8 ya watainiwa waliofanya mtihani.


Sehemu ya Maofisa Elimu kata, Walimu wa kuu na Walimu wa taaluma kutoka Shule 146 za Halmashauri.

Saturday, January 12, 2019

JKT Tanzania SC Ikiwa ugenini imelazimishwa sare ya bila kufungana dhidi ya Lipili FC


.
Na Amani Mbwaga, Iringa.
Timu ya Jeshi la Kujenga Taifa JKT Tanzania imelazimishwa sare ya bila kufungana na kugawana pointi moja moja dhidi ya Timu ya Lipuli FC ya Mkoani Iringa wakati wa mchezo wa Ligi Kuuu Tanzania bara uliyochezwa jana katika uwanja wa Samora uliopo Iringa Mjini.

Kwa mujibu wa ratiba ya ligi kuu Tanzania bara Mchezo huo ulitakiwa kuchezwa jana Ijumaa lakini uliahirishwa kutokana na mvua kubwa kunyesha hali iliyopelekea uwanja kujaa maji na hatimae mchezo kusogezwa mbele na kucheza leo hii.

Mchezo huo ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka Jeshi la Kujenga Taifa makao makuu na vikosi vya JKT akiwemo Mkurugenzi wa Michezo JKT, Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano JKT, Kamanda Kikosi  Mafinga JKT, Afisa Habari wa Timu hiyo na maofisa wengine wa Jeshi ikiwa ni kuwatia moyo wachezaji na kuongeza ari ya ushindi katika michezo yao ya Ligi kuu.

Tuesday, January 8, 2019

Wizara ya Kilimo Kuja na Mkakati Kabambe wa Kuinua Zao la Chai Nchini


Ø Yajizatiti kuanzisha soko la chai nchini Tanzania

Na Amani Mbwaga, Mufindi
Hayo yamesemwa na Naibu waziri wa Kilimo Mhe. Inocent Bashungwa alipokuwa akiongea na Wananchi na wanachama wa Chama cha ushirika cha wakulima wa chai katika kijiji cha Mkonge wakati wa ziara yake ya kutembelea wakulima wadogo na wakubwa wa chai Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.

Akiwa katika Kijiji cha Mkonge Kata ya Luhunga Tarafa ya Ifwagi Mhe. Naibu Waziri Bashungwa alieleza namna wizara ilivyojiwekea mkakati wa kuinua zao la chai nchini, ikiwa na  lengo la kumnufaisha Mkulima ili kulifikisha Taifa katika Uchumi wa kati kwani zaidi ya asilimia 65.5% nchini ni wakulima hivyo ni lazima kufunganisha kilimo na viwanda ili kufikia lengo hilo.

“Ni wakati sasa wa kuona zao la chai linamnufaisha mkulima, nimeshawaelekeza bodi ya chai Tanzania haraka iwezekanavyo tuleteeni ule mkakati wa kitaifa wa kufufua zao la chai nchini na tutoke kwenye uzalishaji wa Tani 34,000 za sasa na angalau kufikia tani Laki nne 400,000 kuwafikia wenzetu wa kenya” alisema

Mhe. Bashungwa alisistiza kwamba ni lazima mkulima aone kwamba zao hili ni zao la kimkakati na linamuondoa kwenye umaskini kama Rais Dkt John Pombe Magufuli anavyotaka wasaidizi wake kuwasaidia wakulima ili kuwezesha taifa kufikia katika kipato cha kati kwa kuangalia fursa zilizopo.

“Uzalishaji wa chai kwenye upande wa masoko tayari tumeshaagiza bodi ya chai kufikia mwezi wa Mei mwaka huu 2019 mkakati wa kuanzisha soko la chai Tanzania pale Jijini Dar es salaam unakamilika na kuhakikisha chai inauzwa hapa nchini ili mwaka wa fedha wa 2020 unapoanza Julai tayari tunakuwa na mnada ili gharama za usafirishaji chai nje zinapopungua basi faida ile ije kumsaidia mkulima” Alisema

Aidha ameitaka Bodi ya chai Tanzania kueleza ni kwa nini wanapanga bei ndogo za ununuzi wa chai kwa wakulima wakati wanunuzi wananunua zaidi ya ile bei ndogo iliyopangwa na wao, bodi ya chai Kupitia kwa Mjumbe wake Dkt. Emmanuel Simbua alieleza namnamchakato unavyofanyika wa upangaji bei na kuahidi kubadilisha viwango vya bei elekezi ya ununuzi wa chai kutoka kwa wakulima mwaka huu 2019 kwa kuwashirikisha wadu wote.

Kutokana na changamoto mbalimbali za wakulima kabla ya mwezi Februari kitafanyika kikao cha wadau wa chai nchini hapa Mufindi kwa sababu ndipo asilimia takribani 70% ya uzalishaji wa chai  nchini unafanywa katika Wilaya ya Mufindi na Njombe na hapo changamoto nyingi za wakulima wa zao hilo zitapatiwa ufumbuzi na hatimae kuwainua wakulima wa chai nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William alisema serikali imejitahidi kutafuta wafadhili na wadau mbalimbali ambapo leo hii Mhe. Mbunge alikuja na Wataalamu kutoka wakala wa barabara vijijini na mjini TARULA kutoka makao makuu Dodoma kwa ajili ya kushughulikia suala la barabara hii Km 40 kutoka sawala hadi Lulanda ikiwa ni moja ya kupunguza changamoto ya miundombinu ya barabara ndani ya mashamba ya chai ili kuzisafirisha kwa urahisi.

Akisoma risala Katibu wa Chama cha Ushirika wa wakulima wa chai Mkonge Bwana Venusto Chang’a alieleza kwamba Changamoto nyingine ni mkulima kutoshiriki katika mnyororo wa thamani katika zao la chai kwa kuishia kuuza majani mabichi pekee na bei kubwa ya pembejeo inayopatikana bila ruzuku ya serikali.

Akijibu changamoto ya bei Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya chai Tanzania Bwana Theophord Ndunguru alikiri changamoto hiyo na kusema kwamba tatizo hilo linatokana na mnada wa soko kuwa Mombasa Kenya hivyo wao kujipendelea lakini pia ubora wa chai hivyo serikali tayari mkakati wake wa kuanzisha mnada wake Jijini Dar es salaam ili kusaidia bei kupanda unakamilika mwaka huu mwezi mei.

Mwaka 2017 chama hiki kilipata tuzo ya kuwa chama bora cha ushirika ngazi ya Mkoa na mwaka jana 2018 chama kilipata tuzo ya mshindi ngazi ya Taifa katika tasnia ya chai katika vyama vya msingi Tanzania sanjari na kufanikiwa kutoa Wakulima bora wa zao la chai kikanda na kitaifa kwa miaka mitano (5) mfululizo kuanzia mwaka 2008-2012.

Kilimo cha chai katika kijiji cha Mkonge kilianzishwa mwaka 1971 chini ya mamlaka ya chai Tanzania (MACHATA) au TTA wakulima waanzilishi walikuwa 174 ambao walimiliki hekta 118. Chama kilianzishwa mwaka 1989 kama kikundi cha wakulima baada ya Mamlaka ya chai Tanzania (TTA) Kusitishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa chama hiki lilikuwa ni kuwaunganisha wakulima wa chai Mkonge katika kilimo cha zao la chai na kuwa na sauti moja katika kudai haki kutatua changamoto pamoja na kutafuta fursa.


HABARI PICHA

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Innocent Bashungwa akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Isaya Mbenje.


Naibu waziri wa kilimo Mhe. Bashungwa  kulia akiwa na Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi Saada Mwaruka akifuatilia Maelekezo ya Naibu Waziri wa Kilimo kuhusu zao la Chai Kuli kwake ni Bwana Theophord Ndunguru Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania




Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Bashungwa Akitoa Maelekezo kwa bodi ya Chai Tanzania katika moja ya maabara ya Taasisi ya Chai Tanzania TRIT Wilaya ni Mufindi wakati wa ziara yake ya kutebelea akulima wa chai.(Picha zote na Amani Mbwaga)

Friday, January 4, 2019

DC Mufindi aongoza kikao cha kamati ya ushauri ya Wilaya Mufindi (DCC) na Kupitisha Mapendekezo ya Mpango wa bajeti ya mwaka 2019/2020.


Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William ameongoza kikao maalumu cha kamati ya ushauri ya Wilaya ya Mufindi kujadili kuridhia na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya Halmashauri zote za Mji Mafinga na Wilaya Mufindi kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

“Hiki ni kikao cha kawaida cha kamati ya Ushauri ya Wilaya ambacho kipo kisheria, serikali yetu ya wilaya mufindi chini ya Rais Wetu Dkt John Pombe Magufuli imetimiza miaka mitatu ya kuwepo madarakani na sisi kama wadau tumetimiza kwa njia moja au nyingine katika kuchangia pato la Taifa  kutokana na shughuli mbali mbali za kiuchumi na kutekeleza shughuli za  maendeleo ikiwemo utoaji wa elimu bure bila malipo afya, maji, kilimo, umeme, barabara na huduma nyingine nyingi za jamii”. Alisema Mhe. William

Kikao hicho kimefanyika kwa mujibu wa sheria ya fedha ya serikali za mitaa namba 9 ya mwaka 2013, Memoranda ya fedha ya serikali za mitaa (2009), agizo namba 15 (1) (a) (b) sheria ya bajeti Na. 11 Kifungu cha 21 ya mwaka 2015 na kanuni za Mikutano za Halmashauri ya Wilaya Mufindi na Mji Mafinga.

Kwa Mwaka 2019/2020 Halmashauri ya Wilaya Mufindi inatarajiwa kukusanya na kutumia fedha zaidi ya  jumla ya Tsh Bilioni 56.3 ambapo kiasi cha zaidi ya Tsh. Bilioni 39.1 ni Matumizi mengineyo kwa mchanganuo kwamba  mishahara ya Watumishi  ni zaidi ya  Bilioni 34.1 na Matumizi ya kawaida ni Bilioni 4.9.
Miradi ya Maendeleo itagharamiwa kiasi cha Tsh Bilioni 17.2 ambapo kati ya hizo, fedha za ndani ni Tsh Bilioni 8.7 na fedha za nje zitakuwa Bilioni 2.

Halmashauri kutokana na vyanzo vyake vya ndani inataraji kukusanya na kutumia jumla ya Tsh Bilioni  6.4 sawa na asilimia 14.4 ya bajeti yote, Mchango wa jamii kwenye Miradi ya  Maendeleo ni zaidi ya Bilioni 4.6 na Taasisi binafsi zinataraji kuchangia wastani wa Tsh Milioni 156.

Aidha Vipaumbele vya Halmashauri ya Wilaya Mufindi kwa mwaka 2019/2020 ni kuongeza upatikanaji wa huduma kwa kukamilisha miradi ya nyuma ambayo haikukamilika ikiwemo ya elimu na afya, ukarabati wa majengo ya baadhi ya shule za msingi, kuhimiza na kuongeza uzalishaji wa wa mazao ya kilimo na kuyaongezea thamani,  kuimarisha misingi ya utawala bora na kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia ya kielekronic.

Kwa upande wake Halmashauri ya Mji Mafinga kwa mwaka wa fedha 2019/2020 imeomba kuidhinishiwa, kukusanya na kutumia zaidi ya kiasi cha Bilioni 25.5 kwa ajili ya matumizi mengineyo na miradi ya maendeleo.
Kiasi cha zaidi ya Sh. Bilioni 3.7 kimekadiriwa kukusanywa kutokana na na vyanzo mbalimbali vya Halmsahauri, Makisio haya ni zaidi ya Sh. Milioni 472.6 ambayo ni asilimia 14.22 ukilinganisha na makisio ya mwaka 2018/2019 ya zaidi ya Bilioni 3.3.

Aidha zaidi ya Bilioni 17.1 zinaombwa kuidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida kati ya fedha hizo kiasi cha Tsh Bilioni 13.8 ni kwa ajili ya mishahara na Tsh Bilioni 3.3 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.

Katika Mwaka huu wa fedha 2019/2020 Halmashauri ya Mji Mafinga inataraji kukusanya na kutumia kiasi cha Bilioni 8.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo Ruzuku kutoka serikali kuu ambayo ni zaidi ya Bilioni 5.4, Fedha za Wahisani zaidi ya Milioni 869 Mapato ya ndani asilimia 40% zaidi Bilioni 1.3,   nguvu za wananchi na wadau wa maendeleo Milioni 768.

Aidha Halmashauri hiyo imetaja vipaumbele vyake vikuu kuelekea Bajeti hii katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato ambapo ni  uanzishaji wa miradi ya kimkakati yenye lengo la kuongeza mapato ikiwemo, ujenzi wa stendi kuu ya mabasi, ujenzi wa maegesho ya magari ya mizigo, ujenzi wa soko la kisasa la mazao ya misitu, ujenzi wa miundombinu ya vitegea uchumi na biashara, lakini pia kuboresha mazingira ya uwekezaji na ujenzi wa viwanda na kuwekeza katika kilimo ikiwemo mradi wa shamba la matunda ya parachichi  na mradi wa umwagiliaji  Mtula.

Mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2019/2020 yameandaliwa kwa kuzingatia mambo yafuatayo, Muongozo wa Bajeti wa 2019/2020, Ilani ya Uchaguzi ya chama Tawala - Ccm ya 2015/2016 -2019/2020, Malengo ya Maendeleo endelevu (SDGs), Dira ya Taifa ya maendeleo 2025, Maelekezo ya Ki- Sekta na Mpango wa maendeleo wa miaka mitano na mipango mikakati ya Halmashauri pamoja na vipaumbele vya Taifa kama vilivyofafanuliwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli wakati wa kufunga bunge la 11 Mjini Dodoma.

Vilevie umezingatia Mwongozo wa Serikali wa kuandaa Mipango na Bajeti wa mwaka 2019/2020 uliotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango mwezi Disemba 2018 ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya Bajeti Namba 11 ya mwaka 2015 sehemu ya 21 na 22.

Kwa Mujibu wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi. Saada Mwaruka na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Ndugu Isaya Mbenje wamebainisha kuwa Rasimu hiyo ya Mpango wa bajeti ya halmashauri hizo ni makadirio ya mapato na matumizi ya miradi ya maendeleo kwa mwaka 2019/2020 hivyo bado yanaendelea kujadiliwa na kupitiwa kwenye Baraza la wafanyakazi Mkoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango.

Kwa hiyo maboresho yoyote yatakayotolewa yatajumuishwa ili kuboresha mpango na bajeti za Halmashauri hizo, vilevile marekebisho yataendelea kufanyika kutegemeana na ukomo wa bajeti utakaotolewa na serikali kwenye maeneo ya ruzuku.

HABARI PICHA
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri Davidi William Mwenyekiti wa Kikao cha Ushauri cha Wilaya (DCC)

Mbunge wa Jimbo la Mufindi kusini Mhe. Menradi Kigola akichangia baadhi ya hoja katika kikao cha ushauri  DCC

Menyekiti wa Hamashauri ya Mji Mafinga Mhe. Charles Makoga

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mhe. Festo Mgina
Kaimu Mkurugenzi wa Hamashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Isaya Mbenje


Bi Saada S. Mwaruka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga
Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Mufindi (DAS)




Waliokaa mbele Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Mufindi wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa Rasimu ya bajeti ya mwaka 2019/2020
Baadhi ya wakuu wa Idara kutoka Halmashauri ya Wilaya Mufindiwakifuatilia kwa makini kikao hicho cha ushauri DCC
Waandishi wa Vikao








Mhandisi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARULA Bwana Sanga akitoa Taarifa ya utekelezaji wa Matengenezo ya Barabara na Mpango wa Bajeti ya TARULA  2019/2020 Katika kikao cha ushauri cha Wilaya ya Mufindi




Diwani wa kata ya Sao Hill akichangia Moja ya Agenda


Afisa Tarafa wa Kasanga Bwana Dugange nae akichangia moja ya agenda ya TARULA

Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Kyomo akisoma Rasimu ya Mpango wa Bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020



Kaimu Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Quman akisoma Rasimu ya Mpango wa Bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020
(Picha zote na Amani Mbwaga)