Mkuu wa Wilaya
Mufindi Mhe. Jamhuri William ameongoza kikao maalumu cha kamati ya ushauri ya
Wilaya ya Mufindi kujadili kuridhia na kupitisha mapendekezo ya bajeti ya
Halmashauri zote za Mji Mafinga na Wilaya Mufindi kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
“Hiki ni kikao cha
kawaida cha kamati ya Ushauri ya Wilaya ambacho kipo kisheria, serikali yetu ya
wilaya mufindi chini ya Rais Wetu Dkt John Pombe Magufuli imetimiza miaka
mitatu ya kuwepo madarakani na sisi kama wadau tumetimiza kwa njia moja au
nyingine katika kuchangia pato la Taifa
kutokana na shughuli mbali mbali za kiuchumi na kutekeleza shughuli
za maendeleo ikiwemo utoaji wa elimu
bure bila malipo afya, maji, kilimo, umeme, barabara na huduma nyingine nyingi
za jamii”. Alisema Mhe. William
Kikao hicho
kimefanyika kwa mujibu wa sheria ya fedha ya serikali za mitaa namba 9 ya mwaka
2013, Memoranda ya fedha ya serikali za mitaa (2009), agizo namba 15 (1) (a)
(b) sheria ya bajeti Na. 11 Kifungu cha 21 ya mwaka 2015 na kanuni za Mikutano
za Halmashauri ya Wilaya Mufindi na Mji Mafinga.
Kwa Mwaka 2019/2020 Halmashauri
ya Wilaya Mufindi inatarajiwa kukusanya na kutumia fedha zaidi ya jumla ya Tsh Bilioni 56.3 ambapo kiasi cha zaidi
ya Tsh. Bilioni 39.1 ni Matumizi mengineyo kwa mchanganuo kwamba mishahara ya Watumishi ni zaidi ya Bilioni 34.1 na Matumizi ya kawaida ni Bilioni
4.9.
Miradi ya Maendeleo
itagharamiwa kiasi cha Tsh Bilioni 17.2 ambapo kati ya hizo, fedha za ndani ni
Tsh Bilioni 8.7 na fedha za nje zitakuwa Bilioni 2.
Halmashauri kutokana
na vyanzo vyake vya ndani inataraji kukusanya na kutumia jumla ya Tsh
Bilioni 6.4 sawa na asilimia 14.4 ya
bajeti yote, Mchango wa jamii kwenye Miradi ya Maendeleo ni zaidi ya Bilioni 4.6 na Taasisi
binafsi zinataraji kuchangia wastani wa Tsh Milioni 156.
Aidha Vipaumbele vya
Halmashauri ya Wilaya Mufindi kwa mwaka 2019/2020 ni kuongeza upatikanaji wa
huduma kwa kukamilisha miradi ya nyuma ambayo haikukamilika ikiwemo ya elimu na
afya, ukarabati wa majengo ya baadhi ya shule za msingi, kuhimiza na kuongeza
uzalishaji wa wa mazao ya kilimo na kuyaongezea thamani, kuimarisha misingi ya utawala bora na
kuimarisha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa njia ya kielekronic.
Kwa upande wake
Halmashauri ya Mji Mafinga kwa mwaka wa fedha 2019/2020 imeomba kuidhinishiwa,
kukusanya na kutumia zaidi ya kiasi cha Bilioni 25.5 kwa ajili ya matumizi
mengineyo na miradi ya maendeleo.
Kiasi cha zaidi ya Sh.
Bilioni 3.7 kimekadiriwa kukusanywa kutokana na na vyanzo mbalimbali vya
Halmsahauri, Makisio haya ni zaidi ya Sh. Milioni 472.6 ambayo ni asilimia
14.22 ukilinganisha na makisio ya mwaka 2018/2019 ya zaidi ya Bilioni 3.3.
Aidha zaidi ya
Bilioni 17.1 zinaombwa kuidhinishwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida kati ya
fedha hizo kiasi cha Tsh Bilioni 13.8 ni kwa ajili ya mishahara na Tsh Bilioni
3.3 ni kwa ajili ya matumizi mengineyo.
Katika Mwaka huu wa
fedha 2019/2020 Halmashauri ya Mji Mafinga inataraji kukusanya na kutumia kiasi
cha Bilioni 8.4 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo kutoka vyanzo
mbalimbali ikiwemo Ruzuku kutoka serikali kuu ambayo ni zaidi ya Bilioni 5.4,
Fedha za Wahisani zaidi ya Milioni 869 Mapato ya ndani asilimia 40% zaidi Bilioni
1.3, nguvu za wananchi na wadau wa
maendeleo Milioni 768.
Aidha Halmashauri hiyo
imetaja vipaumbele vyake vikuu kuelekea Bajeti hii katika kuimarisha ukusanyaji
wa mapato ambapo ni uanzishaji wa miradi
ya kimkakati yenye lengo la kuongeza mapato ikiwemo, ujenzi wa stendi kuu ya
mabasi, ujenzi wa maegesho ya magari ya mizigo, ujenzi wa soko la kisasa la
mazao ya misitu, ujenzi wa miundombinu ya vitegea uchumi na biashara, lakini pia
kuboresha mazingira ya uwekezaji na ujenzi wa viwanda na kuwekeza katika kilimo
ikiwemo mradi wa shamba la matunda ya parachichi na mradi wa umwagiliaji Mtula.
Mapendekezo ya
Bajeti ya mwaka 2019/2020 yameandaliwa kwa kuzingatia mambo yafuatayo, Muongozo
wa Bajeti wa 2019/2020, Ilani ya Uchaguzi ya chama Tawala - Ccm ya 2015/2016
-2019/2020, Malengo ya Maendeleo endelevu (SDGs), Dira ya Taifa ya maendeleo
2025, Maelekezo ya Ki- Sekta na Mpango wa maendeleo wa miaka mitano na mipango
mikakati ya Halmashauri pamoja na vipaumbele vya Taifa kama vilivyofafanuliwa
na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli wakati
wa kufunga bunge la 11 Mjini Dodoma.
Vilevie umezingatia
Mwongozo wa Serikali wa kuandaa Mipango na Bajeti wa mwaka 2019/2020 uliotolewa
na Wizara ya Fedha na Mipango mwezi Disemba 2018 ikiwa ni utekelezaji wa sheria
ya Bajeti Namba 11 ya mwaka 2015 sehemu ya 21 na 22.
Kwa Mujibu wa Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi. Saada Mwaruka na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Wilaya Mufindi Ndugu Isaya Mbenje wamebainisha kuwa Rasimu hiyo
ya Mpango wa bajeti ya halmashauri hizo ni makadirio ya mapato na matumizi ya
miradi ya maendeleo kwa mwaka 2019/2020 hivyo bado yanaendelea kujadiliwa na
kupitiwa kwenye Baraza la wafanyakazi Mkoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na
Wizara ya Fedha na Mipango.
Kwa hiyo maboresho yoyote yatakayotolewa yatajumuishwa ili kuboresha mpango na bajeti za Halmashauri hizo, vilevile marekebisho yataendelea kufanyika kutegemeana na ukomo wa bajeti utakaotolewa na serikali kwenye maeneo ya ruzuku.
HABARI PICHA
Mbunge wa Jimbo la Mufindi kusini Mhe. Menradi Kigola akichangia baadhi ya hoja katika kikao cha ushauri DCC |
Menyekiti wa Hamashauri ya Mji Mafinga Mhe. Charles Makoga |
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mhe. Festo Mgina |
Kaimu Mkurugenzi wa Hamashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Isaya Mbenje |
Bi Saada S. Mwaruka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga |
Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Mufindi (DAS) |
Waliokaa mbele Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Mufindi wakifuatilia kwa makini uwasilishwaji wa Rasimu ya bajeti ya mwaka 2019/2020 |
Baadhi ya wakuu wa Idara kutoka Halmashauri ya Wilaya Mufindiwakifuatilia kwa makini kikao hicho cha ushauri DCC |
Waandishi wa Vikao |
Diwani wa kata ya Sao Hill akichangia Moja ya Agenda |
Afisa Tarafa wa Kasanga Bwana Dugange nae akichangia moja ya agenda ya TARULA |
Afisa Mipango wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bwana Kyomo akisoma Rasimu ya Mpango wa Bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 |
Kaimu Afisa Mipango wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Quman akisoma Rasimu ya Mpango wa Bajeti ya Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2019/2020 |
(Picha zote na Amani Mbwaga) |
No comments:
Post a Comment