Tuesday, January 8, 2019

Wizara ya Kilimo Kuja na Mkakati Kabambe wa Kuinua Zao la Chai Nchini


Ø Yajizatiti kuanzisha soko la chai nchini Tanzania

Na Amani Mbwaga, Mufindi
Hayo yamesemwa na Naibu waziri wa Kilimo Mhe. Inocent Bashungwa alipokuwa akiongea na Wananchi na wanachama wa Chama cha ushirika cha wakulima wa chai katika kijiji cha Mkonge wakati wa ziara yake ya kutembelea wakulima wadogo na wakubwa wa chai Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.

Akiwa katika Kijiji cha Mkonge Kata ya Luhunga Tarafa ya Ifwagi Mhe. Naibu Waziri Bashungwa alieleza namna wizara ilivyojiwekea mkakati wa kuinua zao la chai nchini, ikiwa na  lengo la kumnufaisha Mkulima ili kulifikisha Taifa katika Uchumi wa kati kwani zaidi ya asilimia 65.5% nchini ni wakulima hivyo ni lazima kufunganisha kilimo na viwanda ili kufikia lengo hilo.

“Ni wakati sasa wa kuona zao la chai linamnufaisha mkulima, nimeshawaelekeza bodi ya chai Tanzania haraka iwezekanavyo tuleteeni ule mkakati wa kitaifa wa kufufua zao la chai nchini na tutoke kwenye uzalishaji wa Tani 34,000 za sasa na angalau kufikia tani Laki nne 400,000 kuwafikia wenzetu wa kenya” alisema

Mhe. Bashungwa alisistiza kwamba ni lazima mkulima aone kwamba zao hili ni zao la kimkakati na linamuondoa kwenye umaskini kama Rais Dkt John Pombe Magufuli anavyotaka wasaidizi wake kuwasaidia wakulima ili kuwezesha taifa kufikia katika kipato cha kati kwa kuangalia fursa zilizopo.

“Uzalishaji wa chai kwenye upande wa masoko tayari tumeshaagiza bodi ya chai kufikia mwezi wa Mei mwaka huu 2019 mkakati wa kuanzisha soko la chai Tanzania pale Jijini Dar es salaam unakamilika na kuhakikisha chai inauzwa hapa nchini ili mwaka wa fedha wa 2020 unapoanza Julai tayari tunakuwa na mnada ili gharama za usafirishaji chai nje zinapopungua basi faida ile ije kumsaidia mkulima” Alisema

Aidha ameitaka Bodi ya chai Tanzania kueleza ni kwa nini wanapanga bei ndogo za ununuzi wa chai kwa wakulima wakati wanunuzi wananunua zaidi ya ile bei ndogo iliyopangwa na wao, bodi ya chai Kupitia kwa Mjumbe wake Dkt. Emmanuel Simbua alieleza namnamchakato unavyofanyika wa upangaji bei na kuahidi kubadilisha viwango vya bei elekezi ya ununuzi wa chai kutoka kwa wakulima mwaka huu 2019 kwa kuwashirikisha wadu wote.

Kutokana na changamoto mbalimbali za wakulima kabla ya mwezi Februari kitafanyika kikao cha wadau wa chai nchini hapa Mufindi kwa sababu ndipo asilimia takribani 70% ya uzalishaji wa chai  nchini unafanywa katika Wilaya ya Mufindi na Njombe na hapo changamoto nyingi za wakulima wa zao hilo zitapatiwa ufumbuzi na hatimae kuwainua wakulima wa chai nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William alisema serikali imejitahidi kutafuta wafadhili na wadau mbalimbali ambapo leo hii Mhe. Mbunge alikuja na Wataalamu kutoka wakala wa barabara vijijini na mjini TARULA kutoka makao makuu Dodoma kwa ajili ya kushughulikia suala la barabara hii Km 40 kutoka sawala hadi Lulanda ikiwa ni moja ya kupunguza changamoto ya miundombinu ya barabara ndani ya mashamba ya chai ili kuzisafirisha kwa urahisi.

Akisoma risala Katibu wa Chama cha Ushirika wa wakulima wa chai Mkonge Bwana Venusto Chang’a alieleza kwamba Changamoto nyingine ni mkulima kutoshiriki katika mnyororo wa thamani katika zao la chai kwa kuishia kuuza majani mabichi pekee na bei kubwa ya pembejeo inayopatikana bila ruzuku ya serikali.

Akijibu changamoto ya bei Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya chai Tanzania Bwana Theophord Ndunguru alikiri changamoto hiyo na kusema kwamba tatizo hilo linatokana na mnada wa soko kuwa Mombasa Kenya hivyo wao kujipendelea lakini pia ubora wa chai hivyo serikali tayari mkakati wake wa kuanzisha mnada wake Jijini Dar es salaam ili kusaidia bei kupanda unakamilika mwaka huu mwezi mei.

Mwaka 2017 chama hiki kilipata tuzo ya kuwa chama bora cha ushirika ngazi ya Mkoa na mwaka jana 2018 chama kilipata tuzo ya mshindi ngazi ya Taifa katika tasnia ya chai katika vyama vya msingi Tanzania sanjari na kufanikiwa kutoa Wakulima bora wa zao la chai kikanda na kitaifa kwa miaka mitano (5) mfululizo kuanzia mwaka 2008-2012.

Kilimo cha chai katika kijiji cha Mkonge kilianzishwa mwaka 1971 chini ya mamlaka ya chai Tanzania (MACHATA) au TTA wakulima waanzilishi walikuwa 174 ambao walimiliki hekta 118. Chama kilianzishwa mwaka 1989 kama kikundi cha wakulima baada ya Mamlaka ya chai Tanzania (TTA) Kusitishwa.

Lengo la kuanzishwa kwa chama hiki lilikuwa ni kuwaunganisha wakulima wa chai Mkonge katika kilimo cha zao la chai na kuwa na sauti moja katika kudai haki kutatua changamoto pamoja na kutafuta fursa.


HABARI PICHA

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Innocent Bashungwa akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Isaya Mbenje.


Naibu waziri wa kilimo Mhe. Bashungwa  kulia akiwa na Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe. Jamhuri William


Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi Saada Mwaruka akifuatilia Maelekezo ya Naibu Waziri wa Kilimo kuhusu zao la Chai Kuli kwake ni Bwana Theophord Ndunguru Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Chai Tanzania




Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Bashungwa Akitoa Maelekezo kwa bodi ya Chai Tanzania katika moja ya maabara ya Taasisi ya Chai Tanzania TRIT Wilaya ni Mufindi wakati wa ziara yake ya kutebelea akulima wa chai.(Picha zote na Amani Mbwaga)

No comments:

Post a Comment