Monday, July 30, 2018

Naibu Waziri TAMISEMI Aipa Mwezi Mmoja MSD Kupeleka Vifaa Tiba Kituo Cha Afya Ihongole

Naibu Waziri  Ofisi ya Rais TAMISEMI Mh Joseph Kakunda wa kwanza Kushoto alipowasili katika kituo cha Afya Ihongole wakati wa ziara yake Wilaya ya Mufindi (Picha na Amani Mbwaga)
Na Amani Mbwaga Mafinga- Iringa
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe Joseph George Kakunda ameitaka Bohari ya Dawa (MSD) Kupeleka vifaa Tiba mara moja katika kituo cha Afya Ihongole kilichopo katika Halmashauri ya Mji Mafinga Mkoani Iringa.

Ameyasema hayo leo alipotembelea kituo hicho wakati wa ziara yake ya kikazi katika Wilaya ya Mufindi na Halmashauri zake na kukagua Jengo la Maabara na Chumba cha Upasuaji (Theatre)

Mh Kakunda ameiagiza MSD kuhakikisha wanapeleka vifaa tiba haraka iwezekanavyo na kutoa muda wa mwezi mmoja kuhakikisha vifaa na Madawa yanayotakiwa katika kituo hicho yanafika kwa wakati ili huduma muhimu zilizokusudiwa zianze kutolewa kwa Wananchi.

“Kituo chetu kimejengwa vizuri sana kwa viwango vyetu vya kitaifa, nimekagua chumba cha upasuaji nimeona kiko tayari kabisa kuanza kazi bado vifaa tiba tu” alisema Mh Kakunda.

 Aidha aliwapongeza Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi na Wakuu wa Idara kwa usimamizi mzuri, “kazi hii imefanyika vizuri sana mimi kwa kweli napeleka ujumbe kwa Mhe Makamu wa rais aliyeweka jiwe la msingi kwamba kituo kimekamilika vizuri hongereni sana” alisema Naibu Waziri Mh Kakunda.

Upanuzi na ukarabati wa kituo cha Afya Ihongole ulipangwa kutumia kiasi cha Tsh Milioni 500 ambazo zote zimetolewa na Serikali kuu.

Utekelezaji wa maradi huu ulianza mwezi Novemba 2017 mpaka sasa umegharimu kiasi cha Tsh Milioni 485 ambazo ujenzi na ukarabati upo kwenye hatua za umaliziaji, fedha iliyobaki kiasi cha Tsh Milioni 15 itatumika kuweka mfumo wa GOTHOMIS pamoja na umaliziaji wa malipo ya kazi ndogo ndogo zilizobakia.

Hali ya utoaji huduma katika kituo cha afya Ihongole ni nzuri na imeendelea kuimarika hususani baada ya kuongezeka kwa fedha zinazotumika kununua dawa.

Akisoma taarifa ya upanuzi wa kituo Mganga Mfawidhi wa kituo cha Afya Ihongole Bi Proserpina Kalanje alisema lengo la mradi huo ni kupunguza vifo vya watoto wachanga na kinamama wajawazito kwa kuimarisha miundombinu na kuboresha huduma za Afya katika kituo ili kiweze kutoa huduma za upasuaji wa dharula na huduma ya kuongeza damu.

“Ili kufanikisha hilo Mradi umelenga kuongeza majengo ya upasuaji, Maabara na Wodi ya wazazi lakini pia tunachangamoto ya uhaba wa watumishi kwani mmpaka sasa kituo kina watumishi 16 Wakati Mahitaji ni 49 hivyo tunaiomba serikali kutuongezea watumishi ili wananchi waendelee kupata huduma bora zaidi” alisema Bi Kalanje.

Kituo hiki kilianza kutoa huduma mwaka 2008 ambapo kilikuwa kinahudumia wastani wa watu 5,000 kwa mwaka na kwa sasa kinahudumia wastani wa watu 26,032 kwa mwaka ikiwa ni ongezeko la wastani wa watu 21,032 kutoka katika kata jirani za Kinyanambo, Changarawe na Isalavanu. 


HABARI PICHA


Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe Joseph Kakunda wa kwanza kushoto akiongea na Baadhi ya Watumushi wa Kituo cha Afya Ihongole baada ya kukagua Majengo ya Maabara na Chumba cha Upasuaji (Picha na Amani Mbwaga)
Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ihongole Bi Proserpina Kalanje akisoma taarifa ya kituo kwa Mhe Naibu Waziri TAMISEMI.
Naibu Waziri Mhe Kakunda akisikiliza taarifa ya kituo cha Afya Ihongole Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Mafinga Bi Saada Mwaruka na anayefuatia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga Diwan Charles Makoga.







Naibu Waziri Mhe Kakunda aliyeshika mtoto akipata maelezo ya Jengo la Maabara ambalo tayari limeanza kutoa huduma kwa wagojwa mbalimbali kituoni hapo kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya Mufindi Mh Jamhuri David William

Naibu Waziri TAMISEMI akisalimiana na Baadhi ya Watumishi wa Kituo cha Afya Ihongole
 
 
Naibu Wazziri Mh Kakunda akikagua Jengo Jipya  la Upasuaji(Theatre) katika Kituo cha Afya Ihongole

Baadhi ya Watumishi wa Halmashauri ya Mji Mafinga wakiwa katika Jengo la Upasuaji, aliyevaa suti ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi sasa ni Katibu Tawala (RAS) Mkoa wa Ruvuma

DR.Innocent Mhagama  Mganga Mkuu Halmashauri ya Mji Mafinga akitoa Maelezo ya Jengo la Upasuaji kwa Naibu Waziri TAMISEMI Mhe Kakunda.


Naibu Waziri TAMISEMI Mh Joseph Kakunda (Kushoto) akipokea Taarifa ya Wilaya ya Mufindi kutoka kwa Mkuu waWilaya hiyo Mh Jamhuri David William                               (Picha zote na Amani Mbwaga)


No comments:

Post a Comment