Wednesday, July 25, 2018

Naibu Waziri Ulega Ataka Shamba la Kuzalisha Mifugo Sao Hill Kuwa Mfano.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdalla Hamis Ulega akitoa maelekezo kwa wataalamu wa shamba la Mifugo Sao Hill wakati wa Ziara yake ya Kikazi Mafinga (Picha na Amani Mbwaga)
Na Amani Mbwaga Mafinga, Iringa
Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdalla Hamis Ulega amewataka Mameneja Mashamba ya uzalishaji Mifugo kote nchini, kuhakikisha wanaongeza uzalishaji katika mashamba hayo ili kuwa mfano wa kuigwa na kuleta tija katika jamii zinaozunguka mashamba hayo na Taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo leo wakati wa ziara yake ya kikazi Mkoani Iringa, katika Wilaya ya Mufindi, alipotembelea, miradi mbalimbali ya wananchi katika Halmashauri ya Mji Mafinga na Halmashauri ya Wilaya Mufindi, ambapo amejionea vikundi mbalimbali vya ukusanyaji maziwa yenye ubora kutoka kwa wafugaji na kuyaongezea thamani kisha kuyauza.

Akiwa katika Shamba la Uzalishaji Mifugo Sao Hill Livestock Multplication Unit (L.M.U) lililopo km 13 kusini mashariki mwa mji wa Mafinga katika Kijiji cha Itulavanu, Mhe Naibu Waziri Ulega alipokea taarifa ya utendaji na kisha kutoa maelekezo kwa wataalamu wa shamba hilo kuhakikisha wanaongeza uzalishaji zaidi.

“Tunataka mtoe Mitamba ya kutosha ambayo itakwenda kwa Wananchi, mkakati wetu ni kuona viwanda vya maziwa vinapata maziwa ya kutosha kutoka kwa wafugaji wetu na si kuagiza maziwa kutoka nje kama ilivyo sasa”alisema Mhe Ulega.

Alibainisha kwamba kwa mujibu wa ilani ya mwaka 2015 inayoongoza nchi inawataka kuzalisha Mitamba isiyopungua 5000 kwa mwaka kutoka katika mashamba yake ya Sao Hill, Nangaramo, Kitulo, Ngerengere na Mabuki, hivyo mwaka huu wamedhamiria kufanya zaidi katika uzalishaji wa Mitamba.

Mhe Ulega alisema “Mkakati wa Serikali ni kuboresha Mifugo na kuongeza jitihada za kutoa huduma za magonjwa kuhakikisha tunachanja mifugo, na pia tumepanga kuhamilisha Ng’ombe takribani 3000 kwa mwaka katika vituo vyetu vyote vya Uhamilishaji vya Arusha, Iringa, Tabora, Lindi na Ruvuma, ii kufanya sekta hii kuwa na mchango mkubwa wa maendeleo kwa Taifa letu sambamba kabisa na Tanzania ya Viwanda.

Kwa Upande wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William aliwataka wananchi wanouzungukwa na Shamba hilo kuendeleza ushirikiano na  uhusiano mzuri baina yao ili shamba liwaletee tija wao pamoja na Taifa kwa ujumla.

Akitoa taarifa ya utendaji kwa Naibu Waziri, Meneja wa Shamba la Uzalishaji Mifugo Sao Hill Bwana Nickson Keiya  alisema, Shamba lina ukubwa wa hekta 6,365, lina uwezo wa kutunza ngo’mbe 3000, lakini mpaka sasa kuna ngo’mbe 1,773.

“Aidha Mwaka 2014 Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi ilieta mtambo wa kuzalisha gesi aina ya kimiminika baridi ya nitrogen (LN2 Plant) gesi hii hutumika katika utunzaji wa mbegu za madume (Semen) zinazotumika katika upandishaji wa ngo’mbe kwa njia ya chupa” Alisema Bwana Keiya.

Vilevile gesi hiyo hutumika katika vituo vya utafiti wa magonjwa ya binadamu na wanyama, mtambo huo unauwezo wa kuzalisha lita 5 kwa saa na hutumia Unit 14 za umeme mtambo huu pia umeunganishwa kwenye mtungiwenye uwezo wa kutunza lita 300 wakati wa uzalishaji.

Kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 shamba lilipima na kuwapandisha kwa njia ya Uhimilishaji jumla ya ngo,mbe  451 na kati ya hao walioshika mimba walikuwa 310 sawa na asilimia 69.

Bwana Keiya amemthibitishia Mh Naibu Waziri kwamba sasa wamejiwekea mikakati madhubuti na malengo ya kuhakikisha wanajiendesha kibiashara baada ya wizara kukubali mabadiliko ya bei za mitamba na kuwezesha shamba kujiendesha bila kutegemea usaidizi kutoka makao makuu ya Wizara.


Shamba la Kuzalisha Mitamba Sao Hill ni Shamba linalomilikiwa na serikali chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, shamba lina jukumu la kuzalisha mitamba Chotara inayotokana na Ngo’ombe aina ya Boran (Jike) na dume aina ya Ayrshire kupata mitamba chotara ili kufikia lengo la Taifa la Kujitegemea kwa Chakula, Kuboresha lishe, kukuza uchumi na kipato cha mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa Ujumla.

HABARI PICHA

Naibu Waziri Mhe Ulega akipokea Maelezo Kutoka kwa Meneja wa Shamba Bwana Nickson Keiya Jinsi Mtambo wa  kuzalisha Kimiminika Baridi cha Nitrogeni Kinavyofanya kazi ya utunzaji wa mbegu za madume kwa ajili ya upandishaji wa Ngombe kwa njia ya Chupa (Picha na Amani Mbwaga)



Naibu Waziri wa Mifugo Mhe Ulega wa pili Kushoto  akiangalia baadhi ya majengo mapya yatakayotumika kuhifadhi mifugo itakayozalishwa kwa njia ya chupa katika Shamba la Mifugo Sao Hill.
Baadhi ya Majengo mapya yatakayotumika kuhifadhi Ngombe watakaozalishwa kwa njia ya Upandishwaji wa chupa
Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Ulega akiendesha trekta linalovuna nyasi kwa ajili ya Chakula cha ng'ombe lililopo katika Shamba la Mifugo Sao Hill Mafinga



Meneja wa Shamba la Mifugo Sao Hill Bwana Nickson Keiya akitoa maelezo ya shamba la Malisho kwa Naibu waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Ulega aliyekulia kwake na Kushoto kwake ni Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William 
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Ulega akimuuliza maswali Afisa Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Mji Mafinga juu ya Malisho ya wafugaji wa Mafinga
Meneja wa Shamba la Mifugo Sao Hill Bwana Nickson Keiya Aakisoma Taarifa ya Utendaji wa Shamba kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi (Hayupo Pichani) alipotembelea wakati wa ziara yake ya kikazi katika wilaya ya Mufindi








Baadhi ya ng'ombe wanaopatikana katika Shamba la Mifugo Sao Hill

Naibu Waziri Mhe Ulega akiongea na Vyombo vya Habari kueleza lengo la ziara yake na mikakati iliyopo kutoka wizarani kwa ajili ya maendeleo ya mifugo na uvuvi

Mhe Ulega akiwa katika Picha ya Pamoja  watumishi mbalimbali wa serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri Davidi William

Naibu Waziri Mhe Ulega alipoenda kuongoea na  Wananchi wa Kijiji cha Itulavanu moja ya kjiji kilichokaribu na shamba la Mifugo sao hill kuona jinsi gani wananufaika na uwepo wa Shamba hilo.


Mhe Naibu Waziri akikaribishwa na Mwenyeji wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William
Mhe Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Abdalla Ulega Kushoto na Kulia walioshika maziwa Mbunge wa Mufindi  Kusini Mhe Menradi Kigola wakiangalia kwa makini jinsi maziwa yalivyopakiwa kwenye chupa tayari kwa mauzo kutoka katika kikundi cha wastaafu Mafinga Mjini kinachokusanya maziwa yenye ubora na kuyauza kwa lengo la kujiongezea kipato.






Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdalla Ulega na Mhe Menrad Kigola Mbunge wa Mufindi Kusini  Wakinywa maziwa yanayotengenezwa na chama cha Ushirika cha wafugaji Mufindi walipotembelea wanaushirika hao katika kijiji cha Igowole kilichopo Halmashauri ya Wilaya Mufindi (Picha zote na Amani Mbwaga)

No comments:

Post a Comment