Sunday, July 29, 2018

Naibu Waziri Ulega Akipongeza Chama cha Ushirika cha Wafugaji Mufindi (MUDCO)

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdalah Hamis Ulega na Mbunge wa Mufindi Kusini Mhe Menrad Kigola Wakifurahia Utamu wa Maziwa yanayotengenezwa na chama cha Ushirika cha Wafugaji Mufindi (MUDCO) 

Na Amani Mbwaga, Mafinga- Iringa
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdalah Hamis Ulega amekipongeza chama cha ushirika cha wafugaji Mufindi Dairy Cooperative Society (MUDCO) kutokana na jitihada zake za kuanzisha viwanda vidogo vya kukusanya maziwa kuyaongezea thamani na kuyauza.

Ameyasema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi katika Halmashauri ya wilaya Mufindi, alipotembelea wanachama hao na kuridhika na jitihada wanazozifanya za kuhakikisha Tanzania ya Viwanda inafikiwa ambapo imesaidia pia ajira kwa vijana Wazee na kina mama waliojiunga na Ushirika huo.

“Nawapongeza sana kwa jitihada zenu sisi kama wizara tumefurahi sana na tunawaunga mkono kwa juhudi zenu na ninamuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi ahakikishe anawapa kipaumbele katika fedha za Mikopo inayotolewa na serikali kwa ajili ya vijana na kina mama ili ziwasaidie kufikia malengo yenu mliyojiwekea kwa manufaa ya Taifa letu” alisema Mhe Ulega.

Kwa upande wake Mbunge wa Mufindi Kusini Mhe Menradi Kigola ameungana na wanachama hao kusaidia kutatua baadhi ya changamoto mbalimbali walizonazo ikiwemo suala la usafiri ambapo emeahidi kuchangia pikipiki moja itakayosaidia katika ukusanyaji wa maziwa kutoka kwa wafugaji.

Aidha Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William amesema kwamba atahakikisha anaendelea kuwapa ushirikiano wa kutosha ili kupunguza changamoto walizonazo na hatimaye kuchochea maendeleo ya wilaya ya Mufindi na Taifa kwa ujumla.

Akisoma taarifa kwa Mhe Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi ,Mratibu wa Kitovu chama cha wafugaji wilaya ya Mufindi (MUDCO) Bwana Ernest Haule amesema toka kuanzishwa kwa ushirika huo wamefanikiwa kuongezeka wanachama kutoka 147 mwaka 2014 hadi 414 mwaka 2018 ambapo kati yao mwanaume ni 216 na wanawake 149 pamoja na kikundi kimoja cha wafugaji.

“Ushirika kupitia serikali, wafugaji na mradi wa East Africa Dairy Development (EADD) umeweza kutusaidia kuanzisha biashara ya maziwa kupitia kitovu lakini pia kuwa na vituo vingine vidogo 4 vilivyopo kata za Nyololo, Mtwango, Ikongosi na Mji wa Mafinga vinavyopokea maziwa ya wanachama wetu na kupata huduma mbalimbali kutoka kwenye kituo mama Igowole” alisema Bwana Haule.

Ushirika ulianza kupokea maziwa lita 41 kwa siku mwaka 2016  na kufikia lita 650 kwa siku mwaka huu 2018, ambapo huuzwa kama mtindi na freshi hii ilimetokana na mwitikio mkubwa wa wafugaji kuuza maziwa yao kwa pamoja na kwa soko la uhakika.

Aidha kupitia mradi wa East Africa Dairy Development II (EADD II) na wafanyakazi wa ushirika wameweza kuunda vikundi 89 vyenye wastani wa wafugaji 25-30 kwa kikundi na kuwa na wanavikundi 2423 kati yao,  wanaume ni 1365 na wanawake 1058.

Ushirika huu umeweza kuboresha soko la maziwa na kuwa la uhakika kwa wafugaji wengi sana ambao awali hawakuwa na soko maalumu.
Chama hiki cha Wafugaji Mufindi kina malengo mengi ikiwemo kuendelea kutoa pembejeo kwa wafugaji kwa gharama nafuu na kwa huduma zenye uhakika mfano matibabu, chanjo, na vyakula vya mifugo.

Pia Kuongeza kiasi cha maziwa kutoka lita 650 za sasa kwa siku hadi lita 1500 ifikapo mwakani juni 2019 kutokana na mikakati mbalimbali kwa kuzidi kuhamasisha watu kununua ng`ombe bora wa maziwa.

Chama hiki cha ushirika cha wafugaji Mufindi (MUDCO) kilisajiliwa mwaka 2015 kwa mujibu wa sheria za ushirika za Tanzania kikiwa na malengo ya kuboresha maisha ya wafugaji wote wa wilaya ya Mufindi.

Kwa sasa chama hiki kinafanya kazi katika kata 15, zikiwamo kata 10 za Halmashauri ya wilaya Mufindi na kata 5 za Halmashauri ya Mji waMafinga kwa kupitia soko la pamoja la maziwa na utoaji wa huduma za pembejeo bora za mifugo kwa gharama nafuu..


                                     HABARI KATIKA PICHA


Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Abdallah Hamis Ulega akinywa Maziwa yanayotengenezwa na Chama cha Ushirika wa Wafugaji Mufindi alipotembelea Kiwandani kwao wakati wa Ziara yake ya Kikazi Wilayani Mufindi.
 Mratibu wa kitovu chama cha wafugaji wilaya ya Mufindi (MUDCO) Bwana Ernest Haule akisoma taarifa ya ushirika kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Ulega.
Naibu Waziri Ulega akimpongeza Mratibu wa Kitovu (MUDCO) Bwana Ernest Haule kwa kuwasilisha vizuri taarifa ya chama cha wafugaji Mufindi. 

Mratiu wa Kitovu cha Ushirika wa Wafugaji Mufindi Bwana Ernest Haule wa kwanza Kushoto akishangilia baada ya Mhe Ulega kusifia Utamu na Ubora wa Maziwa ya (MUDCO)


Mhe Ulega akitoa maagizo kwa Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi (aliyevaa miwani) kuhakikisha  anatoa kipaumbele kwa ushirika huo katika kuwapatia mikopo inayotolewa na Serikali kwa akina mama na vijana ili kuchochoea maendeleo na mipango yao madhubuti kwa maendeleo ya Taifa

Naibu Waziri Mhe Ulega akisalimiana na Mbunge wa Mufindi Kusini Mhe Menrad Kigola (Picha na Amani Mbwaga)


Naibu Waziri Ulega akisalimiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya Mufindi Mara baada ya kuwasili katika Ofisi za Mkuu wa Wilaya.


Naibu Waziri Ulega akisalimiana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi 
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William akitoa Utambulisho kwa Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Ulega alipowasili Ofsini kwake tayari kwa kuanza ziara ya kikazi.
Naibu Waziri Mhe Ulega akisaini Kitabu cha Wageni Katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya Mufindi (Picha zote na Amani Mbwaga)

No comments:

Post a Comment