Na Amani Mbwaga, Mufindi
WAFANYABIASHARA Wilayani Mufindi wametakiwa kutumia kibiashara fursa ya mikopo inayodhaminiwa na Benki kuu ya Tanzania katika taasisi za kibenki ili waweze kufanya biashara zenye tija ikiwa ni pamoja na kumuunga mkono Rais Magufuli katika dhana yake ya Tanzania ya viwanda.
Hayo yamesemwa Wilayani humo na Ofisa mkuu mwandamizi wa Benki kuu ya Tanzania (BOT) Bwana Sadiki Nyanzowa wakati akitoa mada ya Elimu kuhusu uwekezaji katika masoko ya fedha (Government Securities) kwa wafanyabiashara wilayani humo na kusema kuwa lengo la Benki kuu kudhamini ni kutaka wafanyabiashara na wajasiliamali waweze kukua na Kukopesheka ili waweze kuboresha biashara zao.
Alisema kuwa Serikali kwa kushirikiana na Benki kuu ilianzisha mfuko wa udhamini wa mikopo midogo na ya kati ili kukuza na kuendeleza miradi hiyo na kujenga mazingira ya kuwawezesha wajasiliamali wenye miaradi midogo kupata mitaji na kuongeza ukuzaji wa uchumi.
”Mfuko huu unalenga wajasiliamali wenye miradi midogo na ya kati yenye mitaji yakifedha kati ya Milioni 5 hadi milioni 500,ambapo aombaji wanaweza kutumia mfuko huu wa kudhamini kupitia mabenki na taasisi za kifedha zilizosajliwa chini ya Sheria ya mabenki na Taasisi za fedha ya mwaka 2006”. Alisema
Alisema kuwa kuna sababu mbalimbali zinazozuwia wananchi kunufaika na fursa hii ikiwa ni pamoja na utayari mdogo wa taasisi za fedha kutoa huduma ya mikopo kwa wakopaji wanaoanza biashara kwa mara ya kwanza kwa sababu ya kukosa uzoefu.
Aiitaja sababu nyingine kuwa wakopaji wadogowadogo kutokuwa na uwezo wa kuandaa mchanganuo wa biashara unaokubalika na tasisi za kifedha.
Kwa upande wake Meneja wa Utawala wa Fedha Benki kuu tawi la Mbeya Bakari Ally akizungumza alisema kuwa Mafinga kuna fursa kubwa ya viwanda lakini bado wananchi na wafanyabiashara hawajapiga hatua kiuchumi hii ni kutokana na mitaji midogo.
Ally alisema kama anavyosema Mhe Rais Magufuli anataka wananchi wake wawe na raha kutokanana na furs zote zinazopelekea kubadilisha maisha yao, hivyo kupitia Benki kuu ipo kuwasaidia wananchi katika kufikia dhana ya uchumi wa viwanda kwa kusaidia kuongeza dhamana ya mikopo wanayoitaka katika mabenki.
”Sisi tumekuja Mafinga kwa Lengo la kuleta elimu hii ya dhamana ya serikali tukiona pia ni chagizo la kufanya wananchi waweze kuona fursa mbalimbali ambazo zipo sanjari na kuangalia namna bora ya kuwekeza katika biashara zetu ili mitaji iweze kupanuka na kufanya biashara zenye tija kwa manufa yetu na Taifa kwa ujumla” alisema Bwana Ally.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bwana Isaya Mbenje akifungua kikao hicho aliwataka wafanyabiashara kutumia kikao hicho kama fursa muhimu wa kujifunza namna ya kupiga hatua katika uwekezaji.
Aidha mmoja wa washiriki wa semina hiyo Bwana Henry Mangenya ambae pia ni Mwenyekiti wa TCCIA Wilaya Mufindi ameishukuru benki kuu kwa kuleta elimu hiyo ya kuhusu uwekezaji katika masoko ya fedha kwani wengi wao walikua hawajaipata ipasavyo kwani walikuwa na dhana ya uwekezaji kwenye masoko ni matajiri wakubwa tu lakini kumbe hata watu wa kawaida wanaweza kuwekeza aidha ameiomba benki kuu kuendelea kutoa eimu hiyo nchi nzima.
Chimbuko la mifuko ya udhamini wa mikopo inayosimamiwa na benki kuu ilifanya mageuzi katika sekta ya fedha ya mwaka 1991 na kujenga mazingira bora ya soko huria na kuboresha huduma za kifedha nchini, hata hivyo upatikanaji wa mikopo hasa kwenye sekta ya kilimo na kwa wajasiriamali wadogo na wa kati (SME) ilibaki kama changamoto.
HABARI PICHA
Meneja Utawala wa Fedha Benki kuu tawi la Mbeya Bwana Bakari Ally akizungumza na wafanyabiashara na wajasiriamali wa Wilaya ya Mufindi |
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Isaya Mbenje akifungua rasmi semina hiyo inayoendeshwa na BOT Katika ukumbi wa Halmshauri ya (W) Mufindi |
Baadhi ya Wafanyabiashara na Wajasiriamali wakifuatialia kwa makini semina inayotolewa na Benki Kuu BOT |
Ofisa Mkuu mwandamizi wa Benki kuu ya Tanzania (BOT) Bwana Sadiki Nyanzowa akitoa mada ya Elimu kuhusu uwekezaji katika masoko ya fedha (Government Securities) Wiayani Mufindi. |
No comments:
Post a Comment