Wednesday, December 19, 2018

Halmashauri ya Wilaya Mufindi Yatekeleza Kwa Vitendo Agizo la Waziri wa Mifugo na Uvuvi

Na Amani Mbwaga, Mufindi.
Baadhi ya Viongozi wa Majosho wakiwa katika picha na Kaimu Mkurugenzi
Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Imetekeleza agizo la Waziri wa Mifugo na uvuvi Mhe Luhaga Mpina aliloitoa Disemba 16 akiwa Wilayani Chato Mkoani Geita kuzindua kampeni ya Uogeshaji Mifugo ambapo aliziagiza Halmashauri kote nchini kutekeleza agizo hilo.

Agizo hilo ni kuhusu ugawaji wa dawa za ruzuku kutoka serikalini na kuogeshea mifugo bure kwa wafugaji wote ndani ya miezi 6 katika majasho kote nchini na Mufindi ikiwemo ambapo takribani maboksi 36 ambapo kila boksi lina makopo ya dawa 6 yenye lita 1 na lingine nusu lita Maboksi yamegawiwa bure yakiwa na  dawa aina ya Paranex ambapo inakadiriwa karibu majosho yote yanaujazo wa maji tkribani Lita 1200 hivyo dawa hizo zinatosha kwa josho moja.

Akigawa dawa hizo mgeni rasmi wa shughuli hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Isaya Mbenje amewaasa wafugaji kufuga kisasa na kwa ubora unaotakiwa na ndio maana serikali imeamua kutoa ruzuku ya asilimia 100 kwa dawa hizo ili kusaidia wafugaji kuogesha mifugo yao.

“Dawa hii ikawe kichocheo kwa wafugaji kuogesha mifugo yao na baadae sisi kama wafugaji lazima tuone namna ya kuendeleza majosho yetu na ni lazima mhakikishe mifugo yenu inaogeshwa kwa ratiba kama mlivyojwekea, Ndugu zangu serikali inasisitiza kuogesha mifugo ili kupunguza gharama za kutibu mifugo hiyo na pale inapopatwa na magonjwa yatokanayo na kutoogeshwa”. Alisema Bwana Mbenje

Aidha ameagiza serikali za vijiji kuanza kutunga sheria ndogo za vijiji kuhusu uogeshaji kama kijiji hakina sheria ndogondogo basi watendaji wa vijiji wameagizwa kuhakikisha wanatunga sheria hizo za kumtaka kila mwenye mifugo analazimishwa kuogesha na kama hataki basi sheria kali zichukuliwe dhidi yake.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Elias Jamvia alisema kama walivyosikia katika vyombo vya habari mbalimbali kwamba serikali imetoa dawa ya ruzuku ya kuogesha mifugo kwa asilimia 100 nchi nzima ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya Mufindi

Alibainisha kwamba idara yake inafanya kazi kwa kufuata miongozo, sheria na kanuni mfano leo hii wanasheria ndogo za Halmashauri zinazomtaka mtu asipoogesha wala kuchanja mifugo yake basi anatozwa faini ya shilingi 3000,000 au kifungo cha miezi 12 au vyote kwa pamoja.
“Wito wangu dawa hii iende ikafanye kazi iliyokusudiwa na serikali na si vinginevyo lakini pia majosho hayo yakawe endelevu Alisema Bwana Jamvia.

Kwa mujibu wa maelekezo toka Wizarani mfugaji ataogesha kwa muda wa miezi 6 bure lakini baada ya hapo ataanza kuchangia kidogo ili kupata fedha ya kununulia dawa ili majosho yawe endelevu.
Aidha Daktari wa Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Robert Semaganga alisema kwa sasa Halmashari hiyo inakabiliwa na magonjwa ya kupe ukiacha yale ya kuambukiza kama vile homa ya mapafu na chambavu lakini pia kuna tatizo la minyoo.

Halmashauri kupitia idara ya Mifugo na uvuvi ina mpango mkakati wa kuhakikisha mifugo yote inachanjwa na kukomesha kabisa magonjwa hayo  lakini pia kuna ratiba za chanjo kwa mwaka mzima.

“Rais wetu ameamua kutoa dawa hizi bure mnaona jinsi gani serikali yetu inavyotujali sisi wafugaji hivyo dhamana yetu ni kutekeleza na kufanya yale ambayo waziri ametuagiza na amesema atatembelea majosho hayo kujionea utekelezaji wa agizo lake” alisema Bwana Semaganga.

Kwa mujibu wa Muongozo wa matumizi ya dawa za uogeshaji unawataka viongozi wa serikali ya kijii kusimamia sheria na kuwachukulia hatua wasiofuata, lakini pia kupokea na kutathimini taarifa ya uendeshaji wa josho kulingana na kanuni za katiba ya kikundi.

Kamati ya uendeshaji Majosho nayo ina kazi ya kuhamasisha wafugaji na kuhimiza uogeshaji, kuweka utaratibu wa kuendesha na kusimamia uogeshaji, kukusanya pesa zitokanazo na uogeshaji na kuziwasilisha benki na hatimae kutoa taarifa katika Idara ya Mifugo aidha Afisa ugani atakuwa msimamizi wa josho na kutoa ushauri kwa kamati.

Uzinduzi rasmi wa uogeshaji bure utazinduliwa hivi karibuni katika kata ya sadani na hafla hiyo ya ugawaji dawa bure ulihudhuriwa na Viongozi wote wa majosho 36 yaliyopo katika Halmahsuari ya Wilaya Mufindi wakimwemo wenyeviti, makatibu watunza hazina, wenyeviti wa vijiji na maafisa ugani wa kata zote.





HABARI PICHA


























Picha zote na Amani Mbwaga

No comments:

Post a Comment