Na Amani Mbwaga,
Mufindi.
|
Baadhi ya Viongozi wa Majosho wakiwa katika picha na Kaimu Mkurugenzi |
Halmashauri ya
Wilaya ya Mufindi Imetekeleza agizo la Waziri wa Mifugo na uvuvi Mhe Luhaga
Mpina aliloitoa Disemba 16 akiwa Wilayani Chato Mkoani Geita kuzindua kampeni
ya Uogeshaji Mifugo ambapo aliziagiza Halmashauri kote nchini kutekeleza agizo
hilo.
Agizo hilo ni kuhusu
ugawaji wa dawa za ruzuku kutoka serikalini na kuogeshea mifugo bure kwa
wafugaji wote ndani ya miezi 6 katika majasho kote nchini na Mufindi ikiwemo
ambapo takribani maboksi 36 ambapo kila boksi lina makopo ya dawa 6 yenye lita
1 na lingine nusu lita Maboksi yamegawiwa bure yakiwa na dawa aina ya Paranex ambapo inakadiriwa karibu
majosho yote yanaujazo wa maji tkribani Lita 1200 hivyo dawa hizo zinatosha kwa
josho moja.
Akigawa dawa hizo
mgeni rasmi wa shughuli hiyo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi
Bwana Isaya Mbenje amewaasa wafugaji kufuga kisasa na kwa ubora unaotakiwa na
ndio maana serikali imeamua kutoa ruzuku ya asilimia 100 kwa dawa hizo ili
kusaidia wafugaji kuogesha mifugo yao.
“Dawa hii ikawe
kichocheo kwa wafugaji kuogesha mifugo yao na baadae sisi kama wafugaji lazima
tuone namna ya kuendeleza majosho yetu na ni lazima mhakikishe mifugo yenu
inaogeshwa kwa ratiba kama mlivyojwekea, Ndugu zangu serikali inasisitiza
kuogesha mifugo ili kupunguza gharama za kutibu mifugo hiyo na pale inapopatwa
na magonjwa yatokanayo na kutoogeshwa”. Alisema Bwana
Mbenje
Aidha ameagiza
serikali za vijiji kuanza kutunga sheria ndogo za vijiji kuhusu uogeshaji kama
kijiji hakina sheria ndogondogo basi watendaji wa vijiji wameagizwa kuhakikisha
wanatunga sheria hizo za kumtaka kila mwenye mifugo analazimishwa kuogesha na
kama hataki basi sheria kali zichukuliwe dhidi yake.
Kwa upande wake Mkuu
wa Idara ya Mifugo na Uvuvi Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Elias Jamvia
alisema kama walivyosikia katika vyombo vya habari mbalimbali kwamba serikali
imetoa dawa ya ruzuku ya kuogesha mifugo kwa asilimia 100 nchi nzima ni pamoja
na Halmashauri ya Wilaya Mufindi
Alibainisha kwamba
idara yake inafanya kazi kwa kufuata miongozo, sheria na kanuni mfano leo hii
wanasheria ndogo za Halmashauri zinazomtaka mtu asipoogesha wala kuchanja
mifugo yake basi anatozwa faini ya shilingi 3000,000 au kifungo cha miezi 12 au
vyote kwa pamoja.
“Wito wangu dawa hii
iende ikafanye kazi iliyokusudiwa na serikali na si vinginevyo lakini pia
majosho hayo yakawe endelevu Alisema Bwana Jamvia.
Kwa mujibu wa maelekezo
toka Wizarani mfugaji ataogesha kwa muda wa miezi 6 bure lakini baada ya hapo
ataanza kuchangia kidogo ili kupata fedha ya kununulia dawa ili majosho yawe
endelevu.
Aidha Daktari wa
Mifugo wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Robert Semaganga alisema kwa sasa
Halmashari hiyo inakabiliwa na magonjwa ya kupe ukiacha yale ya kuambukiza kama
vile homa ya mapafu na chambavu lakini pia kuna tatizo la minyoo.
Halmashauri kupitia
idara ya Mifugo na uvuvi ina mpango mkakati wa kuhakikisha mifugo yote
inachanjwa na kukomesha kabisa magonjwa hayo
lakini pia kuna ratiba za chanjo kwa mwaka mzima.
“Rais wetu ameamua
kutoa dawa hizi bure mnaona jinsi gani serikali yetu inavyotujali sisi wafugaji
hivyo dhamana yetu ni kutekeleza na kufanya yale ambayo waziri ametuagiza na
amesema atatembelea majosho hayo kujionea utekelezaji wa agizo lake”
alisema Bwana Semaganga.
Kwa mujibu wa
Muongozo wa matumizi ya dawa za uogeshaji unawataka viongozi wa serikali ya
kijii kusimamia sheria na kuwachukulia hatua wasiofuata, lakini pia kupokea na
kutathimini taarifa ya uendeshaji wa josho kulingana na kanuni za katiba ya
kikundi.
Kamati ya uendeshaji
Majosho nayo ina kazi ya kuhamasisha wafugaji na kuhimiza uogeshaji, kuweka
utaratibu wa kuendesha na kusimamia uogeshaji, kukusanya pesa zitokanazo na
uogeshaji na kuziwasilisha benki na hatimae kutoa taarifa katika Idara ya
Mifugo aidha Afisa ugani atakuwa msimamizi wa josho na kutoa ushauri kwa
kamati.
Uzinduzi rasmi wa uogeshaji bure utazinduliwa hivi karibuni katika kata ya sadani na hafla hiyo ya ugawaji dawa bure ulihudhuriwa na Viongozi wote wa majosho 36 yaliyopo katika Halmahsuari ya Wilaya Mufindi wakimwemo wenyeviti, makatibu watunza hazina, wenyeviti wa vijiji na maafisa ugani wa kata zote.
HABARI PICHA
|
Picha zote na Amani Mbwaga |