Tuesday, September 4, 2018

DC Mufindi Afunga Kiwanda cha Wachina kwa siku 14

Mkuu wa Wilaya Mufindi akitoa tamko la kukifunga kiwanda cha Wachina cha Evergreen kwa Siku 14 Mafinga Mjini

Na Amani Mbwaga Mafinga- Iringa.
Ni baada ya mauaji ya mfanyakazi mmoja wa kiwanda hicho kuuwawa kutokana na kipigo kutoka kwa walinzi wawili ambao ni wamasai na Mchina mmoja katika eneo la Kinyanambo Mafinga Mjini, Wilayani Mufindi Mkoani Iringa.

Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri David William leo amefunga kiwanda cha Wachina kijulikanacho kama Evergreen kinachozalisha Siling Bodi kwa muda wa siku 14 kutokana na Kifo cha Mfanyakazi wa kiwanda hicho lakini pia kutokidhi kwa viwango vya ubora wa afya, mazingira na usalama kazini.

Mnamo tarehe 23 Agosti 2018 Marehemu bwana Omari Ibrahim Chokai aliyekuwa mfanyakazi wa kiwanda hicho cha Evergreen alifariki dunia baada ya kupokea kipigo hadi kufariki kutoka kwa Walinzi wa kampuni hiyo ambao mpaka sasa wanashikiliwa na Jeshi la  Polisi katika kituo cha Polisi Mafinga kwa ajili ya upelelezi zaidi wa tukio hilo.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu inasemekana kwamba siku ya tukio Marehemu na wenzake walikua wakifanya service ya baadhi ya mashine ikiwemo kubadilisha oil ndipo marehemu alijaribu kuondoka na oil chafu na hapo ndio walinzi walimwita mwizi kwa kushirikiana na Mchina Mmoja kumpiga hadi mauti yalipomkuta huku wakifahamu fika kama marehemu huyo ni mfanyakazi wa kampuni hiyo.

Mmoja wa ndugu wa marehemu Bwana Selemani Boke aliwaambia waandishi wa habari kwamba baada ya kifo cha ndugu yao tarehe 24 Agosti 2018 walisafirisha mwili wa marehemu hadi Kondoa Irangi na kuuzika, baadae walienda polisi ili kufahamu kwa kina kuhusu kifo cha ndugu yao ili kuhakikisha kwamba haki inatendeka.

Bwana Boke alisema familiya imetumia zaidi ya Tsh Milioni 3 na laki 5 lakini uongozi wa kiwanda haujafanya lolote na kila walipokuwa wakiomba ushirikiano hawakupatiwa hata kidogo ndipo walipoamua kuandika barua kwa Mkuu wa Wilaya mufindi ili kuona jinsi gani anawasaidia ili haki yao ipatikane.

Mkuu wa Wilaya Mufindi baada ya kupata malalamiko hayo alianza kuyafanyia kazi na leo hii alifika kiwandani hapo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya.

Lakini pia alikuwa na  wataalamu mbalimbali kutoka NEMC, OSHA, Afisa Kazi Mkoa, Katibu wa Chama cha Wafanyakazi TUICO Mkoa wa Iringa na wataalamu wengine kutoka Halmashauri ya Mji Mafinga ambao walifanya ukaguzi wa kiwanda na kutoridhika na mazingira ya kiwanda hasa usalama kwa wafanyakazi na mazingira kutokuwa rafiki.

“Kwa kuzingatia sheria zote za kazi, usalama kazini na sheria ya mazingira kama wataalamu hawa walivyokwishafanya, Mimi Mkuu wa Wilaya Mufindi natamka na ninasema kiwanda kinasimama na nakifunga kwa siku 14 wawe wamerekebisha mapungufu yote yaliyoainishwa na wataalamu na pia ndani ya siku hizo wawe wamelipa gharama zote za kumsafirisha marehemu mpaka kwao Kondoa Irangi zinazofikia Milioni 3 na Laki 5”. Alisema Mhe Jamhuri.

Mkuu huyo wa Wilaya alisema kwa uchungu wasipotekeleza hayo waje hapa wang’oe mitambo yao na kuirudisha china, ni afadhali tubaki na unyonge wetu kuliko kunyanyaswa ndani ya nchi yetu iliyokwishapata uhuru haiwezekani.

Wakikamilisha yote hayo wafanyakazi wote wamehakikishiwa kurudi kazini na asisikie mtumishi hata mmoja anakatwa jina lake wote ni lazima warudi, “Ili mbegu iote ni lazima kwanza ife ndio inamea vizuri sasa tumeamua kufa kwa ajili ya maslahi mazuri mbele ya safari” Alisisitiza Mhe Jamhuri.

Alimaliza kwa kuwataka wafanyakazi kuchukua tamko hilo kama ni hatua nzuri ya kurekebisha hali ya kazi ili baada ya siku 14 mambo yawe mazuri.

Kwa upande wake Mratibu wa NEMC Nyanda za Juu Kusini Bwana Goodlove Mwamsojo alisema toka wamekipa kiwanda hicho cheti cha mazingira kwa ajili ya kuendesha shuguli zake hawajatekeleza shariti hata moja.

Hivyo kwa mujibu wa sheria ya mazingira ya mwaka 2004 mazingira ya kiwanda ni hatarishi, hawa  watu wanatishia usalama na afya za wafanyakazi hivyo wamestahili kupigwa faini ambayo haitapungua wala kuzidi Tsh Milioni 50.

“Sisi tutaendelea kufanya kazi wa mujibu wa sheria ya mazingira na kama kweli wana nia ya kuendeleza uchumi wa nchi hii ni lazima wajali afya za Watanzania” alisema Bwana Mwamsojo.

Kwa upande mwingine Msimamizi wa Ofisi ya Wakala wa usalama na Afya Ofisi ya Kanda nyanda za juu kusini Mbeya Injinia Faston Uswege alisema sisi kama OSHA tunasimamia sheria namba 5 ya mwaka 2005 ya uslama kazini.

“Watu wa OSHA Walipita mwezi wa 12 mwaka jana na wakatoa maelekezo ikiwemo kuwapatia vitendea kazi nya kiusalama na mpaka sasa halijatekelezwa” alisema Bwana Uswege.

Lakini pia suala la vyoo, kulingana na idadi ya wafanyakazi karibu 400 kutumia idadi ya matundu yaliyopo haiwezekani lakini pia vyoo havina hadhi ya kwenda kujisaidia na pia suala la maji ya kunywa yanayotumika hapa si safi na salama lakini mwajiri hajali hata kidogo.

Hatua imechukuliwa na OSHA kukitoza kiwanda hicho faini isiyopungua wala kuzidi Tsh Milioni 17 lakini pia ametakiwa atoe vitendea kazi kwa wafanyakazi wote ndani ya siku 14 alizopewa.

Aidha Afisa kazi Mkoa wa Iringa Bwana Daudi Samweli alisema kiwanda kimekuwa na manyanyaso na hakuna uongozi unaoeleweka kila mchina anayekuja ni Bosi.

“Kwa kufuata matakwa ya sheria ya kazi na miongozo mbalimbali ya kisera sisi tunawafikisha mahakamani viongozi wa kiwanda hiki ili watekeleze mambo tunayowaambia kila siku lakini pia wafanyakazi wenyewe hawana mikataba na hawataki kutoa, sasa hatutakubali kuona wafanyakazi wananyanyasika kwa namna yoyote ile" alisema Bwana Samweli.

Katibu wa chama cha wafanyakazi TUICO Mkoa wa Iringa  na Njombe Bwana Karim Bachalla kwa upande wake alisisitiza kwamba Wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi hii lakini pia nao wawekezaji wafanye kazi kwa kufuata sheria taratibu na matakwa ya nchi.  

HABARI PICHA
Mkuu wa Wilaya Mufindi (Katikati )akitoa maelekezo kwa Wachina Kushoto kwake ni Katibu wa TUICO Mkoa wa Iringa na Njombe Bwana Karim Bachalla 

Ukaguzi wa Kiwanda Ukiendelea

Mitambo ndani ya Kiwanda cha Evergreen

Wafanyakazi wakiendelea na kazi wakati wa ukaguzi



Majadiliano ya Wataalamu Mbalimbali wakiwa katika Ukaguzi wa Kiwanda cha Evergreen



Mratibu wa NEMC Nyanda za Juu Kusini Bwana Goodlove Mwamsojo (Kulia) akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya Mufindi baada ya kumaliza ukaguzi wa kiwanda


Msimamizi wa Ofisi ya Wakala wa Usalama na Afya OSHA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini Mbeya  Injinia Faston Uswege akitoa mrejesho ya walichokiona baada ya kufanya ukaguzi ndani ya kiwanda cha Evergreen Mafinga Mjini.

Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William Akiongea na Wafanyakazi na Wamiliki wa Kiwanda cha Evergreen kuelezea nia ya Kukifunga kutokana na kutokidhi vigezo.


Injinia Faston Uswege Kutoka OSHA Nyanda za Juu Kusini akitoa Tamko la Kukitoza Faini kiwanda cha evergreen kwa kwenda kinyume na sheria  na taratibu za Afya Mazingira na Usalama Kazini.



Afisa Kazi Mkoa wa Iringa Bwana Daud Samweli nae akieleza alichokibaini na hatua zitakazochukuliwa


Katibu wa chama cha wafanyakazi TUICO Mkoa wa Iringa  na Njombe Bwana Karim Bachalla kwa upande wake akisisitiza kwamba Wafanyakazi wanatakiwa kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi
Baadhi ya Wachina na Wafanyakazi wa Kiwanda hicho wakisikiliza kwa makini maelekezo ya serikali (Picha zote na Amani Mbwaga)
Kwa Maoni au Ushauri Wasiliana nasi:
Mob:+255 656 632 566
E-mail:prof.mbwaga@gmail.com

Saturday, September 1, 2018

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mgumba afanya ziara Kiwanda cha chai Kilima- Uniliver Mufindi

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba wa pili Kushoto akipata maelezo kutoka kwa Meneja Mkuu wa Kiwanda cha kuchakata chai cha Kilima aliyevaa kofia ya kijani Bwana Abdallah Hamad katika Maabara ya kupima ubora wa chai  kiwanda hicho kipo chini ya Kampuni ya chai ya UNILEVER TEA TANZANIA LIMITED (Picha na Amani Mbwaga).

Na Amani Mbwaga, Mufindi- Iringa.

Naibu waziri wa kilimo Mhe Omary Mgumba amefanya ziara ya kutembelea kiwanda cha kuchakata chai Kilima kilichopo chini ya Kampuni ya uzalishaji chai Tanzania (Unilever Tea Tanzania Limited) wilayani Mufindi Mkoani Iringa.

Katika ziara hiyo ameridhishwa na juhudi zinazofanywa na kampuni hiyo za kuendelea kuzalisha chai zaidi na yenye ubora wa hali ya juu kwa kutumia mitambo ya kisasa na pia katika ulimaji wa chai ambapo pia wanatumia umwagiliaji wa mitambo ya kisasa.

Lengo la ziara ya Mhe Naibu Waziri ni kuona shughuli za kilimo cha chai jinsi zinavyofanyika katika wilaya ya mufindi, kukutana na wakulima wa chai na wawekezaji kujua wanafursa gani changamoto gani na wana mikakati gani ya kusonga mbele na kupanua masoko.

“Najua changamoto kubwa katika zao hili ni soko na hasa ukizingatia soko kuu liko Kenya, hivyo ni lazima tuwe na chai bora ili kushindana na chai ya kenya na ya nchi nyingine, lakini pia watu wa utafiti na vyuo vyetu ni lazima vitusaidie kupunguza gharama za uzalishaji ili kupata chai yenye ubora na itakayomnufaisha mkulima” alisema Mhe Mgumba.

Aidha serikali ina mpango wa kufungua soko lake la chai hapa nchini ili kuwavutia wanunuzi ikiwa ni pamoja na kuitangaza nchi lakini pia kuwasaidia wakulima kuuza chai yao kwa tija.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William alisema anajivunia uwepo wa Kampuni ya chai Uniliver katika wilaya yake kwani inamchango mkubwa sana katika wilaya na jamii inyozunguka kampuni hiyo yenye mashamba ya chai na viwanda.

“Uwepo huu unawanufaisha wananchi wa mufindi kwa kupata fursa za ajira lakini pia ni walipaji wazuri wa kodi inayochangia maendeleo ya uchumi wa wilaya na nchi kwa ujumla” alisema Mhe William.

Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya chai Tanzania UNILEVER Bwana Ashton Eastman alimshukuru Mhe Naibu waziri kwa ujio wake na kumweleza baadhi ya mafanikio ikiwemo kuwa na Bwawa kubwa la maji kwa ajili ya umwagiliaji wa chai, uzalishaji wa zao la chai bora, uendeshaji wa viwanda vya kuchakata chai kabla haijaenda sokoni na hivyo kuendana na sera ya viwanda ya nchi.

Aidha alitoa changamoto zinazokabili kampuni hiyo hasa ya ardhi na ubora wa chai kuwa mdogo kutoka kwa wakulima wadogowadogo hali inayopelekea wakulima hao kutonufaika vizuri na kilimo cha chai kisha kupelekea kuhamia shughuli zingine mbali na kilimo hicho.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bwana Theophord Ndunguru alisema changamoto ya bei ya chai ni kubwa kwani huwa inapanda na kushuka kulinganisha na bei ya sokoni.

“Kabla ya mwaka 2011 tulikuwa hatuna mfumo rasmi wa upangaji bei ya majani mabichi ya chai kwa hiyo majadiliano yalikuwa yanakuwa magumu sana, kuanzia mwaka 2012 wadau wa chai na bodi ya chai tuliandaa mfumo rasmi wa kuandaa bei elekezi kwa ajili ya majani ya chai” alisema Bwana Ndunguru.

Ule mfumo umewekwa kwa uwiano ambao majani mabichi ya chai huangaliwa gharama halisi za uzalishaji wa chai za mkulima mdogo, kilo moja ya chai na gharama za mwenye kiwanda katika namna ya kusindika na masoko kisha kupata uwiano.

Akijibu changamoto ya bei za wakulima wanapopeleka chai kiwandani Meneja wa fedha wa UNILEVER Bwana Eliya Jonas alisema “sisi kama Uniliver tunalipa zaidi ya bei ya serikali iliyopangwa, tunalipa Tsh 314 halafu 87 unakuwa na 417 vilevile tunalipa motisha ya ubora wa chai ambayo inaenda kwa Tsh 87 mpaka 125”

Kwa mwaka wa fedha uliopita Unilver ililipa  bei kati ya Tsh 411 hadi 523 kwa mkuima wa chai na kuthibitisha hili walitambulika  mwaka jana na kikao cha wadau wa chai na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa bodi ya chai amethibitisha hili, waliibuka washindi  kwa kuwa  walipaji bora wa chai Tanzania na kupata tuzo ya heshima.





Mkurugenzi Mkuu wa Unilever Njombe  Bwana Allawi Mdee wa pili kulia akitoa maelezo ya awali kwa Waziri wa Kilimo  Mhe Omary Mgumba wa kwanza kushoto  kabla ya kuanza kutembelea miradi ya  kampuni hiyo ya Mufindi .


Mkurugenzi mkuu wa Unilever Tanzania Bwana Ashton Eastman wa kwanza kushoto akitoa maelezo ya mashamba ya chai yanayolimwa kwa njia ya umwagiliaji Kwa Naibu Waziri Mhe Mgumba  katika eneo la Ngwazi Wilayani Mufindi


Naibu Waziri wa Kilimo akiendelea kupata maelezo ya kilimo cha chai kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa Unilever Tanzania





Mkurugenzi Mkuu wa Unilever Tanzania Bwana Ashton Eastman akimuonesha Naibu waziri Ramani ya eneo wanalomiliki ikiwemo Mashamba ya chai Viwanda pamoja na maeneo mengine ya Michezo na Burudani Kulia ni Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William.


Meneja Mkuu wa Kiwanda cha Kuchakata chai cha Kilima Bwana Abdallah Hamad Kulia akimkaribisha Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mgumba katika kiwanda hicho.

Bwana Hamad akisalimiana na Msaidizi wa Naibu Waziri Bwana Shija


Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akisaini kitabu cha wageni katiak ofisi ya Meneja mkuu wa Kiwanda cha kuchakata chai cha Kilima

Naibu waziri wa Kilimo Mhe Mgumba wa Pili Kulia kushoto kwake ni  Mkurugenzi Mkuu wa Unilever Tanzania Bwana Ashton Eastman, Kulia kwake ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bwana Ndunguru na anaefuatia ni Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William Wakiwa katika Vifaa maalumu tayari kwa kutembelea zoezi zima la uchakataji wa chai ndani ya kiwanda



Bi Rebeka Mamuya Meneja Kiwand a cha Kibwela akitoa maelezo kwa Naibu waziri na wageni wengine ndani ya kiwanda  jinsi chai inavyopitia mchakato wake katika hatua mbalimbali kuanzia inavyoingia kiwandani hadi bidhaa ya mwisho inavyopatikana. 


Maelezo kwa Naibu Waziri yakiendelea
Baadhi ya Mitambao ndani ya Kiwanda






Bidhaa ya Chai iliyokwisha chakatwa tayari kupelekwa Sokoni


Naibu waziri Mhe Mgumba akipokea maelezo kutoka kwa Meneja  Mkuu wa Kiwanda cha Kilima katika Maabara ya Kupima ubora wa chai inayozalishwa na kuipanga katika makundi tofautitofauti klingana na ubora wake kabla ya kwenda Sokoni


Naibu Waziri katikati akiuliza baadhi ya maswali kuhusu upimaji wa chai bora




Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bwana Theophord Ndunguru wa Kwanza Kushoto akimweleza Naibu Waziri wa Kiimo njia nyingine inayotumika kupima ubora wa chai kuwa ni kupitia rangi zake.

Mkurugenzi Mkuu wa  Kiwanda cha Kilima Bwana Abdallah Hamad Kushoto akimuonesha Naibu waziri Matokeo ya Vipimo walivyokuwa wanafanya na kujua chai ipi unaubora zaidi na kisha kuzipanga kulingana na ubora wake unaotokana na matokeo ya Maabara baada ya vipimo 

Hili ni eneo lijulikanao kama Boiler ndio chanzo cha joto lanapozalishwa kwa njia ya kuni kwa ajili ya kwenda kukaushia chai inapotoka mashambani.




Mkurugenzi Mkuu wa Unilever Njombe Bwana Allawi Mdee wa Kwanza kulia akiwa na Naibu Waziri, Mkurugenzi Mkuu wa Unilever Tanzania Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bwana Ndunguru.



Naibu waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba akipokea Majani ya chai Grade 1 toka kwa Mkurugenzi Mtendaji mkuu wa Unilever Tanzania yanayozalishwa kiwandani hapo ili kwenda kuijionea ubora wa bidhaa hiyo.

Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhri William nae akipokea Majani Hayo kutoka kwa Bwana Ashton Eastman Mkurugenzi Mkuu Unilever Tea Tanzania Ltd.


Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bwana Ndunguru nae akipokea

Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Mgumba akiwa katika picha ya pamoja na Wafanyakazi wa Kiwanda cha chai Kilima pamoja na viongozi wengine waandamizi wa serikali na wa bodi ya Chai Tanzania (Picha zote na Amani Mbwaga)

Kwa Maoni au Ushauri Wasiliana nasi:
Amani Mbwaga
Mob: +255 656 632 566
E-mail:prof.mbwaga@gmail.com