Serikali imetangaza kuwa haitawaruhusu wahitimu wa elimu ya juu wanaodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwenda nje ya nchi kwa masomo zaidi au kufanya kazi mpaka watakapomaliza kulipa madeni yao.
Akizungumza bungeni hivi karibuni, Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Jenista Mhagama alisema hatua hiyo inalenga kuongeza kiwango cha ukusanyaji wa mikopo ambayo imeshawanufaisha wahitimu wengi ingawa ni wachache wanaorejesha.
"Tumezungumza na idara ya uhamiaji ili wale wote wanaotaka kwenda kufanya kazi nje ya nchi wasiruhusiwe mpaka watakapomaliza kulipa mikopo yao ya elimu ya juu. Lengo ni kuepuka ukwepaji unaojitokeza baada ya kuajiriwa," alisema.(Martha Magessa)
Suala la wahitimu wa Kitanzania kutafuta kazi nje ya nchi limekuwa likizungumzwa na wadau wengi kama njia mbadala ya kupata ajira, kutokana na kuwapo kwa ushindani mkubwa wa soko la ndani la ajira.
Wahitimu
Hata hivyo, baadhi ya wadau hawaoni manufaa endelevu ya mpango huo, wakisema chombo kinachohusika na mikopo hakijajipanga vilivyo kukusanya madeni na ndiyo maana kimeshindwa kuwafikia hata wadaiwa waliomo nchini.
Leonard Mhongole ni mhitimu wa Chuo Kikuu cha Ardhi mwaka 2010. Anasema mkakati huo hauwezi kuleta tija kwa kuwa ni watu wachache sana wanaofikiria kwenda nje ya nchi.
"Mamlaka husika zinaangalia sana waajiriwa wa serikalini lakini kwa wale tunaofanya kazi sekta binafsi au waliojiajiri hatufikiwi. Kama watu wote watabanwa kama inavyotakiwa nadhani fedha za kutosha zitarudi serikalini," anasema na kuongeza:
"Mimi binafsi nilitakiwa niwe nimeanza kulipa mkopo wangu lakini kwa kuwa hakuna anayenitaka kufanya hivyo siwezi kuwatafuta wahusika...inawezekana wametoa msamaha kwa baadhi ya watu."
Kwa upande wake, mwanafunzi wa shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Joseph Isindikiro, anasema utekelezaji wa mkakati huo ni ukiukwaji wa haki ya msingi ya mtu kupata elimu.
"Mpango huo hautawezekana kwa sababu serikali yenyewe imekiri kuwa kuna tatizo la ajira na kupendekeza wahitimu kuomba kazi nje ya nchi. Sasa itakuwaje wao wenyewe wazuie ilhali wanajua mhusika hana uwezo huo na ajira hiyo ndiyo tegemeo lake?" anahoji.
Anaongeza kusema kuwa kufanya hivyo ni sawa na kumtia mtu hatiani kutokana na haki yake ya kupata elimu kama inavyobainishwa katika Katiba.
CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment