Tuesday, July 4, 2017

Umeipata hii ya Ajira kumwagwa?


SERIKALI inatarajia kutoa vibali 3,000 vya ajira katika sekta ya afya, zikihusisha madaktari na wauguzi kwa ajili ya vituo vya afya vya kata ili kuboresha sekta hiyo, imeelezwa hapa jana.

Pia serikali imetangaza kuwa itatoa vibali vya ajira za maofisa hesabu 535 kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati nchini ili kushughulikia ipasavyo ukusanyaji wa mapato.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, ndiye aliyetangaza neema hiyo kwa wasomi wanaosubiri ajira serikalini wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu maadili na uwajibikaji mahali pa kazi.

Alisema vibali vya ajira hizo vitatolewa wiki ijayo huku akiwataka wafanyakazi hao kufanya kazi kwa kuzingatia sheria kanuni na taratibu ili kujenga utumishi wa umma wenye uadilifu.

"Naomba wanaoharibu wasihamishwe na kupelekwa maeneo mengine, wakifanya hivyo watakuwa wanaharibu utumishi wa umma, ufumbuzi ni kuchukua hatua palepale alipo," alisema Dk. Ndumbaro.

Aliongeza kuwa sekta zinatakiwa kujenga utamaduni wa kuwapongeza watumishi wa umma wanaofanya vizuri kwenye maeneo yao ya kazi ili wajitume zaidi na kuhamasisha wengine.

Katika kikao kazi hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara ambaye pia aliwahi kuwa Naibu Katibu Mkuu katika Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tamisemi, Eliakim Maswi, alisema vituo vingi vya afya vimefungwa kutokana na watumishi kuwa na vyeti vya kughushi hivyo vingi havina watumishi.

Alisema uhakiki wa vyeti feki bado haujamalizika, lakini akasisitiza kuwa ni muhimu kwa sasa serikali kutoa vibali vya ajira mpya kwa kuwa watumishi waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi ni wengi hivyo kuna haja ya kuziba pengo hilo.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Mpoki Ulisubisya alisema serikali itaendelea kuajiri watumishi katika sekta ya afya.

Katika ufafanuzi kuhusu ajira mpya zitakazotolewa wiki ijayo, Dk. Ulisubisya alisema kila mkoa utapata mgawo wa wataalamu hao watakaoungana na madaktari 258 ambao walisailiwa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi Kenya, lakini baadaye wakaajiriwa nchini.

Katika mwaka huu wa fedha, serikali imeahidi kutoa vibali vya ajira za moja kwa moja 52,436 katika sekta zake mbalimbali.

Aprili 19, kufuatia Mahakama ya Kenya kutoondoa pingamizi lililofunguliwa dhidi ya ajira za madaktari kutoka nchini walioombwa huko, Rais John Magufuli aliamua wataalamu 258 waliokuwa wamejitokeza kuchangamkia fursa hiyo waajiriwe na serikali.

Madaktari hao ndiyo waliokidhi vigezo vilivyotakiwa kwenda kufanya kazi nchini Kenya kati ya 496 waliokuwa wameomba.

Machi 18, ujumbe wa serikali ya Kenya ukiongozwa na Waziri wa Afya nchini humo, Dk. Cleopa Mailu ulikutana na Rais Magufuli na kuomba kuajiri kwa mkataba madaktari 500 ili kupunguza uhaba wa wataalamu hao wa afya uliotokana na mgomo nchini humo.

Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Muhammad Kambi alipapata kusema idadi ya madaktari wanaohitajika nchini ni 3,510 na katika idadi hiyo, mahitaji zaidi yapo kwenye hospitali za wilaya kunakokosekana madaktari 832, za rufani (460), vituo vya afya (816), Bugando (152) na Hospitali ya Taifa Muhimbili madaktari 235.

Nyingine ni KCMC (143), hospitali za rufani za mikoa (460), madaktari 111 katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI), Hospitali ya Ocean Road (57), Mirembe (37), CCBRT (26) na Rufani Mbeya (106).

Mei 3, Waziri Kivuli wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Godwin Mollel aliliambia Bunge kuwa uwiano kati ya madaktari na wagonjwa nchini kwa sasa si mzuri.

Akinukuu ripoti ya Madaktari Wenza wa Afrika (Africa Cuamm) ya mwaka jana, Dk. Mollel alisema asilimia 74 ya madaktari wanaishi mjini na daktari mmoja anahudumia wagonjwa 78,880 kwa maeneo ya vijijini, kinyume cha maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) linalotaka daktari mmoja ahudumie wagonjwa elfu moja (1:1,000).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotolewa Oktoba 2016, Tanzania ina upungufu wa asilimia 58.1 ya madaktari bingwa, wauguzi wa sekta ya umma II kwa asilimia 54.4, wataalamu wa miale kwa asilimia 50.8 na maofisa kliniki kwa asilimia 50.

Pia kuna upungufu wa madaktari wasaidizi na madaktari wasaidizi wa meno kwa asilimia 46.2, wafamasia kwa asilimia 49.9, mabwana afya kwa asilimia 45.7, mafundi sanifu wa maabara kwa asilimia 41.5, maofisa kliniki wasaidizi kwa asilimia 40.7 na madaktari kwa asilimia 37.3.

Wakati serikali ikishindwa kuajiri madaktari, Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Obadia Nyongela, aliiambia Nipashe mwishoni mwa mwaka jana kuwa kuna madaktari 1,700 mtaani ambao wana sifa, lakini hawajaajiriwa.

"Kama mwaka huu (2016) utaisha bila vibali vya ajira kutoka, maana yake mpaka mwakani (2017) kutakuwa na madaktari 2,866 wasio na ajira licha ya kuwapo kwa upungufu wa wataalamu hao," alisema Dk. Nyongela.

Chanzo Muungwana Blog.

Saturday, July 1, 2017

PUBLIC RELATIONS & MARKETING MANAGER'S: JKT Kuongeza Idadi ya Vijana Vikosini.

PUBLIC RELATIONS & MARKETING MANAGER'S: JKT Kuongeza Idadi ya Vijana Vikosini.: Mahafali ya Ufungaji wa Mafunzo ya Awali ya Kijeshi Oparesheni Magufuli Kujitolea Mafinga JKT, Tarehe 28 Juni, 2017 .                      ...

JKT Kuongeza Idadi ya Vijana Vikosini.

Mahafali ya Ufungaji wa Mafunzo ya Awali ya Kijeshi Oparesheni Magufuli Kujitolea Mafinga JKT, Tarehe 28 Juni, 2017.                                                                                                                                       
Vijana wa Mafinga JKT Wakitoka nje ya Uwanja mara baada ya kumaliza Gwaride la Kuhitimu Mafunzo yao ya awali ya Kijeshi Tarehe 28 Juni 2017


Mgeni Rasmi Mkuu wa wilaya ya Mufindi Jamhuri David William Akipokea Salamu ya Heshima Kutoka kwa Gwaride lililoandaliwa na Vijana wa Mafinga JKT Oparesheni Magufuli Kujitolea wakati wa Kuhitimu Mafunzo yao ya awali ya Kijeshi.
Na Amani Mbwaga                                                   
Mafinga, Tanzania.
Jeshi la kujenga Taifa JKT limejipanga kidete kuongeza idadi ya vijana wa Tanzania kujiunga na Mafunzo ya awali ya kijeshi, baada ya kufufua Vikosi na Makambi ya awali ya Jeshi hilo.

Hayo yamesemwa na Mwakilishi wa Mkuu wa JKT Luteni Kanali AS Kagombola ambaye  ni Mkurugenzi wa Ustawi wa Jamii JKT, alipokuwa akitoa salamu kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi hilo Meja Jenerali Michael Isamuhyo, wakati wa kufunga mafunzo ya awali ya kijeshi ya Kundi Magufuli katika Kikosi cha Mafinga JKT, Kilichopo wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.

Mkuu wa JKT amempongeza Mh Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kuona umuhimu wa vijana na  kufufua vikosi hivyo vya JKT.

Tarehe 15 Machi 1967 Kikosi cha Mafinga JKT Kilifunguliwa rasmi kikiwa na vijana wachache ambao walijiunga kufanya shughuli za kujenga Taifa.
Baadhi ya sababu za kuanzishwa kwa JKT ni Kubadili fikra za Vijana wa nchi hii kutoka ile hali ya ukoloni ya kutegemea nchi nyingine ili kuleta Maendeleo, Kuwafunza Vijana Kujenga Mshikamano na umoja wa kitaifa ili kulinda uhuru wa Taifa lao.

Pia ni kuwaunganisha vijana bila kujali itikadi zao, kujifunza uzalendo na stadi za maisha ili waweze kujiajiri na kujitegemea mara wamalizapo mkataba wao wa kujitolea kwa miaka miwili.

Luteni Kanali Kagombola alisema, “katika kutambua hilo Serikali imerejesha Makambi Matano (05) yaliyokuwa yamesitishwa kufanya mafunzo,  ili kuongeza zaidi uwezo wa Kuchukua Idadi kubwa ya Vijana” Makambi yaliyofunguliwa ni 826 KJ Mpwapwa Dodoma, 839 KJ Makuyuni Arusha, 845 KJ Itaka Songwe, 846 KJ Luwa Rukwa, 847 Milundikwa Rukwa, wakati huohuo Makuyuni Arusha tayari imeshaanza kuchukua vijana na sasa wanaendelea na mafunzo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe Jamhuri David William ambaye alikuwa Mgeni Rasmi na Kufunga Mafunzo hayo amewataka vijana kufanya kazi kwa bidii, Uhodari,Uadilifu  na Weledi wa hali ya juu mara wapatapo nafasi za ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama.

“Aidha kwa wale watakaomaliza mkataba wao wa JKT na kurudi nyumbani nawataka mkawe raia wema na kamwe msijiingize katika mambo ya uhalifu na ujambazi, bali mkashirikiane na jamii kwa yale mazuri mliyojifunza hapa Jeshini ili kuilinda nchi yetu na kuleta maendeleo kwa Taifa letu” alisema Mhe Jamhuri William.

Naye Mkuu wa Kikosi cha Mafinga JKT  Luteni Kanali Hamis Maiga aliwashukuru wahitimu wa kundi la Magufuli Kujitolea kwa kuwa na nidhamu kubwa wakati wote wa Mafunzo yao ya miezi sita.

Alisema Kikosi Kimepata vijana waadilifu wenye nidhamu na Ubunifu wa hali ya juu, kwani wametuachia Mashine ya Kusaga Nafaka na kupaki unga, Bwawa kubwa la Ufugaji wa Samaki  na mengine mengi.

Wito wake kwa vijana hawa wa JKT ni kutunza kiapo walichoapa cha Uhodari, Utii na Uaminifu, kwa lengo la kubadilisha changamoto zilizopo katika jamii na kuzibadili kuwa fursa.

Serikali ilirejesha Mafunzo ya JKT Kwa vijana wa Kujitolea mwaka 2001 baada ya kusitiswa mwaka 1994.
Oparesheni katika Mafunzo ya JKT zilizowahi kupita Toka 2001 ni:

Oparesheni Mkapa             2001
Ø Miaka 40 ya JKT                 2002
Ø Utandawazi                          2004
Ø Jiajiri                                    2005
Ø Kasi Mpya                             2006
Ø Maisha Bora                          2007
Ø Uadilifu                                  2008
Ø Kilimo Kwanza                      2009
Ø Uzalendo                                2010
Ø Miaka 50 ya Uhuru                2011
Ø Sensa                                      2012
Ø Miaka 50 ya JKT                    2013
Ø Miaka 50 ya Muungano          2014
Ø OP Kikwete                             2015
Ø OP Magufuli                            2016- Hadi Sasa.



                                      HABARI KATIKA PICHA.

Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Jamhuri David William akitoa hotuba  kwa Hadhira iliyohudhuria Mahafali ya Kuhitimu Mafunzo ya Awali Ya Kijeshi Katika Kikosi cha Jeshi  Mafinga
Mwakilishi wa  Mkuu a JKT Luteni Kanali AS Kagombola ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ustawi wa Jamii JKT akijiandaa kutoa Salamu za Mkuu wa JKT

Kamanda  Kikosi wa Kikosi cha Jeshi Mafinga Luteni Kanali Hamis Maiga akitoa wito kwa vijana waliomaliza mafunzo ya awali ya Kijeshi, Kundi la OP Magufuli Kujitolea.
Kamanda Kikosi Luteni Kanali Hamis Maiga akimtambulisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Prof:Riziki Shemdowe
Paredi Kamanda Kapteni  Bakari Namgugu Akimshukuru Mgeni Rasmi Mara baada ya Kumaliza Ukaguzi wa Gadi za Maonesho ya kwata ya Mwendo wa Pole Na Haraka, katika Mahafali ya Vijana  JKT Oparesheni Magufuli Kijitolea Katika Kikosi cha Jeshi Mafinga.











BrassBand ya Mafinga JKT Ikitulia wakati wa Ukaguzi wa Mgeni Rasmi Mkuu wa wilaya ya Mufindi wakati wa Mahafali ya Kumaliza Mafunzo ya awali ya Kijeshi Kikosini Hapo.

Gwaride likitoka nje ya Uwanja.


Baadhi ya Ndugu , Jamaa, Marafiki na Wananchi wa Mkoa wa Iringa Wakifuatilia Kwa Makini Sherehe  Za Kumaliza Mafunzo ya Awali ya Kijeshi Katika Kikosi Jeshi Mafinga.

Kikundi cha Singe


Kikundi cha Sarakasi cha Mafinga JKT








Mgeni Rasmi Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Katikati akiwa katika Picha Ya Pamoja na Wakuu   mbalimbali wa vikosi vya Jeshi waliosimama nyuma.
Mgeni Rasmi akiwa katika picha ya Pamoja na Kamati Tendaji ya Kikosi cha Jeshi Mafinga




Mgeni Ramsi akiwa Katika Picha Ya Pamoja Viongozi wa Serikali ya Vijana Op Magufuli


Bwawa la Ufugaji wa Samaki la Kikosi cha Jeshi Mafinga Unaosimamiwa na Vijana wa Kujitolea  Mafinga JKT

Vijana wa JKT Mafinga (SM) Oparesheni Magufuli wakilisha Samaki Chakula

Kijana wa JKT (SM) Oparesheni Magufuli akiwapa elimu ya Ufugaji wa Samaki Wazalendo wa Mujibu waSheria waliomaliza Kidato cha Sita Mwaka Huu.


Jengo la Kiwanda Kidogo cha Kusaga nafaka na Kupaki Unga Bora Cha Mafinga JKT.

Kwa Mawasiliano Zaidi.
Mob: + 255 656 632 566
           :+  255 765 058 711
Twiter:@amanmbwaga






Monday, December 8, 2014

Tuhakikishe washenzi wote hawarudi madarakani, Uchaguzi Serikali za Mitaa Na Uchaguzi Mkuu 2015: By Denis Mpagaze.


Pale Pombe, tisheti na kofia vinapotuchagulia viongozi, chamoto tunakipata!
Denis Mpagaze
Tunaingia kipipndi cha uchaguzi. Tutaskia mengi. Lakini kubwa zaidi ni zawadi au tuseme takrima. Zawadi zenye kila aina ya sura ya mkono mtupu haulambwi au nipe niupe au muosha huoshwa au atoaye hupokea. Kutoa na kupokea zawadi ni jadi yetu Watanzania.

Mgeni hupokelewa na kukirimiwa anapokuwa na mzigo kichwani, kule kwetu Kigoma tunaita “umugemu”. Kadhalika wanasiasa hutuletea zawadi. Hutuletea kofia, pombe na tisheti. Hakika ni zawadi za kipumbavu na madhara yake huwa nikulia na kusaga meno kwa muda wote waongozapo.

Leo ndugu zangu walimu,mmeteseka vya kutosha, mmepigikika vya kustosha, mmedhulumiwa vya kutosha, wengi wenu malipo ya likizi yamebaki msamiati, gharama za matibabu zimelipwa na Mungu hakika ni malipo ya zawadi za wanasiasa. Mmetuvurugia mfumo mzima wa elimu kwamba mnalipa kisasi kwa mgomo wenu wa kimya kimya bila kujua mnaumiza watoto wenu.

Watoto wa wabaya wenu hawasomi kwenye shule mnazofundisha. Wanasoma “international schools”, shule ambazo ada ya mwanafunzi mmoja ni mshahara wako wa mwaka mzima. Maisha yenu ndugu walimu hayataboreshwa kwa migomo baridi bali kwa kuwaondoa viongozi dhalimu madarakani. Muda ndiyo huu, kama mnataka maisha mema kafanyeni uamuzi wa busara.

Ndugu zangu wakulima, poleni sana kwa yanayowasibu. Mliamini katika kile kibwagizo cha KAMA MNATAKA MALI MTAYAPATA SHAMBANI na kwa moyo wote shambani mkahudhuria. Kimechowapata hata shetani anasikitika. Pembe jeo kwenu imekuwa sawa na kuchoma sindano ya kushonea viraka kwenye kidonda. Mmeingia katika mikopo mikubwa mkitegemea baada ya kuuza basi mlipe mikopo hiyo na nyie kufurahia matunda ya kazi ya mikono yenu. Kimechotokea kimewashangaza wenyewe. Mazao yenu yamekosa soko, madeni yamewabana na sasa wengi mnatamani kufa badala ya kuishi.
 Watoto wenu wamepoteza dira kwa sababu ya usaliti wenu wenyewe kwa kuchagua viongozi balaa. Mliona zawadi ni bora kuliko uzao wenu. Mkawachagua viongozi makenge kwa zawadi ya kofia, pombe na tisheti. Lakini kwa kuwa matatizo ni daraja basi tumieni daraja hilo kuvuka ng’ambo kwa maana ya kwamba achaneni na viongozi waliowatesa kwa muda mrefu. Msiwarudishe madarakani. Muwavuke. Muda ndiyo huu.

Ndugu zangu wafanyabiashara kilio chenu wote tumekisikia. Mmejitahidi kuwekeza katika biashara kwa lengo la kupata faida na kuishi maisha mazuri. Wengine mmechukua mikopo yenye riba kubwa mkiamini kabisa mtarejesha na hatimaye kupiga hatua. Lakini matokeo yake yamewashangaza. Mmelazimishwa kulipa kodi pasipo kupata faida. Mkajikuta mashakani kufilisika. Mkasemeza,
“ Na sasa tuandae mgomo wa nchi nzima kuukataa mfumo huu wa kulipishwa kodi kinyampala”. Harakati zenu zikawa mbio za sakafuni. Mkatiwa msukosuko hatimaye mkasalimu amri. Matokeo yake wengi mmejitoa katika biashara na wengine mmeishia kumlilia Mungu. Msilie, maana hata Mungu mwenyewe kasema mnaangamia kwa kukosa maarifa.
Kuwaondoa madarakani viongozi washenzi ndiyo maarifa yenyewe. Fanyeni hivyo kwa kuwapigia kura za hapana. Muda ndiyo huu. Mnawafahamu. Nendeni mkachague viongozi wenye utu badala ya kujifanya mko “busy”.
Nawajua. Wakati wakulima wenzangu wanauza haki yao ya kupiga kura kwa zawadi ya pombe, tisheti na kofia, wafanyabiashara huwa mnauza haki yenu kwa kujifanya mko “busy” na biashara zenu.

Ndugu zangu wanafunzi hasa wa Elimu ya juu mnanihuzunisha sana kwa jinsi mmevyoishi. Kuanzia mnavyokula mpaka kulala ni majanga. Wengi mnalala “stoo”, wengine mnalala kwenye nyumba zilizokuwa na mabanda ya kuku na mnalazimishwa kulipia kodi kubwa. Katika hili mmekosa mtetezi. Wengi mmeshasahau mlo wa mchana mnaita eti pasi ndefu kufikiria mnaweza kupambana na mziki wa kitabu cha chuo kikuu.
Acheni kujidanganya. Lakini linalonitoa machozi zaidi ni wengi wenu mmetoka familia duni sana kiasi kwamba kamkopo hako hako unakokapata baada ya kutoka jasho tena kwa kuchelewa ugawane na wadogo zako au wazazi wako. Mnatia huruma nyie? Lakini mnashangaza pia. Kwa sababu ya ukata wengi wenu mnamaliza shahada ya kwanza humjawahi kununua kitabu hata kimoja. Kazi kutoa “copies” tu! “Unagraduate” na “box” limejaa “miscopies” tu. Darasa zima kitabu “origino” anacho mwalimu tu. Unapitia mfumo huu goigoi wa elimu na kutegemea kupambana kwenye soko la ajira na mtoto wa kigogo aliyesoma “Oxford University”.

 Saana utaishia kuchekesha wakati wa usaili. Fedheha hii ni malipo ya makosa tuliyoyafanya ya kuchagua viongozi dhalimu. Jitokezeni basi katika chaguzi hizi.

Ndugu zangu machinga, leo hii mnaitwa uchafu na wale wale mliowachagua wakawatete. Mmejaribu kuukataa ushenzi kwa maandamano ya amani lakni cha moto mkakiona. Yaani mlisahau kama nchi yetu ni ya ajabu sana. Yaani maandamano ya amani, watu wanapigwa. Sasa sijui amani ndiyo kipigo? Tunajua wengi mmepoteza mali zenu na kuamua kurudi vijijini kwenda kuwa mafukara kwa sababu mliamini kudai haki zenu kwa maandamano ya amani.

 Labda tu niwakumbushe kwamba hapa nyumbani maandamano ni mwiko ila mnauhuru wa kufanya maamuzi mara moja tu kila baada ya miaka mitano. Na pale mnapokosea ndiyo kilio na kusaga meno vinatokea. Muda ni huu,msirudie kosa. Jitokezeni mkachague viongozi bora. Ni bora kuchagua kiongozi mbovu kuliko kumrudisha kiongozi aliyekutesa kwa kipindi chote hicho!

Ndugu zangu waendesha bodaboda mnafanya kazi nzuri sana ya kurahisisha usafiri nchini lakini mnanyonywa kweli. Kutwa nzima kushinda kwenye makoti makubwa, yenye kujaa kila aina ya vumbi na jasho. Lengo lenu ni kujikwamua katika maisha, lakini kinyume chake mmebaki kuwindwa na askari wa usalama barabarani mithili ya suala na simba nyikani.
Matokeo yake mnakwenda mwendo kasi ili kuwakwepa wabaya wenu na kuishia kuvunjika miguu na kwenda kutaabika mikonoi mwa madaktari waliokata tamaa na maisha! Yote haya ni kwa sababu mlikosea katika uchaguzi ulio pita. Mlichagua makenge mkidhani ni viongozi. Msirudie kosa, waondoeni madarakani waliowaumiza.

Madakatari pamoja na kusoma kwenu kwa miaka mingi, mmeshindwa kuonesha umahiri kwa sababu mazingira ya kazi si rafiki. Mapato yenu yamekwenda tofauti na mategemeo yenu. Matokeo yake mmekuwa wenye hasira kwa wogonjwa. Vinywaji vikali vimekuwa faraja kwa ndugu zangu madaktari. Inasikitisha.
Mmekuwa mkitufundisha kanunu za afya bora huku mkiwa wa kwanza kuzivunja. Eti Daktari mmoja hawezi kufanya upasuaji bila kupata fanta moja ya gongo na fegi mdomoni. Ebo! Msikubali hawa waliowafanya hivi kurudi madarakani.

Ndugu zangu wavuvi huko kanda ya ziwa na kwingineko, poleni kwa kuitwa wanaharamu kwa kutumia nyenzo haramu za uvuvi kami vile nyavu. Unajua mambo mengine yanashangaza. Kwani nyavu hivi zinaingiaje nchini? Si wao wenyewe? Viwanda vya kutengeneza nyavu si vya kwao? Kwa nini asikamatwe anayezitengeneza? Huu ni uonevu. Nvyavu nenu zinachomwa bila fidia. Mnaingia hasara. Maisha mnayaona machungu na cha moto mnakipata. Mwisho mnakata tamaa na kumwachia Mungu. Acheni kumtwika mizigo Mungu wangu. Yote haya mmeyasababisha wenyewe kwa kuchagua viongozi dhalimu. Pengine mateso hayo mnayoyapata ni ishara nzuri kwamba muamke na kusema basi inatosha. Msimu ndiyo huu. Jitokezeni mkachague viongozi bora kwa maisha bora ya wavuvi wote Tanzania.

Kwenu wafugaji. Mmejikuta katika vita kubwa ndani ya nchi yenye amani. Kila kukicha mnamwaga damu huku wenye jukumu la kuwalinda wakitafuna mishikaki ya kuku huku wakiangalia Asernal ikimenyana na Man U. Maisha yenu ya ufugaji yamekuwa magumu. Malisho kwa wanyama wenu imekuwa balaa. Askari wa mbugani wamewafanya nyie vyanzo vyao vya mapano.
 Mnatozwa faini kubwa pasipokupata msaada. Asira yenu ikiwaka mnajikuta katika vita na wakulima. Sikilizeni. Hakuna haja ya kupigana na mkulima. Huyo siyo adui yenu. Adui yenu ni yule aliyewapa tisheti, kofia na pombe mkampa kura. Muondoeni huyo! Muda umefika.

Ndugu zangu waandishi wa habari, poleni kwa adha za kila aina wakati mkitekeleza majukumu yenu ya kila siku. Kwanza mmetukanwa kwamba mu wavivu wa kufikiri. Hiyo haikutosha, mmeendelea kupokea vitisho, vipigo na mpaka wengine kupoteza baadhi ya viungo vyao na hata kufa. Leo ni vilema na wakati hawakuzaliwa hivyo. Wanaotenda yote haya wako pale kwa sababu ya kura zenu. Wamiliki wamendelea kuwatumikisha kana kwamba nyie si lolote si chochote. Kupata kwenu ujira ni mpaka mwajiri wako aone inafaa. .
 Serikali yenu inajua kabisa mnaonewa, sasa kwa kuwa ni mpango wake kuwa na media dhaifu basi mnaishia kulia pasipo msaada. Fanyeni uchaguzi wenye busara na hakika mtapona.

Ndugu zangu watanzania, hakikia tumepigika, tuko katika wakati mgumu. Rasilimali zetu zinatafunwa kwa kasi sana na viongozi tuliowaweka madarakani. Kulindana kwao ndiyo fasheni. Mahakama tuliyonayo ndiyo kabisa haina meno. Kumbe ni wakati muafaka sasa kutorudia kosa.
Tuhakikishe washenzi wote hawarudi madarakani. Msimu ndiyo huu. Tunaanza na serikali za mitaa, na baadaye tutamalizia na uchaguzi mkuu wa rais na wabunge. Chondechonde, tukifanya kosa tutazikwa wazima. Tufanye maamuzi pasipo msukumo wa tisheti, kofia na pombe.