Na Amani Mbwaga Mafinga- Iringa
Mkuu wa Mkoa Iringa
Mhe Amina Juma Masenza ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kupata
hati safi katika mkutano maalumu wa baraza la Madiwani lililojadili majibu ya
hoja za mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali (CAG) kwa mwaka
unaoishia tarehe 30 Juni 2017, mkutano huo umefanyika leo katika Ukumbi wa
Halmashauri ya mji Mafinga Mkoani Iringa.
“Kwa namna ya
kipekee nachukua fursa hii kuipongeza Halmashauri ya Mji wa Mafinga kwa kupata
hati safi na pia nazipongeza Halmashauri zetu zote 05 za Mkoa wetu wa Iringa
kwa kupata hati safi za ukaguzi zilizoishia Juni 2017, kwani kitendo hiki kimeupa
heshima kubwa Mkoa wetu, nawashukuru sana na hongereni waheshimiwa madiwani na
watendaji wa serikali kwa kazi nzuri” alisema Mhe Masenza.
Katika mwaka wa
Fedha ulioishia Juni 2017 Halmashauri ya Mji wa Mafinga imepata hati ya
kuridhisha kutokana na ukaguzi uliofanywa na Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti mkuu
wa hesabu za serikali, mkaguzi alianisha mapendekezo mbalimbali na kushauri
hatua zinazotakiwa kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na kutaka majibu ya hoja
alizotoa.
Aidha Mhe Masenza
ameliambia baraza la Madiwani kwamba tayari serikali imeshatoa Fedha kwa ajili
ujenzi wa Miundombinu ya shule mbalimbali katika mkoa wa Iringa na Halmashauri
ya mji wa Mafinga ni moja kati ya halmashauri zilizonufaika na Fedha hizo kwa
ajili ya kupokea kidato cha tano mwaka huu 2018.
“Miongoni mwa shule
zilizokwisha pokea fedha hizo ni Shule ya Sekondari Changarawe Tshs
80,000,000/= kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 4 na Tshs 150,000,000/= kwa ajili ya
Mabweni, vilevile Shule ya Sekondari JJ Mungai nayo imepokea Tshs
80,000,000/= kwa ajili ya Madarasa na Tshs 150,000,000/= kwa ajili
ya mabweni, Ujenzi huu ni kutoka katika Force Account na Mwisho wa
utekelezaji wa ujenzi huo ni tarehe 30 Agosti 2018” Alisema Mhe Masenza.
Kwa upande wake Mkuu
wa Wilaya ya Mufindi Mhe Jamhuri William akitoa salamu za Wilaya kwa Mkuu wa
Mkoa Iringa, alisema “Kwa Ujumla mkuu wa mkoa wewe mwenyewe ni lazima useme na
utupe maelekezo ili baraza hili liweze kutekeleza na tupo tayari kupokea
maelekezo yako na kuyafanyia kazi”
Aidha Mwenyekiti wa
Halmashauri ya Mji wa Mafinga Mhe Charles Makoga amewataka watumishi wa
serikali kuongeza umakini katika kazi na kutimiza wajibu wao ili hoja
ndogondogo zilizojitokeza zisijirudie tena.
Kwa upande mwingine Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Bi. Saada Mwaruka aliliambia baraza kuwa katika
mwaka wa Fedha 2016/2017 ofisi yake imeandaa majibu ya hoja na ushauri
mbalimbali katika hoja zilizotolewa na Mkaguzi ambapo majibu yatahakikiwa na
ofisi ya mkaguzi ili kuweza kumaliza na kuendelea kutekeleza ushauri
uliotolewa.
“Majibu hayo
yamewasilishwa leo hii katika mkutano wa baraza la madiwani ili kuweza kupata
ushauri ambao utatumika katika kuboresha utendaji wa kazi na kupunguza au
kumaliza kabisa hoja mbalimbali zilizotolewa na ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti
mkuu wa Hesabu za Serikali” alisema Mwaruka.
Mkutano huo maalumu
wa baraza la madiwani kujadili hoja za mdhibiti na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali
kwa mwaka unaoishia 30 Juni 2017 ni utekelezaji wa agizo alilolitoa Waziri
mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kasim Majaliwa kwenye kikao na Wakuu
wa Mikoa kilichofanyika tarehe 29 April 2017, ambapo aliwataka wakuu wa
Mikoa kote nchini kufuatilia kwa karibu
ili kuhakikisha Halmashauri zote zinafanyia kazi ipasavyo hoja zote
zilizotolewa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2016/2017
na zile zilizotolewa miaka ya nyuma.
Aidha Mhe Waziri wa
Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi kupitia barua yake ya tarehe 20 April 2018
alisisitiza kuwa wakuu wa mikoa kote nchini wanatakiwa kushiriki kikamilifu
katika vikao maalumu kwenye Halmashauri wanazosimamia kwa lengo la kujadili hoja
na Mapendekezo yote yaliyotolewa na Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa Hesabu za
Serikali kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
HABARI KATIKA PICHA
Mkuu wa Mkoa Iringa akisoma Hotuba wakati wa mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji Mafinga. |
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Akiteta jambo na Katibu Tawala (RAS) Wa Mkoa Wa Iringa Bi Wamoja Ayubu Dickolagwa Kulia Kwake ni Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jahuri William. |
Mkuu wa Wilaya Mufindi Mhe Jamhuri William akitoa salamu za wilaya ya Mufindi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa wakati wa Mkutano maalumu wa Baraza la madiwani Halmashauri ya Mji wa Mafinga |
Mkurugenzi wa Mji wa Mafinga Bi Saada Mwaruka akijibu baadhi ya hoja zilizoulizwa na waheshimiwa Madiwani. |
Baadhi ya Waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga wakifuatilia kwa makini Majibu ya Hoja za Mkaguzi na Mdhibiti mkuu wa Hesabu za wa seikali. |
Baadhi ya Wataalamu wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Wakifuatilia kwa makini Maelekezo ya Mkuu wa Mkoa Kuhusu hoja zilizotolewa na CIG tayari kwa kuzitekeleza ipasavyo na kwa wakati muafaka |
Mheshimiwa Diwani wa Kata ya Sao Hill Denis Kutimile akichangia hoja katia mutano maalumu wa Baraza la Madiwani Halmashauri ya Mji wa Mafinga. |
Afisa Kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Iringa anaesimamia serikali za mitaa nae akichangia hoja(Picha na Amani Mbwaga) |
Mtunza Hazina wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Ramadhani Mbuguyu akijibu baadi ya hoja za idara yake wakati wa mkutano maalumu wa Baraza la Madiwani |
Mkaguzi wa ndani Halmashauri ya Mji wa Mafinga Erick Ntikahela akitolea ufafanuzi baadhi ya hoja. |
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Mji wa Mafinga Voster Mgina nae akijibu baadhi ya hoja zinazohusu elimu. |