Thursday, October 10, 2013

Fedha za Mrisho Ngassa zakamatwa






UNAZIKUMBUKA zile Sh45 milioni ambazo, Mrisho Ngassa alipeleka kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kuilipa Simba? Zimezua utata.

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imeingilia kati malipo ya Sh 45 milioni ambazo Mrisho Ngassa aliilipa Simba na kulitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuzuia kwa muda mpaka zilipiwe kodi.
Hata hivyo, tayari TFF imeilipa Simba Sh 40 milioni, huku ikibakiza Sh5 milioni wakati bado inasubiri maelekezo kamili ya TRA.
Ngassa alipeleka hundi ya Sh45 milioni kwa TFF ili wailipe Simba wiki iliyopita baada ya kuamriwa na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji kufanya hivyo kutokana na kusaini mkataba wa klabu mbili.
Hata hivyo, Simba imelipwa Sh 40 milioni tu, huku TFF ikishikilia hundi ya Sh5 milioni mpaka itakapopata maelekezo kamili ya TRA.
Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah, aliithibitishia Mwanaspoti jana Jumatano kuwa wamepewa maagizo na TRA kuwa wasiilipe Simba fedha hizo mpaka zikatwe Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT),
Osiah alisema alishaandikia hundi ili kulipa fedha hizo, lakini kutokana na maagizo hayo ya TRA, wamelipa Sh 40 milioni huku kiasi kilichobaki wakisubiri maagizo mengine ya TRA.
Alisema alikuwa amepanga kuandika barua TRA ili kupata ufafanuzi kwani anachojua ni kuwa Simba haijasajiliwa katika malipo ya VAT na klabu pekee iliyosajiliwa kwa mfumo huo Tanzania Bara ni Yanga. Mchezaji huyo amecheza klabu zote kubwa nchini ambazo ni Simba, Yanga na Azam
“Katika barua nataka kupata ufafanuzi kwa sababu sisi (TFF) si mawakala wa TRA kwa Simba, sisi ni mawakala wa TRA kwenye mapato ya milangoni ya timu zote, naona tayari Simba wamelipwa Sh 40 milioni kiasi kilichobaki tunasubiri kupata maelekezo ya TRA,” alisema.
Katika hatua nyingine, Osiah alifafanua kuwa alikuwa amepata barua ya Simba iliyoandikwa na Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Evodius Mtawala, ikiagiza kuwa fedha hizo si za Simba ila anapaswa kulipwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hanspoppe.
“Simba wamesema fedha hizo alipwe Hanspoppe. Hata hivyo tulikuwa tumeshawalipa Simba,” alisema.

No comments:

Post a Comment