Askari Polisi wa kike mkoani hapa amefariki dunia papo hapo baada ya kukanyagwa na tairi la gari na kupasuka kichwa.
Askari huyo Rehema James (30), alikutwa na umauti juzi wakati akiwa amepanda katika usafiri wa baiskeli maarufu kama daladala eneo la Kambarage mjini Shinyanga.
Watu walioshuhudia tukio hilo waliliambia gazeti hili kuwa, askari huyo alikuwa amepakizwa kwenye baiskeli ndipo gari hilo lilipomgonga na kufariki dunia.
Walisema waliona gari aina ya scania lenye namba za usajili BLQ 546 likimgonga askari huyo na kufariki dunia papo hapo na ubongo wake ukiwa nje huku mwendesha baiskeli akifanikiwa kuruka kutoka kwenye baiskeli hiyo na kukimbia.
Walieleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendesha baiskeli kutaka kulipita gari hilo wakati likikata kona na Rehema alijigonga kwenye tela la gari na kuanguka chini ambapo tairi lilimpitia na kumpasua kichwa.
Utingo wa gari hilo, God Makunga, alisema wakati gari lao likikata kona ghafla alisikia kishindo kikubwa kwenye gari na baada ya kushuka akamkuta mwanamke huyo amekanyangwa na tairi la gari.
Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga ACP Kihenya Kihenya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Alisema Rehema alikuwa abiria kwenye baiskeli na baadaye akagongwa na gari hilo, na tayari mwili wake umesafirishwa kwenda nyumbani kwao jijini Dar es Salaam kwa mazishi yanayotemewa kufanyika leo.
Alisema chanzo cha ajali hiyo kinachunguzwa na jeshi la polisi linaendelea kumtafuta dereva wa gari hilo kwani alitoroka mara baada ya ajali kutokea na kuacha gari lake eneo la tukio.
Kamanda Kihenya ametoa wito kwa watumiaji wa barabara wakiwamo madereva wa magari na waendesha baiskeli kuwa makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabaranisource: gumzo la jiji.
Read more: http://talkbongo.blogspot.com/2013/08/inatisha-askari-wa-kike-afariki-dunia.html#ixzz2b5N5VLi2
No comments:
Post a Comment