Friday, February 23, 2018

Baraza la Madiwani Mufindi lapitisha Rasimu ya Bajeti 2018/2019

               

Na Amani Mbwaga Mafinga, Iringa

Kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya wilaya mufindi leo  Februari 23, 2018 kimepitisha Rasimu ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti yake kwa  mwaka 2018/2019.

Kikao hicho Maalumu cha Baraza la Madiwani cha Kujadili, Kuridhia na Kupitisha Mapendekezo ya Bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi, Mkoani Iringa na Kuhudhuriwa na Waheshimiwa Madiwani Wabunge na Watendaji wa serikali.

Kwa mwaka 2018/19, Halmashauri ya Wilaya Mufindi inatarajia kukusanya na kutumia fedha jumla ya Tshs. 62,926,405,980.00 Bilioni.

Ambapo kiasi cha  Tsh. 45,720,685,980.00 ni matumizi  mengineyo kwa mchanganuo kwamba, mishahara ya watumishi ni Tshs.40,728,501,380.00 na matumizi ya kawaida ni Tshs 4,992,184,600.00.

Miradi ya Maendeleo itaghalimiwa kiasi cha Tshs. 17,205,720,000.00 ambapo kati ya hizo fedha za ndani ni Tshs 6,509,186,000.00 na fedha za nje ni Tshs 3,713,764,000.00.

Halmashauri ya Wilaya Mufindi kutokana na vyanzo vyake vya ndani inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya Tshs 4,162,860,000.00 sawa na asilimia 7 ya bajeti yote, hii ni ongezeko la asilimia 7 kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018.

Mchango wa jamii kwenye Miradi ya Maendeleo ni Tshs. 4,642,613,000.00 na Taasisi binafsi zitachangia wastani wa Tshs. 156,000,000.00

Lengo Kuu la Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Kutoa huduma nzuri na endelevu kwa wananchi.

Halmashauri ya Wilaya Mufindi Inatekeleza lengo hilo na pia Inatekeleza Malengo yake Makuu ambayo ni Kuimarisha Utawala Bora na Usimamizi wa rasilimali watu na fedha ili kujenga Ustawi wa jamii, Kutoa huduma bora za kijamii na kuinua uchumi wa wananchi ili kuwa na jamii inayojiamini kwa kumiliki njia kuu za uchumi na pia Kuimarisha Miundombinu ya kiuchumi na utunzaji wa Mazingira.

Katika kutekeleza Malengo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bwana Isaya Mbenje alivitaja Vipaumbele vya Halmashauri katika rasimu ya bajeti 2018/2019  iliyopitishwa na baraza la madiwani kuwa ni  Kuongeza upatikanaji  wa huduma za kukamilisha miradi ambayo haikukamilika kwa miaka ya nyuma (hasa kwenye sekta ya Elimu Sekondari na Afya). Mfano, Majengo na vifaa vya maabara,  majengo ya zahanati na vituo vya afya.

Ukarabati wa baadhi ya majengo ya shule za msingi yaliyochakaa, Kuhimiza na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuyaongezea thamani ili kukuza uchumi na kuongeza kipato kwa wananchi.

Kuimarisha misingi ya Utawala bora na ushiriki wa jamii ili kujiletea Maendeleo kwa kupambana na umasikini wa Kipato (SDG Na.1 No Poverty),Kuimarisha mifumo ya kukusanya mapato kwa njia ya kielectroc na kusimamia matumizi sahihi na yenye Tija na mwisho Kuwekeza kwenye Miradi ya kuongeza mapato ili kuweza  kujitegemea.

Aidha Kaimu Mkurugenzi Bwana Isaya Mbenje alieleza kwamba Mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2018/2019 yameandaliwa kwa Mujibu wa Sheria ya Bajeti na 11 ya mwaka 2015 kifungu cha 18 (1) (a-c) na (2) kifungu cha 22 pamoja na kanuni yake na 17d (3) (a-d), inamtaka Afisa Masuhuli wa Halmashauri Kuandaa na Kuwasilisha Mpango wa Bajeti ya Halmashauri kila mwaka wa Fedha.

Aidha Memoranda ya Fedha ya mwaka 2009 inataka Halmashauri kuidhinisha Bajeti yake miezi miwili kabla ya kuanza kwa mwaka wa Fedha husika, ambapo tayari suala hilo limetekelezwa na Halmashauri ya wilaya ya Mufindi hadi kufikia kupitishwa kwa Bajeti hiyo.

Kwa upande Mwingine Mapendekezo ya Bajeti hii imeandaliwa kwa kuzingatia Mwongozo wa bajeti wa mwaka 2018/2019, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala –CCM ya 2015/2016-2019/2020, Mpango wa pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/2017, Malengo 17 ya maendeleo endelevu (SDGs), Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Maelekezo ya        Ki-sekta na Mpango Mkakati wa Halmashauri wa Maendeleo wa Miaka Mitano.

“Rasimu hii ya Mpango wa Bajeti ya Halmashauri ni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Miradi ya Maendeleo kwa mwaka 2018/2019, bado yanaendelea kujadiliwa na kupatiwa ushauri kwenye vikao vya ngazi ya Mkoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI Pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango” alisema Kaimu Mkurugenzi Bwana Isaya Mbenje.

Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mhe Festo Mgina aliwashukuru Wataalamu na waheshimiwa madiwani kwa michango yao mizuri na mapendekezo waliyoyatoa ili kuboresha na kuipitisha bajeti na kuwataka waendelee na moyo huo wa umoja na ushirikiano kwa maendeleo ya Wananchi.

Aliongeza pia Bajeti hiyo wamezingatia sana Mapato ya ndani ili kuhakikisha asilimia 60% zinapelekwa kwenye miradi ya Maendeleo.

Aidha amewataka watendaji wa Halmashauri hii kujipanga kwa ajili ya utekelezaji na kutaka kuendelea kuvumbua vyanzo vingine vya Mapato.

“Mkurugenzi wewe pamoja na timu yako tuendelee kuchapa kazi, tunasifa ya Ushirikiano kati ya timu ya Madiwani na Timu yako, tuendeleee kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano Kwani Wananchi wanatarajia sana baraza hili hivyo ni lazima tuwaletee maendeleo” Alisema Mheshimiwa Mgina wakati akihitimisha kikao hicho cha Bajeti.


                                          HABARI KATIKA PICHA
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Halamashauri ya Wilaya Mufindi Mhe Festo Mgina Akiongoza Kikao Maalumu  cha Baraza la Madiwani cha  Kupitisha Rasimu Bajeti ya Mwaka 2018/2019 (Picha na Amani Mbwaga)
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Isaya Mbenje akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Madiwani wakati wa kujadili na Kupitisha Rasimu ya Bajeti ya mwaka 2018/2019 (Picha na Amani Mbwaga)


Baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wakifuatilia kwa makini Uwasilishaji wa Rasimu ya Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi (Picha na Amani Mbwaga)

Diwani wa Kata ya Madabulo Mhe Enrich Nyeho akichangia Rasimu ya Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi.
Mganga Mkuu Wilaya ya Mufindi (DMO) Dkt Fredrick Mugalura akijibu baadhi ya Hoja zilizotolewa naWaheshimiwa Madiwani Wakati wa Kujadili Rasimu ya Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya Mufindi 2018/2019.
Kaimu Afisa Ardhi Maliasili na Mazingira Bwana Shabani Ardha nae akitoa maelezo kwa baraza la madiwani kwa baadhi ya hoja zilizotolewa na waheshimiwa Madiwani.
Meza kuu ikiendelea kwa makini kuchambua nakupitisha Rasimu ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya Mufindi mwaka2018/2019. (Picha zote na Amani Mbwaga)

Thursday, February 1, 2018

PUBLIC RELATIONS & MARKETING MANAGER'S: TAZAMA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2017/2018

PUBLIC RELATIONS & MARKETING MANAGER'S: TAZAMA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2017/2018: Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya kidato nne ambapo ufaulu umeongezeka kwa asilimia saba. Shule  iliyoshika...

TAZAMA MATOKEO YA KIDATO CHA NNE 2017/2018


Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya kidato nne ambapo ufaulu umeongezeka kwa asilimia saba. Shule  iliyoshika namba moja inatoka Mbeya.

Jumla ya watahiniwa  385, 767 walisailiwa kufanya mtihani kidato cha nne mwaka 2017, kati yao 287,713 sawa na asilimia 77.09 ndio wamefaulu ambapo wasichana ni  143,728 sawa na asilimia 75.21 na wavulana 143,985 sawa na asilimia 79.06.


Akitangaza matokeo hayo leo Januari 30, 2018 Katibu Mtendaji wa Necta,  Dk Charles Msonde amesema mwaka 2016 watahiniwa waliofaulu walikuwa 277,283 sawa na asilimia 70.09.

Amesema matokeo ya watahiniwa 50 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya baadhi ya masomo ya mitihani hiyo, watapata fursa hiyo mwaka huu.

"Watahiniwa 77 wa shule ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani watapata fursa mwaka 2018," amesema Dk Msonde.

Dk Msonde amesema watahiniwa 265 waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani  matokeo yao yamefutwa huku mtahiniwa mmoja akiandika matusi katika karatasi yake ya majibu.
Bofya hapa chini kuona matokeo


Chanzo: Muungwana 

Tuesday, September 19, 2017

Vijana wanaopitia JKT hufanikiwa katika Maisha.


Na Amani Mbwaga                                                15 Septemba 2017 Mafinga, Tanzania.
Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa Mhe.Amina Masenza akikagua gwaride la vijana Mujibu wa Sheria Op Tanzania ya Viwanda 2017 katika kikosi cha Jeshi Mafinga JKT.
 (Picha na Amani Mbwaga)
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa Iringa Mhe Amina Juma Masenza wakati wa Kufunga Mafunzo ya awali ya Kijeshi kwa Vijana wa JKT Mujibu wa Sheria kundi Tanzania ya Viwanda katika Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa Mafinga (JKT)  kilichopo Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa.

“Uzoefu unaonesha kuwa vijana wote wanaopita JKT hufanikiwa katika Maisha yao kutokana na kuwaandaa vijana kuwa na Uzalendo Uadilifu Ukakamavu, Utii, Uhodari, Uaminifu na kwa kujifunza shughuli mbalimbali za uzalishaji mali” alisema Mhe Masenza.

Pamoja na kwamba JKT halitoi ajira kwa vijana lakini mafunzo haya waliyoyapata ni sawa na ajira, kwani wamejifunza, Kilimo Ufugaji, utunzaji wa mazingira na shughuli nyingine za mikono, hizo ni fursa za ajira zitakazowafanya waweze kujitegemea katika hali yoyote.

Aidha Mhe Masenza alitoa wito kwa vijana wahitimu kwamba mafunzo ya Kijeshi waliyoyapata yakaimarishe amani na utulivu wa nchi na jamii kwa ujumla.

Pia amewataka vijana wakadumishe sifa nzuri ya Mafinga JKT na Jeshi kwa Ujumla.

Naye Mwakilishi wa Mkuu wa JKT Meja Jenerali Michael Isamuhyo na Mkurugenzi wa ustawi wa Jamii JKT Kaimu Kanali AS Kagombola alisema mafunzo hayo ya Jeshi la Kujenga Taifa  yamelenga kuwaanda vijana wa Kitanzania kuwa na moyo wa Uzalendo, Kupenda kazi za Mikono Kujituma, Kuilinda, Kuitetea na Kuifia nchi yao.

Aidha katika kutekeleza majukumu makuu ya JKT Uzalishaji Mali, Mafunzo ya awali ya Kijeshi na Malezi kwa vijana ikiwemo stadi za maisha na stadi za kazi kuwa kielelezo cha kutosha kwa jamii.

Pamoja na majukumu yote hayo JKT imeendelea kuboresha miundombinu ya Vikosi mbalimbali vya Jeshi ili kuweza kuongeza idadi kubwa ya Vijana kujiunga na Mafunzo hayo muhimu kwa Taifa

Kwa upande wake Mkuu wa Kikosi cha Mafinga JKT Luteni Kanali Hamisi Maiga aliwataka vijana kutoyumbishwa na watu wasiolitakia mema taifa letu bali wazingatie kiapo chao cha Utii, Uhodari na Uaminifu
“Fanyeni mambo yenye tija kwa taifa na yasiyo na tija achaneni nayo” alisema Luteni Kanali Hamisi Maiga

Waasisi wa Taifa letu waliona umuhimu wa vijana wa kitanzania kupata mafunzo na kutoa malezi kwa lengo la kutetea na kulilinda taifa ili kuendana na mila na desturi na utamaduni wa Taifa letu .

JKT ilipewa jukumu la malezi kwa vijana kwa lengo la kuondoa  makovu yaliyoachwa na wakoloni ambayo yalianza kuenezwa kwa vijana wasomi kwa wakati huo.

Kabla ya kuanzishwa chombo hiki vijana wale wasomi walijengewa kasumba ya wao kuwa bora kuliko vijana wengine  waliopata elimu ya kiwango cha chini, hali hii ilipelekea mgawanyiko wa matabaka ya kielimu.

Kwa kuona umuhimu huo JKT Ilianzishwa rasmi na kuanza kutoa Mafunzo ya vijana wasomi na wasiosoma bila kubaguana, baadae JKT iliongezewa jukumu la uzalishaji mali na Ulinzi.

JKT ilianzishwa Julai 10, 1963 katika uwanja wa ndani wa michezo wa Taifa (Indoor Stadium) majira ya saa kumi na moja jioni, ambapo vijana 11 kutoka wilaya 11 wakiwa makatibu wa vijana TYL walijiunga kwa mafunzo katika kambi ya JKT Mgulani jijini Dar es salaam

Sanjari na hilo Mwaka 1964 ilitungwa Sheria ya JKT (The National Service Act) ambayo ilimpa madaraka Mkurugenzi wa JKT Kuandikisha Vijana wa Kujitolea Kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa.

Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho mwaka 1966 na 1967 ili kuwawezesha vijana waliokuwa wakihitimu elimu ya Sekondari ya Kidato cha nne na Sita Kujiunga JKT Kwa mujibu wa Sheria.

Mafunzo haya ya JKT kwa vijana wa Kujitolea na Mujibu wa sheria yaliendelea kwa ufanisi mpaka mwaka 1994, serikali ilipositisha kwa sababu mbalimbali za Kiuchumi.

Kusitishwa kwake, watafiti walisema kuwa jamii ilishuhudia mmomonyoko mkubwa wa maadili na uwajibikaji usiozingatia nidhamu, hasa kada ya vijana.

Mmomonyoko huo ulizusha malalamiko ya makundi mbalimbali ya jamii yakitaka kurejeshwa kwa taasisi hiyo, hali iiyowezeshwa na Serikali ya Awamu ya Tatu chini ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Benjamini William Mkapa, Kuyahuisha Mwaka 2001 kwa Vijana wa Kujitolea .

Mnamo machi 26 mwaka 2013, Serikali ya Awamu ya nne chini ya Amiri Jeshi  Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete alizindua upya mpango wa Mafunzo ya JKT kwa vijana wa Mujibu wa Sheria.

Hadi sasa katika Serikali hii ya awamu ya tano ya Rais na Amiri Jeshi Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli imeendelea kutoa mafunzo hayo ya vijana wa mujibu wa Sheria na Kujitolea kwa Kiwango cha hali ya juu hii inatokana na kurejeshwa kwa baadhi ya Makambi ya JKT yakiwemo ya Makuyuni, Mpwapwa, Itaka, Milundikwa, na Luwa.


Mgeni Rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Amina Juma Masenza akipokea Salamu ya heshima kutoka katika gwaride la vijana Mujibu wa sheria Op Tanzania ya Viwanda 2017 katika kikosi cha Jeshi Mafinga (Picha Na Amanin Mbwaga)










Baadhi ya  ndugu, jamaaa na wananchi wa mji wa Mafinga wakifuatilia kwa makini Paredi ya Vijana wa JKT Mafinga

Kijana wa JKT Mujibu wa Sheria Service Man Mshindi wa Kwata akipokea zawadi

Kijana wa JKT  Service Girl Mshindi wa Usafi akipokea zawadi

Paredi Ikitoka nje ya Uwanja





Kikundi cha Kwaya ya Vijana Wa JKT Mujibu wa Sheria 2017 


Kikundi cha Ngoma cha Mafinga JKT






Kikundi cha Sarakasi cha Mafinga JKT






Kikundi cha Singe cha Vijana Mujibu wa Sheria OP Tanzania ya Viwanda Mfinga JKT 2017


Kikundi cha Kareti Op Tanzania ya Viwanda Mujibu wa Sheria 2017





Vijana wa JKT Mafinga wakionesha uwezo wao Mkubwa wa Kareti


Mgeni Rasmi Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Amina Juma Masenza akimshukuru  Afisa Habari na Uhusiano wa Mafinga JKT Koplo Elias Mbega mara baada ya Kukabidhiwa zawadi iliyoandaliwa na Ofisi ya Habari na Uhusiano Mafinga JKT (Picha na Amani Mbwaga)



Kijana wa wa Kikundi cha Sanaa Mafinga JKT Service Man Paul Kwayu akimkabidhi Mkuu wa Kikosi Luteni Kanali Hamis Maiga CD ya Kwaya ya Kikosi Mafinga JKT.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa Mhe Amina Juma Masenza akihutubia Hadhara iliyojitokeza katika Mahafali ya Vijana wa Mujibu wa Sheria Op Tanzania ya Viwanda 2017
Mwakilishi wa Mkuu wa JKT na Mkurugenzi wa Ustawi wa Jamii JKT Kaimu Kanali AS Kagombola kitoa Salamu za  Mkuu wa JKT

Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Mafinga JKT Luteni Kanali Hamis Maiga akiwaasa Vijana wa JKT


Mgeni rasmi akiwa katika Picha ya Pamoja na aadhin ya Maofisa na askari wa  Kikosi cha Jeshi Mafinga


Mkuu wa Mkoa akia katika Picha ya Pamoja na viongozi wa Vijana OP Tanzania ya Viwanda 2017 (Picha zote na Amani Mbwaga)


Kwa mawasiliano zaidi Wasiliana nasi:
Mob 0765058711
        0656632566
Email:prof.mbwaga@gmail.com