Monday, December 16, 2013

Makabiliano yazuka jeshini Sudan Kusini


Taarifa zinasema kuwa makabiliano yametokea kati ya walinzi wa Rais huku mgogoro wa kisiasa ukitokota Sudan Kusini
Milio ya risasi imesikika usiku kucha hadi asubuhi ya leo katika mji mkuu wa Sudan Kusini Juba kwa mujibu wa maafisa wa balozi na wengine waliohsuhudia tukio hilo.
Inaarifiwa mapigano hayo yametokea kati ya walinzi wa Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir.
Makabiliano yanasemekana yalianza saa nne usiku wa kuamkia leo katika kambi kuu kuu za jeshi mjini Juba na kuendelea kuwa makali kwa karibu saa moja kabla ya kundi moja kufurushwa.
Milio ya risasi ilisikika usiku kucha na kusababisha hali ya taharuki huku wananchi wakizuiwa kutoka nje.
Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, taarifa kutoka katika balozi za Marekani na Uingereza mjini Juba, zimetaka raia wa nchi zao kujizuia na kutoka nje.
Ubalozi wa Marekani umesema kuwa duru mbali mbali zinaarifu mapigano makali ya ufyatulinaji wa risasi yamesikika katika sehemu mbali mbali mjini Juba.
Mwandishi wa habari wa shirika la AFP amesema kuwa aliona wanajeshi waliokuwa wamejihami vikali wakishika doria katika barabara za Juba mapema asubuhi ya leo makabiliano makali yakiendelea katika kambi za jeshi.
Hata hivyo hakuna taarifa rasmi kutoka kwa jeshi kwani huduma za simu zimesemekana kutatizika.
Duru za kiijeshi zilisema kuwa makabiliano yalizuka kati ya kikosi cha jeshi cha Tiger, wakati moja ya kikosi ambacho kina wanajeshi wengi wa kabila la Nuer kushuku kuhusu muundo wa kikosi kingine cha jeshi ambacho wanajeshi wake wengi ni wa kabila la Dinka na hivyo kuanza kugombana kiasi cha kuanza kufyuatuliana risasi.
Inaarifiwa wanajeshi hao wa Nuer wamewafukuza wenzao wa Dinka ambao wengi wao walifuzu hivi karibuni na kuajiriwa katika serikali ya Rais Kiir.

Chanzo bbc swahili.

No comments:

Post a Comment