Na Amani Mbwaga, Mafinga
Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) imefanya ziara hivi karibuni katika Shamba la Miti Sao Hill ikiwa ni lengo la kujitambulisha kwa wajumbe wa bodi hiyo lakini pia kuona shughuli mbalimbali zinazosimamiwa na Wakala.
Akiongoza wajumbe wa Bodi hiyo Bi. Piencia Kiure mara baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi Shamba la Miti Sao Hill na kutembelea baadhi ya miradi na amepongeza juhudi hizo na kusema toka ameanza ziara hiyo katika maeneo mbalimbali ya Nyanda za Juu Kusini lakini Shamba la Miti Sao Hill ni mfano wa kuigwa kwa utendaji bora na uliotukuka.
“Nimefurahi sana taarifa zenu ni nzuri sana na pia nimeona jinsi mnavyotekeleza suala la wajibu kwa jamii yaani Corporate Social Responsibility (CSR) ikiwepo kutenga fedha kwenye bajeti yenu katika miradi ya maendeleo vijijini hapa mmenikuna zaidi kwani na mie ni mdau mkubwa sana wa (CSR) Na kwa kufanya hivyo kunasaidia sana kuwa na mahusiano mazuri baina yenu na jamii inayozunguka shamba hongereni sana”.
Kwa upande mwingine Bi. Kiure ameitaka Shamba la Miti Sao Hill Kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania Kuendelea na juhudi za Ujenzi wa Viwanda hasa vya mazao ya nyuki kwani shamba hilo limefanikiwa sana katika shughuli za ufugaji nyuki na kuwa na vifaa vya kisasa vya ufugaji nyuki na vile vya kuchakatia mazao hayo.
“Sisi kama bodi tunaona Sao Hill mna uwezo huo na tunasisitiza zaidi kuwa na viwanda hivyo kwani nia mnayo uwezo mnao na nguvu mnazo za kutekeleza agizo hilo mkisaidiana na viongozi wenu kutoka TFS Makao makuu hili litasaidia sana hata wale wafugaji wadogo wadogo kuinuka na hatimae kuwa na kipato cha kutosha kisha kuchangia uchumi wa Taifa”.
Aidha amewataka watumishi wote wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kuongeza kuboresha utendaji kazi zaidi ili kuongeza mapato na kusaidia kukua kwa uchumi wa nchi na hii inatokana na kipindi kilichopo ambapo nchi imeamua kuja na mpango wa kujitegemea zaidi na kupunguza misaada kutoka nje kutoka asilimia 42% hadi sasa kufikia asilimia 8% ili kuweza kujiendesha wenyewe kwa mapato ya ndani.
Mkurugenzi wa Usimamizi Rasilimali za Misitu na Nyuki TFS Bw. Zawadi Mbwambo amewataka watumishi wote kuendelea na juhudi kufanya kazi kwa bidii na kuendeleza misitu kwa faida ya kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.
“Nashukuku Sao Hill na TFS kwa ujumla tunaenda vizuri na ndio maana hata bungeni kwa kipindi hiki hakuna maswali mengi bungeni tayari tumeshawarahisishia kazi mawaziri wetu zaidi tunaendelea kupokea pongezi hivyo tusibweteke na sifa hizo bali tuongeze bidii za kufanya kazi kwa Uhodari ushirikiano na kwa weledi wa hali ya juu kwa manufaa ya Taifa letu”
Kwa Upande wake Meneja Shamba la Miti Sao Hill Bw. Heriberth Haulle amesema uwepo wa Shamba la Miti Sao Hill umekuwa mkombozi mkubwa kwa uchumi wa wilaya ya Mufindi na Mkoa wa Iringa kwa ujumla na kumekuwa na mahusiano mazuri baina ya shamba na wananchi wanaozunguka shamba.
Aidha shamba limekuwa likichangia sana katika shughuli za maendeleo katika vijiji vyote vinavyozunguka shamba mfano kupitia ukatishaji wa leseni za kufanya shughuli za uchakataji mazao ya misitu kwa umoja wa wadau wa mazao hayo wamekuwa wakichangia 2% ya leseni hizo na mapato yanayopatika hupelekwa katika Halmashauri zinazozungukwa na msitu ili kuchochea shughuli za maendeleo vijijini kulingana na vipaumbele vyao.
“Mpaka kufikia mwezi mei mwaka huu 2019 tumekusanya zaidi ya Milioni 315 kama mpango wa wavunaji kuchangia shughuli za maendeleo vijijini na tayari fedha hizo zilishapelekwa katika Halmashauri zinazozungukwa na shamba letu”
Mbali na hilo pia Shamba la Miti Sao Hill katika Bajeti ya mwaka 2019/2020 imetenga zaidi ya milioni 172 kwa ajili ya kutoa huduma kwa jamii hususani kujenga mabweni 02 ya Wasichana katika shule za sekondari na huu pia ni mchango wa shamba kwa jamii.
Akitoa neno la shukrani Kaimu Meneja wa TFS Nyanda za juu Kusini Bw. Ebrantino Mginje amesema maelekezo na ushauri uliotolewa na bodi kwa ziara nzima umechukuliwa na tayari hatua za utekelezaji zinaanza mara moja ili kuwa na misitu endelevu kwa faida ya sasa na baadae.
Bodi hii ya Ushauri ya Wizara kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS ilizinduliwa rasmi machi 9 mwaka 2019 Jijini Mwanza na Waziri wa Maliasili na Utalii nchini Tanzania Dkt. Hamisi Kigwangalla na inaongozwa na Mwenyekiti wake Brigedia Jenerali Mbaraka Mkeremy.
MATUKIO KATIKA PICHA
Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Wizara Kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania TFS Bi. Piencia Kiure akitoa maelekezo kwa Watumishi wa TFS Shamba la Miti Sao Hill (Hawapo pichani) |
Meneja Tarafa ya I Irundi Shamba la Miti Sao Hill Bi. Glory Fortunatus akitoa maelezo ya Bustani ya Miche Irundi wakati Bodi ya Ushauri ilipotembelea eneo hilo |
(Picha zote na Amani Mbwaga) |