Na Amani Mbwaga Mafinga, Iringa
Kikao cha Baraza la Madiwani Halmashauri ya wilaya mufindi leo Februari 23, 2018 kimepitisha Rasimu ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti yake kwa mwaka 2018/2019.
Kikao hicho Maalumu cha Baraza la Madiwani cha Kujadili, Kuridhia na Kupitisha Mapendekezo ya Bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa Fedha 2018/2019 kimefanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi, Mkoani Iringa na Kuhudhuriwa na Waheshimiwa Madiwani Wabunge na Watendaji wa serikali.
Kwa mwaka 2018/19, Halmashauri ya Wilaya Mufindi inatarajia kukusanya na kutumia fedha jumla ya Tshs. 62,926,405,980.00 Bilioni.
Ambapo kiasi cha Tsh. 45,720,685,980.00 ni matumizi mengineyo kwa mchanganuo kwamba, mishahara ya watumishi ni Tshs.40,728,501,380.00 na matumizi ya kawaida ni Tshs 4,992,184,600.00.
Miradi ya Maendeleo itaghalimiwa kiasi cha Tshs. 17,205,720,000.00 ambapo kati ya hizo fedha za ndani ni Tshs 6,509,186,000.00 na fedha za nje ni Tshs 3,713,764,000.00.
Halmashauri ya Wilaya Mufindi kutokana na vyanzo vyake vya ndani inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya Tshs 4,162,860,000.00 sawa na asilimia 7 ya bajeti yote, hii ni ongezeko la asilimia 7 kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018.
Mchango wa jamii kwenye Miradi ya Maendeleo ni Tshs. 4,642,613,000.00 na Taasisi binafsi zitachangia wastani wa Tshs. 156,000,000.00
Lengo Kuu la Mamlaka za Serikali za Mitaa ni Kutoa huduma nzuri na endelevu kwa wananchi.
Halmashauri ya Wilaya Mufindi Inatekeleza lengo hilo na pia Inatekeleza Malengo yake Makuu ambayo ni Kuimarisha Utawala Bora na Usimamizi wa rasilimali watu na fedha ili kujenga Ustawi wa jamii, Kutoa huduma bora za kijamii na kuinua uchumi wa wananchi ili kuwa na jamii inayojiamini kwa kumiliki njia kuu za uchumi na pia Kuimarisha Miundombinu ya kiuchumi na utunzaji wa Mazingira.
Katika kutekeleza Malengo hayo Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Bwana Isaya Mbenje alivitaja Vipaumbele vya Halmashauri katika rasimu ya bajeti 2018/2019 iliyopitishwa na baraza la madiwani kuwa ni Kuongeza upatikanaji wa huduma za kukamilisha miradi ambayo haikukamilika kwa miaka ya nyuma (hasa kwenye sekta ya Elimu Sekondari na Afya). Mfano, Majengo na vifaa vya maabara, majengo ya zahanati na vituo vya afya.
Ukarabati wa baadhi ya majengo ya shule za msingi yaliyochakaa, Kuhimiza na kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kuyaongezea thamani ili kukuza uchumi na kuongeza kipato kwa wananchi.
Kuimarisha misingi ya Utawala bora na ushiriki wa jamii ili kujiletea Maendeleo kwa kupambana na umasikini wa Kipato (SDG Na.1 No Poverty),Kuimarisha mifumo ya kukusanya mapato kwa njia ya kielectroc na kusimamia matumizi sahihi na yenye Tija na mwisho Kuwekeza kwenye Miradi ya kuongeza mapato ili kuweza kujitegemea.
Aidha Kaimu Mkurugenzi Bwana Isaya Mbenje alieleza kwamba Mapendekezo ya Bajeti ya mwaka 2018/2019 yameandaliwa kwa Mujibu wa Sheria ya Bajeti na 11 ya mwaka 2015 kifungu cha 18 (1) (a-c) na (2) kifungu cha 22 pamoja na kanuni yake na 17d (3) (a-d), inamtaka Afisa Masuhuli wa Halmashauri Kuandaa na Kuwasilisha Mpango wa Bajeti ya Halmashauri kila mwaka wa Fedha.
Aidha Memoranda ya Fedha ya mwaka 2009 inataka Halmashauri kuidhinisha Bajeti yake miezi miwili kabla ya kuanza kwa mwaka wa Fedha husika, ambapo tayari suala hilo limetekelezwa na Halmashauri ya wilaya ya Mufindi hadi kufikia kupitishwa kwa Bajeti hiyo.
Kwa upande Mwingine Mapendekezo ya Bajeti hii imeandaliwa kwa kuzingatia Mwongozo wa bajeti wa mwaka 2018/2019, Ilani ya Uchaguzi ya Chama Tawala –CCM ya 2015/2016-2019/2020, Mpango wa pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/2017, Malengo 17 ya maendeleo endelevu (SDGs), Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Maelekezo ya Ki-sekta na Mpango Mkakati wa Halmashauri wa Maendeleo wa Miaka Mitano.
“Rasimu hii ya Mpango wa Bajeti ya Halmashauri ni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Miradi ya Maendeleo kwa mwaka 2018/2019, bado yanaendelea kujadiliwa na kupatiwa ushauri kwenye vikao vya ngazi ya Mkoa, Ofisi ya Rais TAMISEMI Pamoja na Wizara ya Fedha na Mipango” alisema Kaimu Mkurugenzi Bwana Isaya Mbenje.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Mhe Festo Mgina aliwashukuru Wataalamu na waheshimiwa madiwani kwa michango yao mizuri na mapendekezo waliyoyatoa ili kuboresha na kuipitisha bajeti na kuwataka waendelee na moyo huo wa umoja na ushirikiano kwa maendeleo ya Wananchi.
Aliongeza pia Bajeti hiyo wamezingatia sana Mapato ya ndani ili kuhakikisha asilimia 60% zinapelekwa kwenye miradi ya Maendeleo.
Aidha amewataka watendaji wa Halmashauri hii kujipanga kwa ajili ya utekelezaji na kutaka kuendelea kuvumbua vyanzo vingine vya Mapato.
“Mkurugenzi wewe pamoja na timu yako tuendelee kuchapa kazi, tunasifa ya Ushirikiano kati ya timu ya Madiwani na Timu yako, tuendeleee kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano Kwani Wananchi wanatarajia sana baraza hili hivyo ni lazima tuwaletee maendeleo” Alisema Mheshimiwa Mgina wakati akihitimisha kikao hicho cha Bajeti.
HABARI KATIKA PICHA
Mwenyekiti wa Baraza la Madiwani Halamashauri ya Wilaya Mufindi Mhe Festo Mgina Akiongoza Kikao Maalumu cha Baraza la Madiwani cha Kupitisha Rasimu Bajeti ya Mwaka 2018/2019 (Picha na Amani Mbwaga) |
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Mufindi Bwana Isaya Mbenje akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizotolewa na Waheshimiwa Madiwani wakati wa kujadili na Kupitisha Rasimu ya Bajeti ya mwaka 2018/2019 (Picha na Amani Mbwaga) |
Baadhi ya Waheshimiwa Madiwani wakifuatilia kwa makini Uwasilishaji wa Rasimu ya Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi (Picha na Amani Mbwaga) |
Diwani wa Kata ya Madabulo Mhe Enrich Nyeho akichangia Rasimu ya Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi. |
Mganga Mkuu Wilaya ya Mufindi (DMO) Dkt Fredrick Mugalura akijibu baadhi ya Hoja zilizotolewa naWaheshimiwa Madiwani Wakati wa Kujadili Rasimu ya Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya Mufindi 2018/2019. |
Kaimu Afisa Ardhi Maliasili na Mazingira Bwana Shabani Ardha nae akitoa maelezo kwa baraza la madiwani kwa baadhi ya hoja zilizotolewa na waheshimiwa Madiwani. |
Meza kuu ikiendelea kwa makini kuchambua nakupitisha Rasimu ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri ya Wilaya Mufindi mwaka2018/2019. (Picha zote na Amani Mbwaga) |